by Admin | 7 November 2020 08:46 pm11
SWALI: Naomba kufahamu kuwatema farasi maana yake ni nini?. Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wakati mwingine wawateme farasi za maadui wao vitani?
Neno hilo tunalisoma katika kifungu hiki;
Yoshua 11:6 “Bwana akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; UTAWATEMA FARASI ZAO, na magari yao utayapiga moto.
7 Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia.
8 Bwana akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia.
9 Yoshua akawafanyia vile vile kama Bwana alivyomwamuru; AKAWATEMA FARASI ZAO, na magari yao akayapiga moto”.
Kama tunavyojua Yoshua na wana wa Israeli walipovuka Yordani walikutana na maadui zao wengi kule Kaanani, maadui ambao walikuwa na uzoefu mkubwa wa kivita, na wenye majeshi mengi. Na hapa tunaona wana wa Israeli walipofika sehemu moja walikutana na huyu adui yao mmoja “Yabini” mfalme wa Azori ambaye hakumwendea peke yake bali alikwenda kukusanya nguvu kutoka katika mataifa ya kando kando yake ili yamsaidie kummaliza Yoshua na wana wa Israeli wote kwa ujumla,na biblia inasema lilikuwa ni jeshi kubwa kama mchanga wa bahari, wenye magari mengi ya vita na wafasi wengi sana.
Lakini utaona hapa Mungu anampa maagizo Yoshua na kumwambia kuwa watakapowapiga wasichukue chochote bali wayachome magari yao ya vita na wawateme farasi zao.
Kutema farasi maana yake nini?
Kutema ni kujeruhi tishu za misuli ya miguu, ambazo zinasababisha mtu au mnyama kuweza kutembea, au kukimbia au kuruka au kupanda. Tishu hizo ngumu kwa mwanadamu au kwa mnyama zipo sehemu ya nyuma ya miguu kuanzia kwenye paja hadi kwenye goti, na kwa mnyama vivyo hivyo kwenye miguu yake ya nyuma.
Tishu hizo zikikatwa huwa haziponyeki, na mtu au mnyama unakuwa mlemavu wa kudumu. Hawezi kukimbia, au kuruka au kutembea.
Hivyo ilikuwa ni desturi za kivita zamani na hata sasa, farasi wa kivita, wasiohitajika, hawakuachwa hivi hivi bali walitemwa (walikatwa tishu hizo) ili kusudi kwamba wasije tumiwa kwa vita tena na maadui zao. Kwahiyo wanyama hao walibakia kuwa hawana kazi yoyote tena baada ya hapo.
Sasa ni kwanini Mungu hakuwaruhusu wana wa Israeli wawachukue farasi wale, wawasaidie pengine kwa ajili ya vita vilivyokuwa mbele yao, lakini badala yake akawaamuru wawateme?
Ni kwasababu Mungu alitaka tegemeo lao liwe kwake na sio kwenye silaha au majeshi..Na kwamba wajue kuwa yeye huwa haikoi kwa silaha au kwa majeshi bali kwa Roho wake.
Daudi alisema..
Zaburi 20:7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu”.
Na kama tunavyoona, wana wa Israeli hawakutumia magari wala farasi mahali popote walipovuka Yordani, lakini waliogopwa na maadui zao wote waliowazunguka, hiyo ni kwasababu walimtumaini Mungu peke yake ambaye angeweza kuwaokoa.
Vivyo hivyo na sisi, tukitaka tumshinde shetani kabisa kabisa au maadui zetu, hatupaswi kuweka tumaini letu kwa wanadamu au kwenye mali au chochote kile, bali tuweke tumaini letu kwa Yesu Kristo Bwana wetu, awezaye kutuokoa. Huku tukiwa tumezavaa silaha zote za haki (Waefeso 6) ili kusudi kwamba shetani akitaka kututema, sisi ndio tuwe wa kwanza kumtema yeye, Kwa jina la Yesu.
Bwana akubariki.
Je! Yesu akirudi leo unao uhakika wa kwenda naye? Je! Unahafahamu kwa hizi ndio zile nyakati ambazo biblia ilitabiri kutakuwa na makundi mawili ya wakristo? (yaani wanawali werevu na wanawali wapumbavu Math. 25) ambao wote wanadai wanamngojea Bwana? Lakini wale wapumbavu waliikosa karamu kwasababu hawakuwa na mafuta ya kutosha katika taa zao. Hivyo nyakati hizi kigezo cha kusema wewe ni mkristo pekee haitoshi, kusema wewe umeokoka haitoshi, unapaswa ujiulize ni nini kinachonipa uhakika ndani yangu kuwa Kristo akirudi leo nitakwenda naye?
Je! Mafuta ya Roho Mtakatifu yaliyo ndani yangu yaninitosha au yalishakwisha siku nyingi?
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/07/kuwatema-farasi-maana-yake-ni-nini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.