NITAPOKEAJE NGUVU YA KUSHINDA DHAMBI?

by Admin | 3 February 2020 08:46 pm02

Kurudi Nyuma kiimani maana yake nini?..Nitapokeaje nguvu ya kushinda dhambi?

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lizidi kubarikiwa..Karibu tujifunze maandiko.

Swali la kujiuliza leo ni nini maana ya kurudi nyuma…Mtu mmoja ukikutana naye na ukapata bahati ya kumwuliza je umeokoka?..Atakuambia ndio niliokoka ila nimerudi nyuma…Ukizidi kumwuliza je umerudi nyuma kwa namna gani atakwambia…Tamaa za kimwili zilinizidia hivyo nikajikuta ninarudi nyuma na kuangikia katika uasherati

Kama jambo hili unalipitia na wewe ndugu yangu wa thamani nataka leo hii nikuambie kuwa hukurudi nyuma…bali ulikuwa hujaokoka kabisa!…hivyo unapaswa uokoke. Leo nitakuambia mtu aliyerudi nyuma anakuwaje..

Mtu ambaye amempokea Yesu Kristo kikamilifu kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, na kudhamiria kabisa kuuacha ulimwengu kwa vitendo, na kubeba msalaba wake na kumfuata Yesu na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi…Mtu wa namna hiyo anakuwa tayari ameshaokoka..Na katika ulimwengu wa roho..anakuwa amekufa kwa habari ya dhambi, na yu hai kwa habari ya haki na anakuwa amehama kutoka mautini kuingia uzimani, na kuyavua matendo yote ya giza. Huyo anakuwa yupo chini ya mikono salama ya Yesu mwenyewe…Bwana Yesu anampa nguvu ya ajabu ya kushinda dhambi na ulimwengu kwa kutiwa muhuri na Roho Mtakatifu…Mtu huyo shetani hawezi tena kwa namna yoyote kumnyakua kutoka mikononi mwa Mungu…Uhai wake unakuwa unafichwa pamoja na Kristo.

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu”.

Mtu huyo anakirimiwa uwezo wa ajabu wa kushinda dhambi..kiasi kwamba kutenda dhambi kwake ni uchaguzi..sio kitu kinachomlazimu kama vile pumzi…Shetani anapomletea vishawishi vya kufanya uasherati ni kama mtu anayepitisha viatu barabarani …hivyo ni uamuzi wa Yule mnunuzi aidha anunue au asinunue…vilevile na Yule muuzaji anakuwa hana uwezo wa kumlazimisha anunue au akivae(ni jambo la uchaguzi), halihusishi kulazimisha…Ndivyo shetani anavyokuwa mbele ya mtu aliyeokoka kikamilifu.

Lakini kwa mtu ambaye hajaokoka dhambi kwake ni sheria, sio jambo la kuchagua, ni lazima afanye, atake asitake..anakuwa mtumwa wa ile dhambi, anakuwa na wakati mwingine na uwezo wa kujizuia kwa kipindi Fulani lakini baada ya muda mfupi anairudia ile dhambi kwa kishindo..… shetani anapomletea ushawishi wa kutenda dhambi kuna nguvu ya ajabu inamsukuma kuifanya ile dhambi hata kama hapendi, na kisha anakwenda kuifanya…

Ndio maana unasikia mtu anakwambia yaani nashindwa kuitawala tamaaa yangu najikuta nafanya hiki au kile, nashindwa kuacha kufanya uasherati, nashindwa kuacha kujichua, nashindwa kuacha kuangali picha chafu za ngono, nashindwa kuacha kunywa pombe, nashindwa kuacha kuvuta sigara, nashindwa kuacha kusikiliza miziki ya kidunia n.k…. Sasa huyo ni mtu ambaye hayupo ndani ya Kristo..

Na hali hiyo ya kushindwa kuishinda dhambi inatokana na mtu mwenyewe hajaamua kumfuata Kristo kwa kujikana nafsi, anatamani kuokoka na huku bado anatamani kuendelea kuishi na girlfriend wake/boyfriend wake, anatamani kuokoka lakini bado anazipenda movie zake na tamthilia zake na miziki yake, anakuwa hayupo tayari kuviacha kwa vitendo…hivyo ule uwezo wa kushinda haushuki ndani yake.

Sasa kwa mtu ambaye kashaokoka kikamilifu na uwezo huo wa kushinda dhambi umeshuka ndani yake…kuna uwezekano wa kupitia vipindi Fulani vidogo vidogo vya kurudi nyuma..Kurudi kwake nyuma hakutakuwa kuvuka kabisa mstari na kurudia ulimwengu hata kufikia viwango vya kurudi kufanya uasherati au kurudi kutoa mimba, au kurudi kunywa pombe au kuvuta sigara…hapana..bali kurudi kwake nyuma kunakuwa ni aidha kupunguza kiwango chake cha kusali kidogo..pengine alikuwa anasali masaa kadhaa lakini sasa kajikuta kapunguza anasali muda mfupi …alikuwa ana upendo sana, anajigundua upendo wake umepungua kidogo…alikuwa anasaidia watu lakini kajikuta kapunguza…alikuwa anajituma kuhubiria wengine lakini kajikuta kapunguza…na sio kaacha kabisa hapana! Bali kapunguza….Mtu wa namna hiyo ndio KARUDI NYUMA KIIMANI!..Na si mtu karudi kwenye uasherati, karudi kwenye ulevi, karudi kwenye anasa ndio karudi nyuma…Huyo hajarudi nyuma bali alikuwa hapo kwanza hajaokoka kabisa!..hivyo anapaswa aokoke.

Na kama imetokea mtu kashaokoka kabisa na nguvu ile ya kushinda dhambi ilishashuka juu yake…kiasi kwamba dhambi mbele yake ikija ni chaguo…na si kiamrisho…kiasi kwamba alishaacha uasherati na kulikuwa hakuna nguvu yoyote ya kumchukua katika dhambi hiyo, alikuwa ameushinda ulimwengu kiasi kwamba uuaji kwake ilikuwa ni kitu ambacho asingeweza kukifanya kwa namna yoyote ile…Mtu wa namna hiyo akaamua kwa idhini yake kuchagua kurudi kwenye dhambi…Basi biblia imesema wazi kuwa mtu wa Namna hiyo amemsulubisha Kristo mara ya pili hivyo ile neema ya kuvutwa tena kurudi kutubu..inaondolewa kabisa…kamwe hatasikia tena nguvu ya kutubu na hivyo ataendelea kuwa mbaya hivyo hivyo mpaka mauti…Kwasababu nguvu inayotuvuta kwa Mungu na kutushikilia ndiyo inayoitwa Neema, sasa mtu aliyeipokea hiyo neema na kwa idhini yake anayarudia matapishi  huyo haiwezekani kutubu…Sio kwamba siku moja atataka kutubu asisamehewe!..Hapana…bali ile hali ya kutaka kutubu inaondolewa ndani yake kiasi kwamba hatatamani hata kutubu tena. Anakuwa kama watu ambao hawataki kusikia injili kabisa.

2 Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

21 Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.

22 Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni”.

Na tena inasema katika Waebrania..

Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri”.

Hivyo kama umeokoka kikamilifu, na unaona kuna nguvu ya kushinda dhambi ndani yako..Usigeuke kurudi nyuma ndugu yangu…usirudie uasherati wala uzinzi wala ulevi, wala utoaji mimba usiichezee hiyo Neema uliyopewa (Nguvu ya kushinda dhambi ni ya kuithamini sana kuliko kitu kingine, maana ndiyo Neema yenyewe hiyo)…Usipoithamini kutakuwa hakuna nafasi ya pili wewe au mimi kurudia utakatifu tena…Ndicho kilichomkuta shetani. Aliichezea neema na hivyo akajiharibia mwenyewe…

Kadhalika kama ulikuwa unadhani kwamba kwa kufanya kwako uasherati ni kwamba ulirudi nyuma baada  ya kuokoka!…Na leo unataka kutubu!..Basi Neema ya kukuvuta kwa Kristo bali inalia moyoni mwako… Hivyo Leo fahamu kuwa hukurudi nyuma bali ulikuwa hujaokoka kabisa!!..Na kama leo hii unataka kutubu na kusema unataka kuokoka kabisa na kuacha dhambi na ulimwengu..Ukidhamiria kutoka moyoni kwa vitendo kwamba kuanzia leo na si kesho unaacha kutazama yale matamthilia ya kihindi na ya kifilipino unayoyatazama yenye maudhui ya kipepo, unaacha kuvaa vimini na unakwenda kuvipiga moto vyote sasa hivi, unaacha kuvaa suruali haijalishi una gauni moja tu, unaacha kupaka wanja, hereni, kuvaa wigi, kujichubua, unaacha kusikiliza miziki ya kidunia na unaifuta yote hata kwenye simu yako..na kuanzia leo ukisema ninaamua kumfuata Yesu kwa gharama zozote na kwamba upo radhi hata kuchukiwa, kutengwa, kuonekana mjinga na kujikana nafsi kwa viwango vyote na kwenda kubatizwa ubatizo sahihi…hapo ndipo utaona uweza wa Mungu juu ya maisha yako wa kushinda dhambi, utakapopokea uwezo wa kushinda Uasherati, ulevi, anasa, na vitu vyote vya kidunia kirahisi havitakuendesha na kukufanya ufanye jambo usilotaka wewe kulifanya.

Idadi kubwa ya watu wanaojiita wakristo hawajapokea uweza huo ndio maana wao kushinda dhambi ni ngumu…Bado hawajamuonja Kristo..Kumuonja Kristo maana yake ni kuonja huo uwezo ndani yako..Na pasipo huo uwezo kushuka ndani yako..kamwe huwezi kuishinda dhambi..kila siku utasema umeokoka, na kila siku utaongozwa sala ya Toba..lakini baada ya siku mbili tatu utarudia mambo yote ya kale…Fomula pekee ya kuipokea huo uwezo ni hiyo hapo juu…Amua kujikana nafsi kwa kuacha vitu vyote kwa vitendo.

Bwana akubariki sana.

Maran atha!


Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:


Mada Nyinginezo:

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

TIMAZI NI NINI

DHAMBI INAZAA KIFO.

DUNIANI MNAYO DHIKI.

JE WAJUA?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/03/nitapokeaje-nguvu-ya-kushinda-dhambi/