FAHAMU UWIANO MUNGU ANAOHITAJI KUUONA KWETU.

by Admin | 11 January 2021 08:46 pm01

Ipo kanuni moja ya Mungu, ambayo ni vema sisi sote tukaifahamu. Kanuni hiyo ni kuwa Mungu huwa hafanyi mambo yote peke yake, japo anaouwezo wa kutenda mambo yote yeye mwenyewe, lakini ni kanuni aliyojiwekea kwamba sehemu kubwa aitende yeye mwenyewe, na abakishe sehemu ndogo sana ambayo atashirikiana na viumbe vyake, au mwanadamu kuitenda.

Kwamfano Pale Edeni, Mungu alishaiumba kila kitu, angeweza kumwacha Adamu awe anakula tu, na kuisha maisha yake ya starehe kwa milele yote, lakini utaona alimpa Adamu jukumu dogo sana la kuilima na kuitunza bustani yake, jambo ambalo Mungu angeweza kulifanya yeye mwenyewe, kama aliweza kuimba dunia, angeweza pia kuilima na kuitunza bustani ile peke yake, mwanadamu aishi kwa raha siku zote.

Vivyo hivyo hata katika miili yetu hii aliyotupa, sote tunajua ni mali yake, lakini sio kila kitu anakifanya yeye peke yake, asilimia kuwa ni yeye ndio anayeitunza miili yetu, kwamfano ukitafakari, mapigo ya moyo yeye ndio anayeyashughulikia yaende katika mpangilio alioutaka, wewe hauhusiki na kitu chochote hapo,  kukuza nywele, au kucha, huelewi chochote, au kusukuma damu, jambo hilo halikuhusu hata kidogo, kana kwamba sio sehemu ya mwili wako n.k., Sasa fikiria mambo magumu kama hayo anaweza kuyafanya unadhani anashindwa kabisa kukuogesha kila siku, wewe ukiamka tu asubuhi tayari ni msafi? Au kukulisha chakula, wewe ukiamka tayari tumbo limejaa? Au kukutundikia dripu la maji ndani ya mwili wako kiasi kwamba ukipungukiwa na maji kidogo tu lenyewe tu linashusha, na hivyo hakuna haja ya kwenda kutafuta maji nje?..Kwanini aruhusu mpaka uanze kuteseka uandae chakula ule, na wakati mwingine kwenda kujisumbua kutafuta?

Hiyo yote ni kwasababu, Kanuni ya Mungu, ndivyo ilivyo kwetu sisi wanadamu, yeye mwenyewe kachagua afanye kwa sehemu kubwa, na ile sehemu ndogo sana ashirikiane na sisi kufanya.. Huo ndio uwiano wa Mungu. Na kama mtu akiipuuzia sehemu hiyo ndogo asiifanye, ajue kuwa matatizo makubwa sana atakumbana nayo, kama sio kifo kabisa.

Vivyo hivyo na mambo ya rohoni, tunajua kabisa Mungu ndio kila kitu kwetu, yeye ndio msaada wetu, yeye ndio tegemeo letu, yeye ndio kila kitu kwetu, pasipo yeye sisi hatuwezi kufanya lolote, yeye ndiye anayejua kesho yetu, anayejua tutalalaje, tutaamkaje, Tunajua kabisa Mungu anatupigania na kutushindania kwa mambo mengi, mengine hata hatujui, lakini  pia katika hayo yote tupaswa kujua pia yapo mambo mengine anataka tushirikiane naye, ili vyote viende sawa sawa. Vinginevyo tukivipuuzia, tukasema tunamwachia Mungu kila kitu, tujue kuwa tutapata matatizo makubwa sana, hata vile vingine ambavyo Mungu anatutendea yeye mwenyewe bila kutushirikisha tunaweza tusivipate.

Ni sawa na kusema, Mungu ananikuza, anadundisha mapigo yangu ya moyo, anachuja damu yangu kwenye figo, pasipo kujishughulisha hivyo ngoja nisiende pia kujipikia chakula nile , kwani nitashiba tu mwenyewe.. Hapo utakufa ndugu yangu, haijalishi kuwa Mungu anakuhudumia kiuaminifu kwa hayo mengine usiyoyasumbukia. Huo utakuwa ni uvivu uliopindukia.

Ndio maana andiko hili linasema..

Mithali 26:15 “Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake”.

Sasa na rohoni nako vivyo hivyo, yapo mambo ambayo itakuhitaji wewe ufanye ili Mungu aende na wewe.. Na jambo mojawapo ni “MAOMBI” ikiwa  wewe sio mwombaji,  na umeokoka halafu unajidanganya kwa kusema Mungu anajua haja ya moyo wangu kabla hata sijaomba sawasawa na Mathayo 6:32, hivyo atanisaidia tu, mimi siombi, au naomba nikijisikia, kwani mimi ni mteule wake, siwezi potea..ukae ujue kuwa, Utapata hasara kubwa sana ya roho yako kipindi sio kirefu.

Bwana Yesu alivyosema, kesheni mwombe, alikuwa anamaanisha tuombe kweli kweli, kama yeye alikuwa ni mkamilifu, hana kosa lolote aliomba, inatupasaje sisi miti mikavu? Wakati mwingine Mungu anasimama kama jemedari wetu vitani, akitarajia tupigane pamoja naye, tushike panga pamoja naye, tukate pamoja naye,  sio tukae tukimtuzama akitupigania kila siku.

Kama utasubiria Mungu akulinde na washirikina, akutete kwenye mambo yako, akunyanyue katika huduma yako, akufanyie hiki, au kile,  na huku huombi, au hujibidiishi kwake, ukajidanganya kuwa umeokoka, hapo hesabu kuwa umepotea.

Vivyo hivyo katika kuifanya kazi ya Mungu, kuna wengine wanasema, Walio wake watakuja tu, wakisimamia andiko hili, 2Timotheo 2:19. Hivyo hawataki kujishughulisha na jambo lolote la ki-Mungu, hata kufagia uwanja wa kanisa. Ni kweli walio wake watakuja kwasababu Mungu anazo njia nyingi sana za kuwakomboa watu, wake. Lakini ipo asilimia ya huduma yake kaiweka ndani yetu sisi. Ambayo tunapaswa tuitimize. Ili tuweke ule uwiano anaouhitaji.

Lakini tusipoitimiza tukakaa tu hivi hivi,tujue kuwa tupo hatarini sana kufa kiroho. Hata kama tutaona leo hii Mungu anatushindania katika mambo yetu mengi, tujue tu kesho yetu itafika ukingoni. Tutarudi nyuma.

Kwahiyo tukae tukijua kuwa, ili ukristo wetu uende sawasawa, tutambue wajibu wetu na majukumu yetu kwa Bwana, kama vile Bwana anavyoyatambua majukumu yake, na wajibu wake kwetu, lakini kama upande wetu utasua sua, tufahamu kuwa, Mungu hataweza kutembea na sisi hata kidogo.

Hivyo Bwana atutie nguvu, tuwe waombaji, na pia tuone ni nini tunaweza kufanya kwenye kazi ya Mungu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

AINA TATU ZA WAKRISTO.

KIKWAZO CHA EUODIA NA SINTIKE.

Maherodi walikuwa ni akina nani, Na kazi yao ilikuwa ni ipi?

ANGALIENI MWITO WENU.

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

KWANINI KRISTO AFE?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/11/fahamu-uwiano-mungu-anaohitaji-kuuona-kwetu/