JE KUVAA PETE NI DHAMBI?

JE KUVAA PETE NI DHAMBI?

Je kuvaa pete ni dhambi kwa mkristo?


Awali ya yote kabla hatujafahamu kama kuvaa pete ni dhambi au sio dhambi ni vizuri  kwanza tukajua jambo hili kuwa biblia imekataza wanawake wacha Mungu(Wakristo), kujipamba kwa mfano wa wanawake wa kidunia. Biblia ililijua hilo tangu zamani kuwa wanawake wengi watatamani kufanya hivyo, na ndio maana vifungu hivyo vya zuio la kujipamba viliwalenga moja kwa moja wao na sio wanaume..

Tusome,

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”.

Sasa huyo ni Paulo aliandika hivyo, lakini mtume Petro naye pia alilirudia Neno hilo kuonyesha msisitizo wa  maagizo wa maagizo hayo ya Mungu kwa wanawake wote..tusome..

1Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

4 bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

5 Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao”.

Unaona wakina Sara hawakujipamba, wakina Mariamu hawakujipamba, na wanawake wengine wote mashujaa tunaowasoma kwenye biblia hawakufanya hivyo  ni mwanamke mmoja tu katika biblia aliyeitwa Yezebeli ndiye tunamwona alikuwa akijimbana na kujipaka ma-wanja, na sisi sote tunajua tabia zake alikuwa ni mwanamke wa namna gani hakuna haja ya kuzisimulia..

Hivyo kama wewe ni mwanamke uliyeokoka, unamcha Mungu, na umekuwa ukijipamba, kwa mawigi, mikufu, mahereni, make-ups, kucha za bandia, n.k…Ni vizuri kuacha mara moja..Ukristo ni mabadiliko ya rohoni na mwilini, ukishindwa maagizo madogo kama hayo, utawazaje yale mengine?

Sasa tukishapata huo msingi turudi kwenye swali letu lililoulizwa je kuvaa pete ni dhambi?

Jibu ni kuwa; inategemea, zipo pete za mapambo kwa lengo la kujipamba tu, na zipo pete zinazotambulisha ndoa..

Ikiwa pete unazovaa ni kwa ajili ya mapambo, hapo unaingia katika hilo kundi la mapambo ambayo hayamstahili mkristo yeyote, unakuwa huna tofauti na anayevaa vikuku, na mahereni,..fungu lenu ni moja.

Lakini ikiwa pete unayovaa ni kwa ajili ya kuitambulisha Ndoa, Hilo haliwi tena pambo bali inakuwa ni kiashirio cha kitu Fulani, kama tu vile mtu anayevaa saa mkononi, ipo  kwa lengo la kutambulisha majira.

Hivyo ikiwa unakwenda kuoa/ kuolewa, na unahofu labda ukivaa pete ya ndoa itakuwa ni dhambi, hilo sio kweli, biblia imeorodhesha baadhi ya waaminio waliovaa pete katika kanisa la Kristo. Soma.

Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.

2.2 Maana akiingia katika sinagogi lenu MTU MWENYE PETE YA DHAHABU na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;

2.3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,

2.4 je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu”?

Umeona hapo?. Kwahiyo hakuna dhambi yoyote kuvaa pete ikiwa tu ni kwa lengo la kuitambulisha ndoa, tena zipo faida nyingi katika kufanya hivyo, na mojawapo ni kuzuia usumbufu usiokuwa wa lazima, jaribu kufikiria mwanamke ambaye pengine kaolewa bila pete, halafu anatembea barabarani, ni rahisi kusumbuliwa na baadhi ya wanaume ambao hawajaoa wakidhani kuwa hajaolewa, lakini kama angekuwa na pete mkononi mwake, wale watu wangeiona, na ingekuwa ni rahisi kumwacha apitie wakijua kuwa ameshaolewa mtu Yule.

Kwahiyo ina faida nyingi zaidi ya hasara,

Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa, kuvaa pete pia sio lazima kwa wana-ndoa, inawezekana kanisani kwenu hamna huo utaratibu, au kwenye jamii yenu, au nyie wenyewe hampendelei kufanya hivyo, hiyo bado ni ndoa takatifu iliyopokelewa na Mungu..Hilo nalo ni sawa tu kwasababu katika biblia hakuna masharti yoyote yaliyomkataza/kumruhusu mtu avae au asivae pete.

Wakolosai 3:14 “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

15 Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja…;”.

Hivyo amani ya Kristo iamue ndani yako.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Je! Mwanamke anapaswa afunikwe kichwa anapokuwa ibadani?

MAJONZI YA MTUME PAULO KWA NDUGU ZAKE.

YATAMBUE MAJIRA YA KUJILIWA KWAKO.

NI SALAMA ROHONI MWANGU Lyrics

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

UNYAKUO.

KIAMA KINATISHA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Saimon
Saimon
2 years ago

Good