by Admin | 22 October 2020 08:46 pm10
Shalom,
Bwana atusadie ili kila siku tuzidi kuujua uweza wa Mungu,
Kuna wakati Bwana Yesu aliwaambia viongozi wa dini na watu wote kuwa wanapotea kwasababu moja tu, nayo ni kwasababu hawayajui maandiko na uweza wa Mungu (Mt.22:29).
Nasi Bwana atusaidie tusipotee kwa kukosa kuujua uweza wake.
Na moja ya uweza wake ambao pengine hatuujui ni ule uwezo wa kumlipa mtu, kwa kazi asiyostahili, kwasababu tu katia mkono wake shambani mwake..
Embu tafakari ule mfano alioutoa Bwana juu ya yule mtu mwenye nyumba ambaye aliamka asubuhi ili akawaajiri watu wakafanye kazi shambani mwake, pengine saa 12 asubuhi akaenda akakutana na kundi la kwanza akapatana nalo kiasi Fulani cha fedha, biblia inasema akaenda tena saa tatu akukutana na kundi lingine limekaa tu sokoni halina kazi yoyote, nalo pia akaliambia nendeni shambani, akatoka tena sita na saa tisa, akawakuta wengine wapo hawana kazi, akawaambia nao hivyo hivyo nendeni,, na mwisho wa siku, jioni kabisa ile giza linakaribia kuingia akakutana na kundi lingine ambalo kutwa kuchwa limekaa tu, halina kazi yoyote, nalo pia akaliambia nendeni shambani, mkaangalie kazi ya kufanya,
Ni wazi kuwa hili kundi la mwisho halikukutana na kazi yoyote nzito ya kufanya kule shambani, pengine lilikuwa linakufunga funga tu viroba, viwili vitatu, kwani kazi yote ilishamalizwa na wale wengine ambao walikuwepo tangu asubuhi.
Sasa embu tengeneza picha kidogo kwenye kichwa chako, labda wale wa kwanza walipowaona wanakuja waliwacheka au kuwadharau, au kuwahurumia sana? Pengine wakanong’onezana wakisema kama sisi tutalipwa elfu hamsini hamsini, hawa watalipwa sh. Ngapi? kama sio elfu elfu, Lakini matazamio yao yalikuwa tofauti, wakati malipo yalipofika, Mwenye shamba akaja akawalipa wote, fedha sawa sawa, lakini wale wa kwanza wakamlalamikia mwenye shamba wakimwambia mbona umetulipa sawa na hawa, ambao hawajataabika kwa chochote? Lakini Bwana akawaambia maneno haya;
Mathayo 20:13 “Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
14 Chukua iliyo yako, uende zako; NAPENDA KUMPA HUYU WA MWISHO SAWA NA WEWE.
15 SI HALALI YANGU KUTUMIA VILIVYO VYANGU KAMA NIPENDAVYO? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema”?
Unaona? Ameamua kufanya hivyo kwasababu mali ni yake na sio ya yule aliyeajiriwa..Hivyo akitoa vingi au akitoa vichache, hilo ni lake, wewe hupungukiwi kwa chochote maadamu umelipwa kile ulichokubaliana naye. Bwana aliguswa kuona tu walau wamefanya kitu fulani katika shamba lake, haijalishi wamechelewa kiasi gani.
Hata leo hii, tunapaswa tuujue huu uweza wa Mungu, ili tusijione sisi ni wadhaifu kuliko watu mashuhuri waliomtumikia Mungu huko nyuma, au wanaomtumikia sasa, tusijione sisi hatuwezi kulipwa sawa na mitume, tusijione sisi hatuwezi kulipwa sawa na manabii,..Hilo wazo tulifute, Bwana alipatana na mitume wake kuwa katika ulimwengu ujao wataketi katika viti 12 wakihukumu makabila 12 ya Israeli,
Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli”.
Hilo ni kweli kabisa lakini hata mimi na wewe Bwana anaweza kutuketisha pamoja nao, tukayahukumu mataifa, na mitume wasiwe na la kumlaumu Bwana. Kwasababu ni haki yake kutumia vilivyo vyake kama apendavyo. Alisema hivyo pia katika ufunuo..
Ufunuo 3:21 “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi”
Hivyo ndugu yangu tusipotee kwa kutokujua uweza wa Mungu. Unaweza ukajiona umechelewa, pengine umeshakuwa mzee wa miaka 70, unajiuliza hata nikimtumikia Mungu nitakwenda kupata thawabu gani kule? Wewe itende tu kazi yake, maadamu upo shambani kwa sasa endelea kuifanya kwa uaminifu kwa huu muda mchache uliobakiwa nao..Kwasababu huujui uweza wa Mungu!..Thawabu zinatoka kwake na sio kwa mwanadamu, hivyo ukitumika kwa uaminifu, nani ajuaye utapata kilicho sawa na mitume.
Hata na sisi sote pia, kila mmoja wetu, ni kweli kuna mahali amezembea au amechelewa, kuingia shambani mwa Bwana. Amekuwa kama wale wa saa kumi na moja jioni. Sasa huu sio wakati wa kuanza kujilaumu, au kujiona hufai.. Kumbuka hata kama ungekuwa umebakisha wiki moja uondoke duniani, na umeokoka, tafuta kazi ya kufanya ya Bwana, usikae tu hivi hivi, jibidiishe, kwa lolote kwa chochote uhakikishe injili inasonga mbele. Kwasababu hata Bwana hakuwalipa watu ambao hawajafanya chochote.
Na suala la malipo muachie yeye. Ni haki yake kutumia vya kwake kama apendavyo,
Hivyo sisi tuliookoka, tuamke sasa tuanze kwa Bwana kwa hari nyingine mpya. Na wewe ambaye bado upo nje ya Kristo, mlango wa neema upo wazi, lakini hautakuwa hivi sikuzote, njoo kwa Yesu ayabadilishe maisha yako, njoo uokolewe, uoshwe dhambi zako, dunia hii inakwenda kuisha, tunaishi katika dakika za nyiongeza tu. Unyakuo wa kanisa upo karibu, jiulize ukifa leo katika dhambi utaenda kuwa mgeni wa nani huko uendako??
Hivyo tubu, na kama hujabatizwa ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako mapema kabisa, ikiwa utahitaji huduma hiyo unaweza kuwasiliana nasi,. Na baada ya hapo anza kuishi maisha yanayolingana na wokovu.
Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema; Mafarisayo Hupanua HIRIZI zao, na kuongeza MATAMVUA yao?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/22/kumbe-mungu-anaweza-kukulipa-kwa-usichostahili/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.