Nini maana ya “wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto”?

Nini maana ya “wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto”?

SWALI: Biblia inaposema “Na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto” Ina maana gani? (Yuda 1:22).


JIBU: Ukisoma kitabu chote cha Yuda kwa utulivu ambacho ni sura 1 tu, utaona maudhui kubwa iliyoandikwa pale ilikuwa ni kulionya kanisa juu ya kuishindania Imani ambayo walikabidhiwa mara moja tu, (soma binafsi kwa utaratibu utaliona hilo), Na hiyo ni kutokana na kuwa tangu ule wakati  kulizukua wimbi kubwa la manabii wa uongo, ambao walifananishwa na Kora na Balaamu, Pamoja wa watu waovu, mfano wa Sodoma na Gomora na watu wasio na imani (aliowaitwa makafiri), waliojiingiza kwa siri katikati ya kanisa la Mungu, ambao kazi yao ilikuwa ni kuleta  matengano ndani ya kanisa.

Hivyo mtume Yuda alilionya sana kanisa kuhusu watu hawa, na ndipo mwishoni kabisa katika waraka wake akalisihi kanisa, kila mmoja kwa nafasi yake, afanye kazi ya kuwarejesha wengine katika Imani kwa bidii, na ndio hapo akasema..

Yuda 1:22  “Wahurumieni wengine walio na shaka,

23  na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”.

Unaona jambo la kwanza aliwaambia wawahurumie walio katika shaka: Maana yake ni kwamba kuna wapo watu ambao walishaathiriwa na mafundisho ya watu hao waongo, mpaka wakawa na mashaka na Imani, Hivyo watu kama hao aliwasihi, wawahubirie kwa kuwajengea misingi ya Imani tena, ili wasimame, na wasiyumbishwe na uongo unaozagaa huko.

Lakini pia akawaambia..

“na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto”. Hii ikiwa na maana kuwa wapo wengine ambao walikuwa tayari wameshazama kabisa katika udanganyifu wao wa mauti, ni kama vile unamuona mtu ambaye yupo motoni, wewe unadhani njia rahisi kumtoa pale itakuwa ni ipi? Ni wazi kuwa haitakuwa ya kumsihi, au kumwomba, hapana, utatumia maneno ya nguvu na vitendo, kwa kumnyakua kutoka kule motoni ili tu apone kwanza,

Ndivyo ilivyo katika kuwahubiria watu wengine ambao wameshakuwa sugu wa Habari za wokovu (Shetani ameshawapofusha macho), Inapofikia wakati kama huo, injili za upendo na huruma za Kristo hazitawafaa, bali injili za hukumu na ziwa la moto, na mateso ya milele, na dhiki kuu, zinazowangoja watu waovu, ndizo zitakazowatafakarisha Zaidi na kuwageuza.

Kuna watu wanasema, hatupaswi kuhubiri Habari za dhiki kuu, na jehanum ya moto kufanya hivyo ni kuwatisha watu, hivyo inawafanya wawe waoga, wampokee Yesu kwa sababu wanaogopa kwenda kuzimu na sio kwasababu wanampenda.

Ndugu, Ni heri aokoke kwa hofu ya Jehanum, kuliko, upotelee huko milele. Na huko ndiko kuwaokoa wengine kwa kuwanyakua kutoka moto, sio kwa kuwahubiria maneno ya kuwapendezesha, bali kuwaonya na hatari watakayoikuta mbeleni..Na hata hivyo sio uongo, bali ni kweli ndivyo ilivyo kwa watu wote ambao hawatatubu.

Kama biblia inavyosema.

2Wakorintho 5:10 “ Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.

11 BASI TUKIIJUA HOFU YA BWANA, TWAWAVUTA WANADAMU; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia”

Ni kweli kabisa yapo makundi yanayostahili kufundishwa sana juu ya Upendo wa Kristo, kwa mfano watu waliokata tamaa ya Maisha, au mtu aliye katika dhiki na mateso na vifungo vya shetani, au mtu ambaye hamjui Mungu kabisa, au mwenye shauku ya kumjua Mungu, lakini hajui ni wapi pa kuanzia,..Hawa wanastahili injili za Upendo wa Mungu..Ndizo zitakazowafungua na kuwapeleka viwango vingine..

Mathayo 11.28  “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30  kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Lakini lipo kundi lingine ambalo, limeshahubiriwa, na linafahamu kila kitu, lakini bado lipo katika dhambi, pengine ili kuliokoa (kulinyakua kutoka huko liliko) injili inayolifaa ni ile ya Ziwa la Moto wa milele, Na bado tutaendelea kuzihitaji kwa wakati huu wa siku za mwisho.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

JE KIFO NI NINI? NA JE KUNA AINA NGAPI ZA VIFO?

JE NI LAZIMA MKRISTO AOE/AOLEWE?

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments