KUPATA MAONO YA MBINGUNI SIO KUFIKA MBINGUNI.

KUPATA MAONO YA MBINGUNI SIO KUFIKA MBINGUNI.

Kupata maono ya mbinguni sio kufika mbinguni…ndio mwanzo wa safari.

Bwana anatupenda, na wakati mwingine anawachukua baadhi ya watu (sio wote) ili kuwaonyesha mambo yaliyopo kule nyumbani, juu kwa baba yetu.

Anawapeleka kuwaonyesha mambo mazuri aliyowaandalia wanawe, anawaonyesha makazi yao ya kuduma yasiyoharibika na hazina zinazowangoja kule nga’mbo ikiwa watashinda..Anawaonyesha utajiri aliowaandalia na heshima na utukufu..anawaonyesha ni kwa jinsi gani mbingu inavyowatamani na ilivyojiandaa vya kutosha kuwalaki…na mambo mengine mengi ambayo hata hayaelezeki.

Ni mfano tu wa Wana wa Israeli baada ya kutolewa nchi ya Misri na kufikishwa kule jangwani..ambapo maili chache kabla kufika nchi ya Ahadi…Mungu aliwatuma wakaipeleleze nchi ya ile waliyoahidiwa, na aliruhusu waende watu wachache sana(yaani watu 12 tu) ndio walioteuliwa kwenda kuipeleleza…Na walifika kweli Kaanani na kuipeleleza walirudi kila mtu na jibu lake…lakini wote walikubaliana na jambo moja  kuwa nchi ile ilikuwa ni njema sana na imejaa unono na maziwa na asali, na baraka tele na kweli ni nchi yenye urithi mzuri usioelezeka.

Hesabu 13:1 “Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

 2 Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.

3 Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli……..

17 Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani,

18 mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi;

 19 na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome;

 20 nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza.

21 Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi.

22 Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.

 23 Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini.

24 Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli.

25 Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini.

 26 Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi.

27 Wakamwambia wakasema, TULIFIKA NCHI ILE ULIYOTUTUMA, NA HAKIKA YAKE, NI NCHI YENYE WINGI WA MAZIWA NA ASALI, NA HAYA NDIYO MATUNDA YAKE”.

Watu hawa ni kweli walifika katika ile nchi…lakini sio kwamba kwasababu wamefika basi ndio hawana haja ya kurudi tena kwa wenzao…Muda wa wao kufika kule ulikuwa bado…walikwenda tu kuonyeshwa nafasi zao kule…Lakini bado walikuwa hawajaiteka ile nchi, walipaswa warudi kwanza wakapange vita wapambane wayaondoshe yale majitu yaliyoshikilia urithi wao katika nchi ya Ahadi ambayo wameahidiwa, wakishawaangusha ndipo waimiliki…

Ndio maana Bwana Yesu alisema katika..

 Mathayo 11:12 “ Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”

Shetani sasa kashikilia nafasi zetu katika ulimwengu wa roho, tunapaswa tumwangushe chini kabla ya kufika nga’mbo, na vita tunapambana hapa hapa duniani…tutakapomwangusha chini ndipo tutazirithi baraka zetu….(na tunamwangusha chini kwa kuishi Maisha matakatifu na makamilifu ya Neno la Mungu, yanayompendeza yeye),….hatuna budi kupambana vita hapa…kusikia tu mbinguni ni kuzuri tumeandaliwa hiki na kile haimaanishi kwamba ndio tayari tumekwishafika…bado kuna vita vya kupambana kumwangusha shetani katika Maisha yetu..

Shetani hataki tuende mbinguni kabisa, hataki hata kidogo kwasababu anajua uzuri tutakaoukuta kule, … anapambana sana kuhakikisha hatufiki kule, kama alivyopambana na wana wa Israeli kuhakikisha hawafiki nchi ya Ahadi, au hata wakifika basi watafika wachache sana na kwa shida sana..Hebu tafakari katika ule umati wote waliotoka Misri Zaidi ya watu milioni 2 waliofanikiwa kuingia nchi ya Ahadi walikuwa ni watu wawili tu (2)! Na iliwachukua miaka 40 kuingia tu ile nchi ambayo ni maili chache tu, safari ya mwezi mmoja tu. Alikuwa ananyanyua kila aina ya vikwazo walipokuwa njiani..aliwatumia mpaka manabii wa uongo kuwaangusha wana wa Israeli walipokuwa njiani.

Na sisi ni hivyo hivyo…mbinguni hatuendi kwa miguu kama wana wa Israeli walivyokwenda Kaanani, kama tutaishi Maisha ya kutoujali wokovu kama baadhi ya wana wa Israeli walivyokuwa, tutaangamizwa na hatutaurithi ufalme wa mbinguni, kama tukikubali maneno ya manabii wa uongo kama baadhi ya wana wa Israeli walivyokubali kuyasikiliza maneno ya akina Kora na Balaamu basi na sisi hatutairithi nchi.

Kama hatutamheshimu Mungu kama baadhi ya wana wa Israeli walivyokosa kumheshimu Mungu wakiwa safarini basi haijaishi tumeikaribia mbinguni  kiasi gani hatutairithi.. Kama tutakata tamaa na kutoamini kwamba tunaweza kufika mbinguni basi hatutafika kweli kama wale watu ambao baada ya kwenda kanaani kuipeleleza walileta ripoti za kuwaogopesha watu, na wote walikufa..

1Wakorintho 10:5  Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.

6 BASI MAMBO HAYO YALIKUWA MIFANO KWETU, KUSUDI SISI TUSIWE WATU WA KUTAMANI MABAYA, KAMA WALE NAO WALIVYOTAMANI.

7  Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.

8  Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.

9  Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

10  Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11  Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12  Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

Biblia inasema..

Ufunuo 21:7  “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8  Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”

Ufunuo 21:27  “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo”

Mpe leo Yesu Maisha yako kama hujampa. Na pia jikane nafsi yako, jitwike na msalaba wako mfuate Yesu kama ulikuwa hujafanya hivyo..Safari yetu karibia inafika ukingoni, na shetani ndivyo anavyozidi kuongeza jitihada kuwapunguzia watu kasi ya kuingia uzimani..

Kumbuka mtume Paulo alichokisema, aliponyakuliwa kule juu na kuonyeshwa mambo ambayo hayatamkiki, Hiyo ni kuonyesha ni kwa jinsi yalivyo ya ajabu na ya kushangaza kiasi kwamba hata lugha haziwezi kuelezea, (2Wakorintho 12:4)..sasa unasubiri nini..Kimbilia kwa YESU ayaokoe maisha yako.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

RABI, UNAKAA WAPI?

JINA LA MUNGU NI LIPI?

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

TUNA WAJIBU WA KUOMBEA MAHALI TULIPO.

ZIFAHAMU NAMBA KATIKA BIBLIA NA MAANA ZAKE.

HISTORIA YA ISRAELI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments