Kwanini  vizazi vya ukoo wa Yesu vinajipinga katika Mathayo na Luka.

by Admin | 9 December 2020 08:46 pm12

Kwamfano tukisoma katika injili ya  Mathayo, tunaona, mwandishi anaanza kueleza ukoo wa Yesu tangu Ibrahimu Mpaka Yusufu, lakini alipofika kwa  Daudi, aliendelea na kusema Daudi akamzaa Sulemani, (Mathayo 1:6)..Lakini tukirudi tena kwenye Luka hapo hapo tunaona Daudi alimzaa Nadhani (Luka 3:31), Hiyo ni kuonyesha kuwa Yesu alipitia uzao wa Nathani na sio wa Sulemani, kulingana na Luka. Lakini Mathayo anasema alipitia kwenye uzao wa Sulemani, kwanini iwe hivyo?

Pia ukisoma tena mwishoni utaona kulingana na Injili ya Mathayo, baba yake Yusufu alikuwa ni  Yakobo, lakini Luka anatuambia baba yake Yusufu alikuwa ni Eli (Luka 3:23).. Naomba ufafanuzi juu ya hili.

JIBU: Ni wazi kuwa ukisoma kitabu cha Mathayo na kile cha Luka utaona kuna tofauti kubwa kwenye vizazi vya ukoo wa Yesu. Luka anatuambia baba wa Yusufu alikuwa ni Eli, na Mathayo inasema babaye alikuwa ni Yakobo. Lakini je! Hilo linamaanisha biblia inajipinga?

Jibu ni la! Ikumbukwe kuwa zamani katika taifa la Israeli walikuwa na desturi  ya mtu kumnyanyulia ndugu yake uzao, na mtoto huyo kuitwa kwa jina la marehemu ikiwa mtu huyo atakufa kabla hajapata mtoto.. Soma. Kumbukumbu 25:5-6,

Kwamfano, kama wewe ni mwanaume umezaliwa katika familia, na ukaoa, lakini kwa  bahati mbaya ukafa bila kupata mtoto, basi anatafutwa ndugu yako wa karibu aidha katika familia au katika ukoo, Yule aliye karibu zaidi  na wewe, kisha anakwenda kumuoa huyo mke wako uliyemwacha, kisha anamzalia mtoto, lakini huyo mtoto hataitwa kwa jina lake, bali ataitwa kwa jina lako wewe marehemu, haijalishi kuwa watoto huyo watakuwa wametoka katika viungo vya mtu mwingine. Na Wanafanya hivyo ili kulitunza jina lako lisipotee.

Na ndicho walichokifanya Israeli wakati ule, ndicho alichokifanya Boazi kwa Ruthu, (ukisoma Ruthu 4:6-9)

Sasa tukirudi katika Injili. Mathayo aliandika Uzao wa Yusufu (Babaye Yesu), akifuata ubaba  wa kibaolojia, na Luka aliandika uzao wa Yusufu akifuata ubaba wa kijina.

Ikiwa na maana kuwa Eli pengine alikufa kabla ya kupata mtoto, hivyo Yakobo akamchukua mke wake, na kuzaa naye ili kumtunzia jina, ndipo akamzaa Yusufu. Hivyo kibaolojia Yusufu alikuwa ni mtoto wa Yakobo lakini kisheria alikuwa ni mtoto wa Eli.

Na ndio maana Yakobo hatajwi katika injili ya Luka, bali ni Eli.. Lakini Mathayo anamtaja Yakobo Kama baba wa Yusufu lakini kibaolojia. Hivyo maandiko yapo sawa.

Kwafaida ya asiyekuwa na biblia anaweza kuvipitia, vifungu hivyo vya biblia hapa chini:

Mathayo 1:1-16

1 Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.

2 Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake;

3 Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu;

4 Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni;

5 Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese;

6 Yese akamzaa mfalme Daudi.

7 Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;

8 Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia;

9 Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;

10 Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia;

11 Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.

12 Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;

13 Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori;

14 Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi;

15 Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo;

16 Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.

Na..

Luka 3:23-38

23 Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,

24 wa Mathati, wa Lawi, wa Melki, wa Yana, wa Yusufu,

25 wa Matathia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esli, wa Nagai,

26 wa Maathi, wa Matathia, wa Semei, wa Yusufu, wa Yuda,

27 wa Yoana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Shealtieli, wa Neri,

28 wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Eri,

29 wa Yoshua, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Mathati, wa Lawi,

30 wa Simeoni, wa Yuda, wa Yusufu, wa Yonamu, wa Eliakimu,

31 wa Melea, wa Mena, wa Matatha, wa Nathani, wa Daudi,

32 wa Yese, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nashoni,

33 wa Aminadabu, wa Aramu, wa Hesroni, wa Peresi, wa Yuda,

34 wa Yakobo, wa Isaka, wa Ibrahimu, wa Tera, wa Nahori,

35 wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,

36 wa Kenani, wa Arfaksadi, wa Shemu, wa Nuhu, wa Lameki,

37 wa Methusela, wa Henoko, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,

38 wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

JE BWANA WETU YESU ALIKUWA NI MZUNGU?

Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao?

JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/09/kwanini-vizazi-vya-ukoo-wa-yesu-vinajipinga-katika-mathayo-na-luka/