MWACHE YESU, NDIO AWE WA  KWANZA KUKUHURUMIA.

by Admin | 29 March 2020 08:46 pm03

Siku zote mwache Yesu, ndio awe wa  kwanza kukuhurumia!.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo.

Ni jambo la kawaida kila mmoja wetu kuijali kwanza hali yake binafsi, na si dhambi kufanya hivyo, japo hilo halitufanyi tuonekane kuwa wa maana sana mbele za Mungu.. Kuna wakati Bwana Yesu aliitisha mkutano mkubwa sana, pengine eneo la mjini lilikuwa ni dogo la kuuketisha umati mkubwa wa watu, au pengine palikuwa na usumbufu fulani ambao ungewafanya watu wasimsikilize vizuri, Hivyo akaamua kuwaitisha eneo la mbali kidogo na mji, mahali ambapo hapana makazi ya watu, eneo la nyika tupu,..mahali ambapo hakuwaandalia mahema ya kukutania wala hakuwachagulia penye miti mingi, ambapo walau wangekaa chini yake wapate uvuli, bali alichagua eneo la jangwa lenye nyika tupu.

Na mkutano huo ulikuwa ni Mkutano wa siku tatu..

Lakini biblia inatuambia wengi waliposikia habari ile wakatoka mbali sana, wakaenda eneo hilo la jangwa ili kwenda kuyasikiliza maneno ya uzima ya Bwana Yesu,..Watu wale walifikia pengine asubuhi sana na mapema, wakijua kuwa siku zote tatu zitakuwa ni siku za kufunga, za kumsikiliza tu Bwana Yesu si vinginevyo, hivyo walifika mahali pale wakilijua hilo asubuhi sana, wakakaa chini kwenye jua lile, kuanzia asubuhi mpaka jioni,..

Jaribu kutengeneza picha, masaa 12 ya mchana wanamsikiliza tu Bwana Yesu akiwafundisha, na usiku vivyo hivyo.. siku ya kwanza, siku ya pili, mpaka siku  tatu zinakwisha, wamekaa tu pale, nyikani wakimsikiliza Bwana Yesu kwa makini bila kuondoa miguu yao, huku njaa zikiwauma, lakini waliona kile wanachokisikiliza ni Zaidi ya chakula cha mwilini.. Walijua mtu hawezi kuishi kwa mkate tu, bali kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Bwana..

Embu tengeneza tena picha Bwana alikuwa anajua kabisa watu wale, walikuwa katika hali ngumu kweli kweli katika eneo lile la ukame na jua kali, alijua kabisa walikuwa hawajala kwa muda wa masaa mengi sana, alijua kabisa hali zao zinakaribia kuwa mbaya..lakini aliendelea kuwafundisha bila kuwahudumia kwa lolote, kwasababu aliona utayari wao wa kumsikiliza yeye bila kuchoka, mpaka siku tatu kamili zilipokwisha..

Lakini siku ile alipomaliza kuwafundisha, biblia inatuambia Bwana Yesu hakuwaacha hivi hivi waondoke waende zao katika hali zile za njaa bali aliona umaskini wao, aliona njaa zao, aliona mateso yako, aliona kiu yao, aliona mahitaji yao na pale pale  maandiko yanatuambia AKAWAHURUMIA ..embu tusome:

Marko 8:1 “Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

2  NAWAHURUMIA MKUTANO kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;

3  nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

4  Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?

5  Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,

6  Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano.

7  Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.

8 Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba.

9  Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga”.

Unaona hapo?..Walipaswa waondoke vile vile, lakini kwa jinsi alivyoona “WAMEKAA NAYE” siku zote tatu bila kuondoka uweponi mwake, bila kwenda kuhangaika hangaika kuyajali maisha yao, familia zao, biashara zao, miradi yao, ili wapate chakula wao na Watoto wao, badala yake wamedumu pamoja naye kwa siku kadhaa bila kuchoka..basi tukio hilo lilimfanya Bwana Yesu AWAHURUMIE hata kwa yale mengine waliyoyakosa..

Na kama tunavyosoma kitu gani kilifuata.. Wote walishibishwa mikate wakiwa pale nyikani, wakapata na ya kuondokea, mpaka ikabaki na wale samaki vivyo hivyo…Sasa unaweza ukafikiri Bwana Yesu aliwashibisha pale tu…La! Alikuwa anawadhihirishia kuwa baada ya pale na Maisha yao pia yatabarikiwa kwa mfano ule ule wa vikapu, na wala hawatapungukiwa kabisa…Lakini hiyo yote ilikuwa ni kwasababu ya yale maneno ya uzima waliokuwa wanayasikia bila kuchoka ndio yakazaa vikapu vile vya mikate na baraka walizoziendea baada ya pale.

Na sisi tujiulize Je tunaweza kufikia hatua kama hii ya hawa watu?…Je tunaweza kuwa tayari kufunga kutokula kwa ajili tu ya kuutafuta uso wa Bwana kwa kipindi kirefu?, Je tunaweza Kufunga mihangaiko yetu, na shughuli zetu tukatenga wakati wa kuhudhuria ibada na semina ndefu za Neno la Mungu?..kwa kutokujali eneo lenyewe, kutokujali mazingira yanaruhusu kiasi gani, kutokujali umbali, kutokujali hata uzima wako na afya yako?.. Ikiwa tu tutaalikwa mahali ambapo tumewekewa mahema, chini kuna vivuli, lakini bado hatutakwenda ikiwa tunayo makanisa mazuri tena mengine yana feni lakini hatuwezi kukaa hata masaa 2, Je tutawezaje ikiwa tutalikwa mahali penye njika tupu kama pa hawa watu?..Na wakati huo huo bado tunataka Bwana Yesu azihurumie hali zetu,?

Mungu anatuambia tumkaribie yeye na yeye atatukaribia sisi (Yakobo  4:8)..Hivyo tukiwa hatupo tayari kujinyima nafsi zetu na kujitesa katika kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii, katika kuutafuta ufalme wake na haki yake, basi tujue itakuwa shida sana kuyaona matendo makuu ya Mungu maishani mwetu.

Usikazane kutafuta kujihurumia kwanza wewe unapoutafuta uso wa Mungu, subiri kwanza mwache Yesu akuhurumie yeye..jukumu letu ni kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii mengine tumuachie yeye, kwasababu anajua shida zetu, na mahitaji kabla hata sisi hatujamwambia. (Mathayo 6:32).

Bwana atusaidie katika hilo. Na atujalie tuchukue hatua zinazostahili katika hilo.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.

MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

SAKRAMENTI NI NINI, NA JE! IPO KATIKA MAANDIKO?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/29/mwache-yesu-ndio-awe-wa-kwanza-kukuhurumia/