by Admin | 4 April 2020 08:46 pm04
Je! Ni sahihi kwa mkristo kufikiria hivi?..
Jaribu kufikiria mfano huu..
Mtu mmoja alitamani sana kujua afya ya mwili wake, hivyo akakusudia kweli kwenda hospitali kupima afya yake kama ameathirika na Ukimwi au La, Hivyo akafanikiwa kwenda kuonana na daktari akachukuliwa vipimo vyote, Lakini alipomaliza kuchukuliwa tu vipimo akaondoka zake akarudi nyumbani kwake, daktari alipomaliza uchunguzi wake wa vipimo akarudi sasa ili ampe majibu yake, na kumpa ushauri nasaha lakini alipofika hakumwona..
Sasa akiwa kule nyumbani, siku zikapita, miezi ikapita, miaka ukapita, akawa anaishi Maisha ya furaha na ya amani kabisa, siku moja watu wakamuuliza vipi kuhusu afya yako, tunatumai sasa ipo njema kwasababu siku ile tayari ulishakwenda kuonana na Daktari..
Ndipo yeye akajibu, ndio! Natumai itakuwa ni njema!..Watu waliposikia vile wakashangaa kwa jibu lile, unatamai vipi tena? Wakati ulishapata uhakika kwa Daktari,..Lakini yeye akawajibu, ndio nilishaonana na daktari akanichukua vipimo vyote, ila majibu anayo yeye mwenyewe, mimi sijui kingine Zaidi ya hapo, Hivyo yeye Mungu ndiye anayejua kuwa mimi ni muathirika au La!. Hilo ni jukumu lake kama daktari, mimi sihitaji kujua sana kwasababu mimi sio daktari..
Fikiria mtu kama huyo wale watu walimwonaje? Ni Dhahiri kuwa watasema huyu atakuwa amerukwa na akili, alikwenda hospitali kufanya nini sasa kama hakupata majibu ya afya yake, ambayo yangempa uhakika wa afya yake kuwa ni njema au la!.
Na ndivyo ilivyo hata leo kwa mtu ambaye hajapata bado uhakika wa wokovu wake..Watu wengi ukiwauliza Je! Umeokoka watasema ndio, nilishaokoka zamani sana, mpaka nikabatizwa,..Ukizidi tena kuwauliza, sawa Je unaouhakika hata ukifa leo au Yesu Kristo akirudi leo utakwenda naye mbinguni.. hapo ndipo watakapokuambia ninatumai hivyo, wengine watakuambia hilo ni Mungu ndio analolijua..mimi siwezi kujua hukumu zake, na mwingine atakwambia,nikisema hivyo nitakuwa ninajihesabia haki, na kujiona mimi ni kitu fulani mbele za Mungu..wakati bado sijafika lolote linaweza kutokea.
Ndugu Neno WOKOVU ni Neno lenye msingi wa UHAKIKA chini yake, mfano huwezi kusema umeokolewa kwenye moto, na huku bado unajihisi kama upo bado mule mule motoni, vinginevyo hiyo itakuwa ni ndoto tu au bumbuazi fulani limekushika, lakini mfano ukiokolewa kutoka motoni na mtu fulani, utajiona kabisa jinsi unavyohama kutoka ulipokuwepo kwenye mateso na kwenda sehemu nyingine salama..Hivyo ni jambo la uhakika..
Na ndio maana biblia inaweka wazi kabisa kwa kutuambia…
2Wakorintho 13:5 “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa”
Unaona, ukiwa mkristo huendi tu ilimradi, huwi tu kama mshabiki fulani, bali kila hatua inajipima je! Mpaka sasa Kristo yupo pamoja nami au La!, Na je ikitokea leo hii safari yangu ya Maisha imekwisha ghafla Je nitakuwa upande wa haki au hukumu?
Sasa, swali unaloweza kujiuliza ni Je utaupataje Uhakika huo wa wokovu ndani yako?
Unapaswa uangalie mambo mawili la kwanza Ni Je! Tangu uliposema umeokoka, kuna badiliko lolote lililotokea ndani yako?..Je yale matunda ya Roho yamezalika ndani yako?
Sawasawa na Wagalatia 5:22 inayosema..
“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.
Hivyo kama hayo yapo ndani yako, basi hiyo ni hatua ya kwanza ya kukupa uhakika ndani yako.
Na jambo la pili, Je! Tangu ulipoubeba msalaba wako na kumfuata Kristo, Je! Ulipitia vipingamizi vyovyote katika hilo?..Kupitia majaribu sio sifa kwamba ni jambo jema, lakini shetani hawezi kukuangalia umeacha rushwa, akakuvumilia, umeacha ulevi na kuuza pombe kwenye biashara yako akakuangalia tu, umeacha kampani za marafiki wabaya na disko asikuletee udhia, umeacha ulimwengu kwa ujumla wake na mambo yake yote asikuletee dhihaka, umekatisha ghafla yale madili haramu uliyokuwa umepanga wewe na wenzako kwenda kuyafanya shetani akabaki anakutazama tu!..Umekatisha hayo mahusiano ya kiasherati ghafla anakutazama tu…wakati mwingine utapitia kupigwa au kutengwa, n.k. Sasa kama haya hayakuonekana ndani yako basi uhakika huo kuupata ni ngumu, Kristo na mitume wake waliyapitia hayo, vilevile na wewe utakumbana nayo kwa sehemu fulani katika safari yako ya wokovu.
Sasa Ikiwa hayo mambo mawili makuu yameonekana ndani yako, basi uhakika wenyewe wa kama upo katika njia sahihi ya wokovu utatokea wenyewe ndani yako, wala hautahitaji kuulizia bali Roho Mtakatifu mwenyewe atakushuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mungu na umeokoka..
Sawasawa na Warumi 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;
Hivyo ndugu, kama bado mpaka sasa hujapata uhakika huo, Ujue tu, mbinguni hutakwenda haijalishi utasema niliongozwa sala ya toba, au nilibatizwa, au nilikuwa ninahudhuria kwenye maombi..Hutakwenda kwasababu suala la wokovu sio suala la kubahatisha au kuhisi hisi tu bali ni uhakika Mungu anaompa mtu akiwa bado hapa hapa duniani..Na kuwa na uhakika wa kwenda mbinguni sio kujihesabia haki..
Biblia inasema…
2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.
Ukisoma kwenye tafsiri nyingine hususani zile za kiingereza(kjv) Hilo Neno “jitahidini zaidi kufanya imara” linasema hivi..
“brethren, give diligence to make your calling and election sure…”
Neno SURE, linaamisha uhakika, maana yake ujitahidi kuufanya kuitwa kwako na uteule wako uwe wa uhakika..
Hivyo na wewe pia hujachelewa, ndani ya kipindi hichi kifupi cha maisha yako uliyobakiwa nayo hapa duniani, na kabla Bwana hajarudi, anza kuuthibitisha tena wokovu wako, kusudia kweli kuanzia leo kumfuata Kristo, anza kuzaa hayo matunda ya Roho, na kuwa tayari kuubeba msalaba wako..Na Bwana mwenyewe atauweka uhakika huo ndani yako. Nawe utaishi Maisha ya amani kila siku, ambapo hata wimbi lolote likisimama mbele yako, hata bunduki ikiwekwa mbele yako, huna wasiwasi kwasababu unajua ukifa tayari moja kwa moja utakuwa mbinguni kwa Baba.
Bwana akubariki sana.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/04/nimeokoka-ila-mungu-ndiye-anayejua-nitakwenda-wapi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.