Ibada ni nini,Na je ili ikamilike inapaswa iwe na nini na nini?

by Admin | 11 September 2020 08:46 pm09

SWALI: Ibada ni nini, Na je ili ibada ikamilike inapaswa iwe na nini na nini? Na je ni siku gani maalumu ya kufanya ibada?


Ibada ni kitendo chochote kifanywacho kuonyesha unyenyekevu wa hali ya juu, utiifu, heshima, shukrani,  na utukufu, aidha  kwa Mungu au kitu kingine, na hiyo inaambata na mambo kadha wa kadha, ikiwemo kusifu, kuabudu, kusujudu, kuimba, kufunga, kutoa sadaka, na kushiriki maagano ya imani, Na vilevile kujitoa mwili wako kuvitumikia, hiyo nayo ni ibada kamili.

Kibiblia kuna ibada za aina tatu

  1. Ibada kwa Mungu.
  2. Ibada kwa shetani.
  3. Na ibada za wanadamu walizojitungia wenyewe kwa Mungu.
  1. Tukianzana na ibada kwa Mungu:

Hizi, ni zote tuzifanyazo aidha kanisani au manyumbani kwetu wenyewe, tunapokutana kumwimbia na kumwabudu Mungu, au kumshukuru, au kushiriki meza ya Bwana, hiyo tayari ni ibada kwa Mungu.

Matendo 13:2 “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia”.

Na kama tulivyosema awali hata kujitoa mwili wako kwa ajili ya kutenda matendo yote yampendezayo Mungu ni ibada kamili tayari..

Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana”.

  1. Ibada kwa Shetani.

Hizi kwa jina lingine ndio ibada za sanamu. Ambazo biblia imezikemea sehemu nyingi sana katika biblia. Unapokwenda kuisujudia sanamu yoyote ile, iwe na mfano wa mtakatifu Fulani mbinguni, tayari hiyo ni ibada kamili  ya sanamu.. Inayomtia Mungu wivu wa kukuangamiza haraka sana.

Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.

1Wakorintho 10:14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu”.

 Lakini kama hilo halitoshi, unaweza pengine ukawa husujudii masanamu, lakini mwili wako unafanya maasi, hiyo nayo ni ibada kamili ya sanamu sawasawa na kusujudia vinyago.

Wakolosai 3:5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu”;

  1. Ibada watu walizojitungia wenyewe kwa Mungu:

Hizi ni ibada ambazo, hazitokani na Mungu wala shetani, bali zinatokana na watu wenyewe, wamejitungia wakidhani kuwa wanamfanyia Mungu, kumbe wanafanya kimakosa..

Wakolosai 2:20 Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,

21 Msishike, msionje, msiguse;

22 (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?

23 Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, KATIKA NAMNA YA IBADA MLIYOJITUNGIA WENYEWE, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.

Na zina madhara yake makubwa, kwasababu wakati mwingine zinasababisha hata watu waue watu wengine wakidhani kuwa ndio wanampendeza Mungu, kama tu walivyokuwa wanafanya Warumi na Wayahudi kwenye kanisa la kwanza, na jinsi zinavyofanywa na baadhi dini leo hii duniani kuchinja watu. Zote hizo ni ibada ambazo watu wamejitungua lakini hazitokani na Mungu.

Yohana 16:2 “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa ANAMTOLEA MUNGU IBADA.

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa, ibada halisi ni moja tu, nayo ni kwa Mungu muumba wa mbingu na nchi (YEHOVA), na Kristo wake aliyesulibiwa kwa ajili ya dhambi zetu sisi wanadamu. Na maagizo pekee ya ibada hiyo halisi yanapatikana katika biblia tu.. Ibada nyingine yoyote tofauti na hiyo, ni machukizo makubwa kwake.

Na pia tunaikamilisha kwa miili yetu kama biblia inavyotufundisha, kwa kuishi maisha yampendezayo Bwana, ndio ibada yenye maana, ikiwa tutakuwa tunahudhuria kanisani kila siku, tunamwabudu Mungu usiku na mchana, tunamtolea matoleo mengi, tunashiriki meza ya Bwana kila wiki halafu matendo yetu, au miili yetu tumeiuza kwa shetani, ibada zetu bado ni batili..Zinakuwa ni ibada za sanamu, au ibada tulizojitungia tu sisi wenyewe.

Lakini kama utayakamilisha yote ya rohoni na mwilini, basi ibada hiyo  inafaa sana mbele za Mungu, na inathawabu nyingi sana. Wanaomfanyia Mungu ibada kamili wanakuwa marafiki wa karibu sana Mungu.

Na pia hakuna siku maalumu ya kumfanyia Mungu ibada, kwani ibada yetu halisi ipo rohoni, hivyo wakati wowote na muda wowote uwapo na nafasi inaingia uweponi mwa Mungu, kumsifu, kumshukuru, kumwabudu, kumtolea dhabihu za shukrani n.k.. Lakini pia ipo ibada ya watakatifu wote, ambayo inafanyika kila juma, hivyo ikiwa ni jumapili au Jumamosi, inapaswa ifuatwe. Kama tulivyoambiwa tusiache kukutanika pamoja..

Bwana wetu atusaidie sote, tuweze kuyakamilisha hayo.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

USILETE UJIRA WA KAHABA, NYUMBANI KWA MUNGU.

Nyama zilizosongolewa ni zipi?Je kunywa damu ni dhambi?

JE KUVAA PETE NI DHAMBI?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

CHAPA YA MNYAMA

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/11/ibada-ni-ninina-je-ili-ikamilike-inapaswa-iwe-na-nini-na-nini/