MTEGEMEE MUNGU, NA SI MWANADAMU.

MTEGEMEE MUNGU, NA SI MWANADAMU.


Yeremia 17:5 “ Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. 

6 Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.”

Jina la Bwana libarikiwe, Biblia inasema amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana.

Matokeo ya kumwacha Mungu moyoni ni kumtegemea mwanadamu, unapoamini kuwa mtu fulani ndio kashikilia hatma ya Maisha yako, huko ni kumtegemea mwanadamu…

Unapoziamini methali za wanadamu na kuliacha Neno la Mungu huko ni kumtegemea mwanadamu, Unapoamka asubuhi na jambo la kwanza ni kumfikiria boss wako na hata humshukuru Mungu kwa kukuamsha salama, huko ni kumtegemea mwanadamu,

Unapotii maagizo ya watu fulani waliokuzunguka na kuyadharau maagizo ya Mungu, kwa kisingizio usipotii utakosa kazi, utakosa fursa, utakosa heshima, utakosa hadhi. Huko ni kumtegemea mwanadamu na hivyo ni kujikuta unaishi katika laana.

Biblia inasema pia amelaaniwa mtu yule amfanyaye mwanadamu kuwa KINGA YAKE. Unapomtegemea mtu fulani asilimia mia kama mlinzi wako, au kama tumaini lako, ni kuishi chini ya laana…Unapomtegemea mlinzi wako wa getini na kujitumainisha na walinzi wanaokuzunguka ni kujiweka chini ya laana, ndio! Utakuwa na walinzi sio dhambi…lakini kuweka tumaini lako la kwanza juu yao..na kusema wao, wasipokuwepo wewe umekwisha..Ni kuishi chini ya laana, Biblia inasema..

Zaburi 127 :1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. 2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi”.

Unapowaamini madaktari asilimia mia kwamba uzima wako upo juu ya elimu yao, na utaalamu wao, na huku moyoni mwako Imani na Mungu imepotea kabisa, huko ni kumtegemea mwanadamu hivyo ni kujiweka chini ya laana…Elimu ya udaktari yote haiwezi kutibu kifo, lakini yupo mmoja awezaye kuwafufua waliokufa, huyo ndio wa kumtegemea hivyo kujitumainisha kwa madawa, au kwa mahospitali na huku moyoni mwako Mungu hana nafasi..ni kuishi chini ya laana, mwisho wa siku daktari akitoa ripoti hii kuwa una siku kadhaa za kuishi, au wiki kadhaa, unapaniki sana, hiyo ni hatari sana…… madaktari wanapaswa wawe tu ni vyombo ambavyo Mungu anavitumia kutuhudumia, lakini sio waponyaji wako, wala watu wanaostahili kuchukua heshima ya Mungu, kwasababu Mungu anaweza kutumia njia nyingine kukuponya bila kutumia hao..hivyo tumaini letu lote ni kutoka kwa Bwana.

Lakini pia Biblia inasema..

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.

8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

Ukimfanya Bwana ndio jawabu lako la mwisho, na kumwamini yeye kuwa ndio kila kitu…Neno linasema utakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya maji..hautaona hofu wakati wa hari (jua/kiangazi)..wala hautahangaika wakati wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda…

Dalili ya kwanza ya kujipima kama unamtegemea mwanadamu au la ni hofu ya Maisha!! Ukishaanza kuona una hofu fulani ya Maisha kuogopa unaweza kupatwa na jambo fulani baya kutoka kwa watu, usipofanya kitu fulani…labda usipotoa rushwa, au usipokubali kushirikiana nao kwenye jambo fulani na watu fulani, au usipojaribu kufuata njia zao au kuishi kama wao, au kuishi kama wanavyotaka,au kuvaa kama wao, unaanza kuwa na hofu ya kufa, au hofu ya Kesho itakuaje, nitavaaje, nitakulaje, nitaishije!…hizo ni moja ya dalili za kumtegemea mwanadamu…lakini wote wanaomtegemea Bwana biblia inasema hawatakuwa na hofu, hawatakuwa na wasiwasi kuwa Kesho,au Kesho kutwa watakosa riziki, wanajua kabisa katika shughuli zao Mungu atakuwa pamoja nao tu hata kama leo wanajiona hawana kitu, wanajua Kesho Mungu atafungua njia itapatikana tu! Hivyo hawapepeswi na maneno wala upepo wa hofu za Maisha haya…

Wakitishiwa kuwa watafukuzwa kazi wasipofanya jambo fulani, hilo haliwababishi, wakitishiwa kuwa watahatarisha kazi zao wasipomtii boss wao kwenda kumkusanyia rushwa hawaweweseki, kama Danieli alivyozingirwa na maadui waliompangia mabaya kwa mwenendo wake wa kukataa kula rushwa..

Biblia inasema pia mtu yule amtegemeaye mwanadamu hataacha kuzaa matunda, kwanini? kwasababu anakuwa kama amepandwa kando kando ya mto…Na kuzaa matunda kuko kwa namna Mbili..kuzaa matunda ya mwili kama kufanikiwa katika mambo yote ya mwilini…shughuli na kazi zinakuwa zinafanikiwa, na pia uzao wa tumbo unabarikiwa, na namna ya pili ni kuzaa matunda ya roho, ambayo ni upendo, upole, kiasi, uvumilivu, Fadhili, furaha, amani, n.k (Wagalatia 5:22) pamoja na kuwaleta watu kwa Kristo, ambayo thawabu yake ni juu mbinguni.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KITABU CHA UKUMBUSHO

NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

TWEKA MPAKA VILINDINI.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments