by Admin | 16 December 2020 08:46 pm12
Mfalme wa kwanza wa Israeli alikuwa anaitwa Sauli. Mungu alivyomchagua mtu huyu, ilikuwa ni nje ya matarijio ya waisraeli wengi sana. Kwasababu ikumbukwe hapo kabla walikuwa hawana mfalme, hivyo baada ya kuona mataifa mengine yaliyokuwa yanawazunguka yana wafalme hodari na mashujaa na wao pia wakaingiwa na tamaa wakamwomba Mungu awapatie mfalme. Jambo ambalo halikuwa mapenzi ya Mungu, lakini Mungu aliwapa tu hivyo hivyo haja ya moyo wao. Ndipo akawapa huyu Sauli
Sasa, Sauli, alikuwa ni mtu mlaini laini tu, mtu ambaye sio machachari, mtu ambaye, huwezi kumwita shujaa hata kwa sura yake tu, kwa lugha ya kisasa wengine watamuita mtoto wa mama tu. Hiyo ni kweli kwasababu biblia inatuambia hata yeye mwenyewe alijiona ni dhaifu machoni pake mwenyewe Soma 1Samweli 15: 17
Hata siku aliyopokea unabii kutoka kwa Samweli kuwa atakuwa mfalme alishangaa mwenyewe..Jaribu kutengeneza picha, wewe hujui mambo ya siasi, wala hujawahi kuwa na ujuzi wowote wa uongozi, halafu siku moja Mungu anakuambia mwezi ujao utakuwa raisi.. Unaweza kusema Mungu kakosea kunichagua mimi.. amchague mwingine!! Ndicho alichokifanya hata Musa wakati ule alipoitwa na Mungu, alikuwa dhaifu machoni pake mwenyewe, na ni kweli ndivyo ilivyokuwa, lakini uchaguzi wa Mungu ulikuwa juu yake, haijalishi hali ya udhaifu aliyokuwa nayo.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Sauli wakati ule alipokuwa anakwenda kutafuta punda wa baba yake waliopotea, ndipo katika kutembea tembea kwake akafika kwa Nabii Samweli ndipo akamtolea unabii huo.. Sasa moja ya maneno aliyoambiwa na Samweli yalikuwa ni haya..
1Samweli 10:6 “na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, NAWE UTATABIRI PAMOJA NAO, NAWE UTAGEUZWA KUWA MTU MWINGINE.
7 Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe”.
Unaona aliambiwa asiogope, pindi tu Roho ya Mungu itakaposhuka juu yake, atageuzwa moyo na kuwa mtu mwingine kabisa..hatakuwa Sauli Yule wa kwanza tena.
Jambo hilo Israeli hawakulielewa bali waliendelea tu kumdharau Soma (1Samweli 10:27), mpaka siku moja ambayo maadui zao wamesimama wanataka kuwachukua mateka na hawajui cha kufanya, wanalia tu, bila matumaini yoyote ndipo wakamwona Sauli Yule mtoto wa mama anasimama kwa ujasiri wa ajabu ambao hawakuwahi kuuona kwake hapo kabla, halafu anatoa amri kuwa watu wote watakwenda vitani na mtu asipokwenda naye mifugo yake yote itauliwa. Soma 1Samweli 11 yote.
Na kweli walienda vitani na ushindi wakaupata, ndipo kuanzia huo wakati watu wakamwogopa na kumuheshimu Sauli. Biblia inatueleza ushujaa wa Sauli ulikuwa mkubwa sana, mpaka siku anayokaribia kufa..
Ni nini ninataka ukione siku ya leo?
Ilihitaji Roho wa Mungu kumfanya Sauli kuwa mtu mwingine, ilihitaji Roho Mtakatifu kumfanya Sauli kuwa Mfalme atakayeweza kuichunga Israeli. Vivyo hivyo na leo hii, itamuhitaji Roho Mtakatifu ndani ya mtu ili aweze kufanywa kiumbe kipya, aweze kufanya mtu mwingine, aweze kushinda ya ulimwengu huu, aweze kuushinda uzinzi, na ulevi, na anasa. Vilevile aweze kuyashinda majaribu yote ya shetani, yeye peke yake kwa nguvu zake, hataweza hata afanyaje, anahitaji msaada wa Roho nyingine itakayo juu.
Zekaria 4: 6b “..Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi”.
Na ndio maana kuna umuhimu wa kuzaliwa mara ya pili. Pale mtu anapozaliwa mara ya pili, hapo hapo Roho wa Mungu anashuka ndani yake. Na uwezo huo anaupokea.
Je! Mtu anazaliwaje mara ya pili?
Ni kwa kutubu dhambi zake, kisha kubatizwa, na kuanza kuishi maisha yanayoendana na toba yake. Na anapokuwa katika hali hiyo , Roho wa Mungu anashuka juu yake, na hapo anakuwa tayari amezaliwa mara ya pili.
Matendo ya Mitume 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.
Je! Na wewe unataka kupokea uwezo huu wa kufanywa mtu mwingine, uwezo wa kuishinda dhambi kirahisi? Uwezo wa kuyavuka majaribu ya adui?.. Basi tubu,dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha ukabatizwe katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, ikiwa jambo hilo halijawahi kufanyika kwako ipasavyo. Na baada ya hapo Mungu atakumwagia kipawa chake cha Roho Mtakatifu. Na wewe mwenyewe utaanza kuona badiliko lingine ndani ya maisha yako. Kiu ya mambo mengi utaona imekata, n.k. ukiona hivyo ujue hapo tayari Roho kashaanza kukuunda upya.
Fanya hivyo na Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/16/nawe-utageuzwa-kuwa-mtu-mwingine/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.