NEEMA YA MZALIWA WA PILI.

by Admin | 20 May 2020 08:46 pm05

Kuna nguvu katika mzaliwa wa pili.

Shalom, jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe,

Biblia inasema Israeli ni Mzaliwa wa kwanza wa Mungu..

Kutoka 4: 22 “Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni MWANANGU MIMI, MZALIWA WA KWANZA WANGU;

23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako”.

Kama kuna mzaliwa wa kwanza maana yake kuna mzaliwa wa pili..Na kama vile mzaliwa wa kwanza hapo biblia imelitaja ni Taifa la Israeli..maana yake mzaliwa wa pili ni mataifa mengine yaliyosalia…Na hiyo ni sababu Taifa la Israeli ndio limekuwa la kwanza kushiriki Baraka za Mungu kabla ya sisi watu wa mataifa…Sababu  pekee ndio hiyo, kwamba lenyewe ndio mzaliwa wa kwanza, kumjua Mungu.

Itakuwa ni ajabu watoto wa mwisho katika familia wanakuja juu na kuanza kumlaumu mzazi wao kwanini kaka yao amekuwa wa kwanza kunyonya kabla yao?, na kwanini wamerithi nguo za kaka yao na viatu vyake, lakini kaka yao hakurithi vyao? N.k Ukiona mtoto ananung’unika kwa ajili ya hayo basi kuna uwezekano akili yake haijakomaa vizuri…kwasababu kama ingekuwa imekomaa vizuri ingekuwa ni rahisi sana kujua ni kwanini kaka yake kamtangulia kwa kila kitu….angejua ni kwasababu kaka yake ndio kazaliwa wa kwanza na kisha yeye ndio akafuata…hiyo ndio sababu ya kipekee na hakuna nyingine.

Halikadhalika leo hii tutauliza ni kwanini Mungu aliwachagua kwanza Israeli na kuwapa upendeleo ?..Jibu ndio hilo hapo juu la Kutoka 4:22 kwamba Israeli ni MZALIWA WA KWANZA. Hivyo hana budi kunyonya baraka za Mungu kabla yetu, hana budi kuvivaa viatu vipya, na sisi watu wa mataifa tutakapozaliwa baadaye tutavirithi vile vile viatu..Ndio maana tunatumia kitabu cha biblia agano la kale ambalo limejaa Maisha ya Wana wa Israeli tu ili kujifunzia njia za Mungu.

Lakini ipo siri nyingine kubwa juu yetu sisi watu wa mataifa, ambao hatukuchaguliwa kuwa wazao wa kwanza. Na siri hiyo ipo katika msalaba.

Kwa kupitia Yesu Kristo, sisi watu wa mataifa, wakati wetu ulipofika wa kuzaliwa tulipata baraka mara dufu Zaidi ya wana wa Israeli. Bwana Yesu alitufanya sisi ambao hapo kwanza tulionekana kuwa sio warithi,..akatufanya kuwa warithi..Kwasababu urithi siku zote ulimhusu mzaliwa wa kwanza tu.

Waefeso 2:12  “kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.

13  Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.

14  Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga”.

Umeona ni Neema ya namna gani hiyo?..Mimi na wewe hatukustahili kuitwa warithi, waliostahili kuitwa warithi ni jamii ya Wana wa Israeli peke yao, kwasababu wao ndio wazaliwa wa kwanza, lakini sasa sisi watu wa mataifa ni warithi kupitia msalaba wa Yesu Kristo…

Yakobo ulipofika wakati wa kuwabariki wana wa Yusufu, ambapo alitakiwa mkono wa kuume auweke juu ya mzaliwa wa kwanza na ule wa kushoto juu ya mzaliwa wa pili, kinyume chake mikono yake aliipishanisha kama ishara ya msalaba na ule wa kushoto akauweka juu mzaliwa wa kwanza na wa kuume juu ya mzaliwa wa pili(Mwanzo 48:8-17). Siri hiyo ni kubwa sana.

Tendo hilo lilikuwa ni ufunuo wa msalaba, kupitia msalaba Baba yetu wa mbinguni alitubariki sisi tuliokuwa wa uzao wa pili, baraka ambazo zingestahili kupokewa kwa mzao wa kwanza yaani wana wa Israeli. Ni neema kubwa sana tuliyopewa, ambayo hatupaswi kuipuuza hata kidogo..

Je bado unaupuuza msalaba?..je bado upo bize kutafuta fursa za fedha kuliko kutafuta kujua siri zilizopo katika msalaba?..Kumbuka urithi ambao wana wa Mungu wameahidiwa ni mbingu mpya na nchi mpya…Katika mbingu hiyo na nchi hiyo, hakuna kuumwa, hakuna kuteseka, hakuna dhiki, hakuna njaa..hakuna mwanzo wa siku wala mwisho..Milele na milele Watoto wa Mungu watang’aa na kuishi bila tabu wala dhiki, wala majuto..kwa ufupi biblia inasema kuna mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia tuliyoandaliwa.

Ni maombi yangu kuwa injili ya msalaba haitakuwa upuuzi kwetu..Kabla Biblia inavyosema katika..1Wakorintho 1:18  “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”.

Kama hujaokolewa leo ni siku yako..huu sio wakati wa kutanga tanga na kushabikia udhehebu au udini uliokuwa nao..Kumpa Yesu Maisha yako sio dini mpya wala dhehebu jipya..ni Neno la Mungu..Hii neema ya msalaba tuliyoipokea ya kufanyika warithi haitadumu milele, ipo siku itaisha, na Neema hii inatufundisha kuukataa ubaya…maana yake ni kwamba ukiwa mwasherati, mzinzi, mwizi, mlevi, mtukanaji, mtoaji mimba, msagaji na mambo mengine yote yanayofanana na hayo yasiyompendeza Mungu, bado hujaingia katika neema hii, hivyo unahitaji kuingia katika Neema hii..

Kama upo tayari kufanya hivyo leo..basi uamuzi unaoufanya ni wa busara, unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kujitenga dakika kadhaa peke yako na kuomba rehema mbele za Mungu kwa yote uliyoyafanya yasiyompendeza yeye…na dhamiria kutoyafanya tena kwa vitendo, tubia kwa dhati kabisa uasherati wako na usiufanye tena, usagaji wako, utoaji mimba uliokuwa unatenda, ukahaba, uvaaji nusu uchi kikahaba, wizi, utukanaji na mambo mengine yote ya siri..Na Bwana atakusamehe kwasababu yeye ni mwenye huruma na mwingi wa rehema, endapo umedhamiria kweli kwa dhati kuacha hayo matendo maovu uliyokuwa unayafanya.

Baada ya hapo, usikawie haraka sana katafute ubatizo sahihi kama hujabatizwa…kipengele hichi ni cha muhimu sana..Ingekuwa ni mimi mwanadamu natoa maagizo ya kupokea wokovu ningekiruka labda pengine kisingekuwa na maana sana kwangu, lakini sivyo kwa Mungu, kitendo hichi cha ubatizo kina maana sana kwake..hivyo akaagiza kwamba kila aaminiye ni lazima akabatizwe, hata mimi linalihusu agizo hili, hata mchungaji yoyote yule, hata Paulo lilimhusu, zaidi sana Bwana wetu yeye mwenyewe alikuwa kielelezo alikwenda kubatizwa..Hivyo hatupaswi kupuuza hata kidogo, nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ikiwa kweli umemaanisha kutubu na kumwishia Kristo, ukiona jambo hilo ni mizigo kwako, ni wazi kuwa bado hujatubu kwa kumaanisha..Lakini ukizingatia hilo Bwana atakupokea kabisa na Roho Mtakatifu atakuongoza kufanya yaliyosalia.

Na hapo utakuwa umekamilisha wokovu wako na kuzaliwa mara ya pili kulingana na maandiko.Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho na majuto makuu yanakaribia kuja ulimwenguni kote kwa wale wote watakaomkataa Kristo. Bwana atusaidie mimi na wewe tusiwe miongoni mwao. Hizi ni nyakati za mwisho kweli kweli, wala si mzaha..

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

HISTORIA YA ISRAELI.

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

KUPATA MAONO YA MBINGUNI SIO KUFIKA MBINGUNI.

Kuna ufufuo wa aina ngapi?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/20/neema-ya-mzaliwa-wa-pili/