by Admin | 20 January 2020 08:46 pm01
Tabia pekee inayoufautisha uzao wa Mungu na ule wa ibilisi, ni kwamba ule wa Mungu unapohubiriwa kuhusu habari ya dhambi na madhara ya dhambi baada ya kufa huwa unatabia ya kuitikia mara moja na kwenda kutubu kwa kuugua na kumaanisha kweli kuacha dhambi zake, kama vile watu wa Ninawi. Au pale unapoadhibiwa kutokana na makosa yake, basi ni rahisi kutambua makosa yao na kugeuka, kama vile ilivyokuwa kwa Daudi..
Lakini uzao wa ibilisi ni tofauti sana. Unapoelezwa habari za hukumu, badala utubu, wenyewe huwa unakwenda kinyume unaokuwa wa kwanza kupinga, kwa nguvu zote..badala ushukuru kwa kuelezwa habari za uzima wa milele, utaona unaanza kutoa maneno ya kejeli..Na pale inapotokea Mungu anaudhibu kwa makosa yake, hapo ndipo maneno ya kufuru yataanza kutoka katika vinywa vyao. Labda mtu ni mzinzi halafu Mungu kampiga kwa magonjwa ya zinaa yasiyoponyeka, badala atubu kwa makosa yake aliyoyafanya, utamwona anamtukana Mungu na kusema Mungu gani huyu anaruhusu watu wake wateseke, n.k anasahau kuwa ni kwa makosa yake ndio yamemkuta hayo yote..
Halikadhalika siku ile Mungu atakapoiadhibu hii dunia kwa mapigo yake 7 ya mwisho, kwa wale waovu wote ambao watakuwa wamebakia duniani, biblia inatuambia badala watubu, waombe rehema Mungu awasamehe kwa maovu yao, Lakini kwao itakuwa ni kinyume chake..Watamtukana Mungu na kulikufuru jina lake.
Ufunuo 16:8 “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.
9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu.
10 Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,
11 wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao”.
Unaona? Uzao wa Nyoka unavyojidhirisha wazi wazi. Hao ndio wale tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu walikuwa wameshaandikiwa hukumu (Ufunuo 13:8 na 17:8). kama tu vile shetani na mapepo yake walivyo leo hii, japo wanajua kuwa wamekosa, wanajua kuwa ziwa la moto linawangoja huko mbeleni lakini mioyo wa toba hata chembe haupo ndani yao, wala hauwezi kuwepo ndani yao kinyume chake ndivyo anavyozidi kuiharibu kazi ya Mungu,Na kumkufuru Mungu.
Leo hii ukishajiona, habari za hukumu hazikuogopeshi tena hata kidogo, Nataka nikuambie hali yako ya rohoni ni mbaya, sana, una dalili ya kuangukia katika hili kundi la watoto wa ibilisi kamili.. Kama leo hii habari za toba ni kama hadithi tu, ukihubiriwa YESU yupo mlangoni kurudi unasema hilo jambo halipo, unaishia kudhihaki tu na kukejeli na kutukana..moyoni mwako.. Nataka nikuambie upo hatarini sana.
Yuda 1:17 “Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo,
18 ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu.
19 Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho.
Tukizidi kuwaona Watu wa namna hii basi ni dalili madhubuti inayothibitisha kuwa tunaishi nyakati za mwisho. Na hivi karibuni Bwana atatokea mawinguni na watakatifu wake, kukomesha kauli kama hizo na kufuru zake zote wanadamu wanazozitoa.
Yuda 1:14 “Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,
15 ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake”.
Siku ya hukumu inakuja ndugu, Dunia hii imeshaharibika sana, haina muda mrefu, haya mambo yote unayoyaona yanaelekea kufikia mwisho, usidanganyike na amani unayoiona kama ni amani iliyopo duniani biblia inasema pale wasemapo kuna amani ndipo uharibifu unapokuja kwa ghafla, na hawataokoka (1Wathesalonike 5:1-3)…Kama vile unavyopenda kujionyesha mbele za watu wewe ni mtanashati, unavaa vizuri utokapo kwenda mjini, lakini pengine unamatatizo mengi ya siri..kadhalika watu wote unaopishana nao huko barabarani wamependeza wengine wanamatatizo kuliko yako..kadhalika vyote unavyoviona huko nje na duniani kote vinavyovitua nyuma yake vina matatizo makubwa sana…Uzuri wa dunia usikupumbaze na kudhani dunia haina matatizo…Mwisho wa mambo yote umekaribia..na dakika zinavyozidi kwenda ndivyo tunavyozidi kuukaribia ule mwisho..
Na hata kama dunia itakuwa bado miaka 200 mbele je wewe binafsi utakuwa na muda huo wa kuishi?..Muda wako ni mfupi sana hapa duniani..Kama bado unazunguka zunguka kutafuta njia ya uzima mbali na Kristo, acha kupoteza muda, kama bado unaishi maisha ya dhambi na uovu, hutaki kutega sikio lako kusikia habari za hukumu inayokuja, na umilele unaokuja…wakati utafika utakapoungana na kundi hili kufungua kinywa chako kumtukana Mungu wako aliyekuumba wewe..Lakini itasaidia nini, kwasababu biblia inasema Mungu hadhiakiwi..Utakufa na kuelekea katika lile ziwa la Moto, na nafsi yako itakuwa imesahaulika milele.
Lakini kwanini hayo yote yakukute angali unao uwezo wa kuyakwepa sasa?. Katika Muda huu mfupi uliobakiwa nao Mungu anataka kuyabadilisha maisha yako, akuburudishe akupe na uzima wa milele, akulinde wakati wote ukiwa hapa duniani, akupe na tumaini la uzima wa milele baada ya kufa..Kama upo tayari kufanya hivyo leo, basi ujue atakusamehe makosa yako yote na dhambi zako zote ulizowahi kuzifanya huko nyuma, na kufuru zako zote ulizowahi kumtolea huko nyuma..Pengine ulizitoa kwa ujinga tu, na pasipo kujua madhara yake.. leo hii Yupo tayari kukusamehe..Ni wewe tu kuufungua moyo wako.
Hivyo kama umeamua kufanya hivyo Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, . NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Ubarikiwe sana
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312
Mada Nyinginezo:
UFUNUO: Mlango wa 16.
CHUKIZO LA UHARIBIFU
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.
Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?
KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.
WALE WAZEE ISHIRINI NA WANNE (24), WANA KAZI GANI?
Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/20/wakamtukana-mungu-wala-hawakutubu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.