HAKIKISHA UNALIELEWA NENO.

by Admin | 15 January 2020 08:46 pm01

 Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe..Karibu tujifunze Biblia..Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia yetu…Tabia mojawapo ya Mwovu ni kuiba angali vikiwa vidogo..Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUSIKIA NENO LA MUNGU NA KULIELEWA.Hivyo HAKIKISHA UNALIELEWA NENO.

Biblia inasema.

Mathayo 13:18  “Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.

19  Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia”.

Tabia mojawapo ya Mwovu ni kuiba angali vikiwa vidogo..Biblia imemfananisha mwovu na ndege..Ndege akipita juu na kuona mbegu zimekaa hadharani huzipitia na kuzila haraka san ana kuondoka…Kadhalika mwovu naye ni hivyo hivyo…anazunguka duniani kote kuiba mbegu za uzima zinazopandwa ndani ya mioyo ya watu kila siku. Anaziiba hizo kwasababu anajua zitakapomea na kuwa miti mkubwa zitamletea madhara makubwa sana katika ufalme wake.

Na mtu ambaye hajalielewa vizuri Neno ndiyo shabaha kubwa ya shetani.

Mwovu hawezi kulinyakua Neno ambalo mtu kalielewa…Huwa analinyakua lile ambalo Mtu hajalielewa…(yaani mtu kasikia tu lakini halijamwingia mpaka kwenye vilindi vya moyo wake).

Soma tena mstari huu..

Mathayo 13:23  “Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini”.

Umeona?..Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUSIKIA NENO LA MUNGU NA KULIELEWA. Sio kusikia tu bali pia na kulielewa kunajalisha sana.

Kikawaida hata wewe ukisikia kitu na usipokielewa ni rahisi kukipuuzia na kile kitu hata kama kikiwa ni kizuri na chenye maana kiasi gani kama hujakielewa ni rahisi kukipita tu…Na Neno la Mungu ndio hivyo hivyo hatupaswi kulisoma tu ili tuwe tunajua mistari mingi au ili tuonekana mashupavu, au tutimize wajibu fulani tu..bali tunapaswa tulisome na kulisikiliza kwa masikio ya ndani kabisa ambayo yatatufanya tulielewe. Shetani kamwe hawezi kumwibia mtu kitu ambacho kakielewa.

Shetani kamwe hawezi kumtisha mtu, wala kumwangusha mtu ambaye kalielewa Neno. Zaidi anamwogopa sana mtu ambaye kausoma mstari mmoja na kauelewa kwa undani kuliko  watu mia ambao wamesoma biblia yote na kuikariri mistari yote kiufasaha na huku hawajaielewa hata kidogo…Hao hawaogopi watu ambao wamesikia maelfu kwa maelfu ya mahubirini yanayohubiriwa kila siku makanisani, mitaani, na mitandaoni lakini hawayatendei kazi hao hawawaogopi…Zaidi anawatafuta sana watu kama hao..

Unaposikia leo Injili ambayo inamtangaza Yesu Kristo, na inayokufafanulia madhara ya dhambi..Neno lile linapozungumzwa au libapohubiriwa ni sawa na mbegu zinarushwa ndani yako…na moyoni mwako unapokuwa mlegevu kuisikiliza sauti ya Mungu kwa bidii, na kuishia kuchukulia kawaida…mahubiri yale yanapoisha na ukaondoka bila hata kuuliza wala kufuatilia kulitendea kazi au kuuliza mahali ambapo hujaelewa…Basi upo hatarini kutokufikia kumjua Mungu…siku zote utabaki katika hali hiyo hiyo…Hutakaa upate uwezo wa kuishinda dhambi.

Neno la Mungu linahitaji umakini sana(hakikisha unalielewa neno)..usilisome tu au usilisikilize tu ili kusogeza muda..Lisome na kulichunguza kwa bidii kwasababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu. Wokovu huo ni lazima uonekane kwa kila Neno unalojifunza ndani yako…hata kama kuna mahali hatujaelewa tunapaswa tukatafute huku  na huko..tukaulize huku na kule mpaka Neno lile limekuwa Dhahiri kwetu, tumelielewa kweli kweli.

Kuuliza sio ujinga..tenga muda mfuate mchungaji wako, au mwalimu wako, au ndugu yako ambaye unaona anajishughulisha kwa sehemu fulani na mambo ya Mungu Muulize mstari huu unamaana gani?..mbona umenichanganya kidogo!..Muulize mchungaji wako mbona hapa maandiko yanasema hivi na hapa hatufanyi hivi?..Muulize ni kwanini Yesu Kristo alikuja duniani, mwulize unyakuo ni nini?,  mwulize kwanini sehemu moja kwenye biblia ubatizo unasema ni kwa jina la Baba,Mwana na Roho Mtakatifu na sehemu nyingine unasema ni  kwa jina la Yesu?..

Muulize  Israeli ni nini?, siku za mwisho zitakuwaje, mwulize kwanini leo kuna madhehebu mengi?..na maswali mengine mengi, pia uliza kwa watu wengi tofauti tofauti usikie nao wanasemaje kisha piga magoti mwombe Mungu akuonyeshe ukweli na yeye ni mwaminifu (amesema tukimtafuta kwa bidii tutamwona)…usikubali kubaki na maswali ambayo huyaelewi kwa muda mrefu…Hayo maswali ambayo huyaelewi ndio mbegu zenyewe hizo ambazo shetani anazitafuta kwasababu anajua mwishoni zikipata ufumbuzi zitaleta madhara makubwa sana kwake na wewe zitakuletea matunda makubwa sana…Na usipotilia maanani Kulijua Neno la Mungu kwa mapana…Shetani ataliiba na utabaki tu kuwa vile vile muda wote.

Tatizo kubwa tulilonalo wengi ni hofu!..Mtu anaogopa kwenda kumwuliza Mchungaji wake maswali…Bwana Yesu aliulizwa maswali na akayajibu yote…sasa mchungaji au mwalimu au Nabii yeye ni nani asiulizwe maswali?…Tunachopaswa kufanya ni kuwaendea tu kwa hekima na kwa heshima, na kwa unyenyekevu. Na vilevile Mchungaji unapoulizwa maswali, haimaanishi kuwa unajua kila kitu, au utajibu kila kitu kwa ufasaha wote .Lakini kile unachokiona ni kidogo ndani yako, ni kikubwa kwa mtu mwingine aliye mchanga kiroho. Kitamfaa sana kwa wakati huo, Na pia ukikosa majibu kabisa usone vibaya kumwambia sifahamu nitakwenda kutafuta, kuliko kumpotosha ili tu kukisimamia kile unachokiamini.

Bwana atusaidie sana

(hakikisha unalielewa Neno)

Maran atha.


Mada Nyinginezo:

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

WAZAZI WA YOHANA NA YAKOBO.

Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu?

JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?

KUOTA UNAKULA CHAKULA.

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/15/hakikisha-unalielewa-neno/