by Admin | 21 December 2020 08:46 pm12
Leo tutajifunza jinsi gani matatizo yetu yanavyoweza kuweza kutupofusha hata tusiione miujiza yetu.
Kuna wakati Mungu, anakuwa ameshakwisha anza tayari kututendea miujiza, lakini kutokana na kuwa tunayapa sana matatizo yetu uzito mkubwa kuliko yanavyostahili, inatupelekea hata miujiza yenyewe tuiione kama si kitu pale inapoanza kuja.
Embu fikiria wakati Kristo alipokufa na kulazwa pale makaburini, tunaona kuna mambo mengi yalikuwa yanaendelea pale, lakini kikubwa ambacho tunaweza kujifunza leo ni lile tukio la Mariamu Magdalene. Yeye alipofika pale alianza kulia kwa uchungu, akifikiria miujiza yote aliyotendewa na Yesu tangu akiwa duniani, akifikiria jinsi alivyoishi maisha ya haki na upendo usiokuwa na unafiki, wala hakufanya kosa lolote, na leo hii, anaona wamemuua, tena afadhali ingekuwa wamemuua na kumsulubisha tu, na kumwacha, lakini safari hii wameuiba mpaka na mwili wake pia, hilo ndio lililomfanya alie sana kwa uchungu, kiasi cha kumfanya ashindwe kuondoka pale aendelee tu kulia,
Lakini biblia inatuambia muda si muda, akiwa amesimama pale anachungulia ndani ya kaburi ghafla aliwaona malaika wawili, wamekaa, mmoja kichwani pa mahali walipomlazia Yesu na mwingine, miguuni..Lakini wale malaika wawili wakamuuliza swali, Mama unalilia nini?
Yohana 20:11 “Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. 12 Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu.
13 Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka”.
Fikiria, ule uchungu wa mawazo ulimfanya hata asahau kuwa wale ni malaika wa Mungu, Uchungu wa kuibiwa kwa Bwana kulimfanya hata asifikirie wale watu wawili wenye mavazi yaliyong’aa meupe wametokea wapi muda ule, na wanafanya nini pale..Yeye moja kwa moja anaanza kuzungumza nao kama vile, ni watu wa kawaida anaokutana nao barabarani siku zote.
Kama hilo halitoshi, wakati anaendelea kulia pal, nje, akamwona Tena mtu mwingine anatembea tembea karibu yake,(hakujua kama ndiye Yesu) ndipo Yesu akamuuliza swali lile lile aliloulizwa na wale malaika..Mama unalilia nini?..
Yohana 20:15 “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.
16 Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu)”.
Unaona, Yesu alipogeuka na kumshtua MARIAMU!!!..Ndipo akabutuka na kugundua kuwa Yule ni Yesu aliyesimama mbele yake. Kama asingeshtuliwa, bado angeendelea kukaa katika majonzi yake tu, analia lia ovyo wakati Yesu anazungumza na yeye.
Wakati mwingine matamanio yetu yanakuwa makubwa kupitiliza, mpaka yanatupofusha tunashindwa hata kuona miujiza ya Mungu, kama sio kumwona Mungu mwenyewe.
Jambo kama hili utaliona kwa Balaamu pia, wakati ule anataka kwenda kuwalaani Israeli, alipokuwa njiani, punda wake alifunguliwa kinywa na Mungu, na kuanza kuongea naye.. Sasa yeye kwasababu moyo wake wote tayari ulikuwa kule anapoelekea, kuwalaani Israeli, hata kuzungumza na Punda hakuona kama ni muujiza ule, badala yake akaanza kuzungumza naye kama anavyozungumza na mwanadamu mwenzake tu..Kama alivyofanya Mariamu.
Hesabu 22:28 “Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?
29 Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.
30 Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!
31 Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi”.
Umeona? Pengine na wewe umekuwa ukizitazama sana shida zako, kuliko kuutazama uweza wa Mungu. Pengine ipo miujiza mikubwa Mungu ameshaanza kukufanyia lakini huwezi kuiona kwasababu wakati wote ukienda kwa Mungu unatazama tu ukubwa wa shida zako, na sio uweza wa Mungu.
Unasahau kuwa ni Malaika wa Bwana wamesimama pale pale unapopalilia, unasahau kuwa ni Yesu mwenyewe mkuu wa Uzima, amesimama pembeni yako kuzungumza na wewe na wewe juu ya hilo tatizo lako, lakini wewe unalia tu.. Leo nakuambia tuliza moyo wako, usilie mahali ambapo tayari Mungu ameshakusikia, bali, mshukuru yeye, zungumza na yeye, utaona miujiza mingi ambayo tayari ameshaanza kukufanyia katika maisha yako.
Mungu akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/21/mama-unalilia-nini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.