Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.(Zab 119:105)
Leo tuwatazame wanawake hawa wawili ambao tunaona Mtume Paulo,akiwataja kipekee zaidi katika biblia kutokana na bidii yao kwa Bwana. Mmoja aliitwa Euodia na mwingine Sintike. Mtume Paulo anasema wanawake hawa walishindania injili pamoja naye, hii ikiwa na maana bidii yao iliwazidi hata wanawake wengine wote, walikuwa tayari kutumika katika kanisa la Mungu, kama wanawake katika nafasi zao kwa uaminifu pengine bila kuvutwa na mambo mengi, walikuwa tayari kuwatazama kwa bidii wanawake vijana na wazee, pengine sio tu kwenye kanisa hilo moja la Filipi, bali hata kwenye makanisa mengine ya Makedonia, pengine walikuwa tayari kujitoa katika kuhimiza michango kwa ajili ya kazi za mitume, na injili kwa ujumla, walikuwa waombaji wazuri na wafungaji n.k.
Hivyo sifa zao zilivuma sana, mpaka tunaona hapa mtume Paulo akiwataja kwenye nyaraka zake. Lakini walikuwa na dosari moja, ambayo leo hii ni vizuri wanawake wote watakatifu wanaomcha Bwana wakaifahamu kwasababu ipo hata sasa katika kanisa.
Wafilipi 4:2 “Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, WAWE NA NIA MOJA KATIKA BWANA. 3 Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami,….”
Kama tunavyoweza kuona hapo pamoja na bidii yao, walikuwa wanatofautiana kwa mambo kadha wa kadha. Pengine, mmoja alimdharau mwingine, hivyo wakawa hawasikilizani, kila mmoja akawa anafanya kazi kivyake, hata mahali ambapo wangepaswa waunganishe nguvu kwa pamoja watumike, ili kumpiga shetani vizuri, walishindwa kutokana na tabia yao ya kudharauliana, unaona, pengine mmoja alisikia maneno fulani kutoka kwa mwingine akizungumziwa vibaya, na hiyo ikawafanya wasusiane, unaona na mambo mengine kama hayo. Ikawafanya kila mmoja atumike kivyake. Lakini Mtume Paulo alikuja kuwasii kwa waraka wawe na Nia moja.
Wanawake hawa wanawakilisha makundi mbalimbali ya wanawake waliookoka kanisani, Sikuzote ni wanawake ndio wanakuwa wazito katika kushirikiana, utakuta ni kweli anayobidii kwa Mungu, wanamtumikia Mungu kwa moyo wake wote, lakini kuwatambua wanawake wenzake wenye bidii kama ya kwake, na kushirikiana nao, hilo ndio linakuwa tatizo kubwa.
Paulo alimuonya Eudia na Sintike, kwamba katika bidii yao wawe na Nia moja, waukamilishe wito wao. Hata leo hii Kristo anawataka wanawake wote kanisani wawe na Nia moja. Kwani Ibilisi anajua nguvu iliyopo ndani ya wanawake pale wanaposhirikiana kwa pamoja ajili ya kazi ya Mungu, anajua lile ni jeshi kubwa ambalo kwa muda mfupi sana, linaweza kuvuruga mipango yake kama likimaanisha kuwa pamoja. (Zaburi 68:11 )
Anajua wanawake wanayobidii katika kuomba, analijua hilo, anajua wanawake ni wepesi katika imani, na ndio maana wapo kwa wingi kanisani, hivyo hataki jeshi la namna hii liwe na Nia moja, hataki washirikiane kwenye kazi, anataka kila mmoja atumike kivyake vyake ili nguvu iwe ndogo. Na anachofanya ni kupanda mbegu za kuchukiana, kusengenyana, wivu,kusemana, kijicho n.k. ili tu wachukiane.
Hivyo kama wewe ni mwanamke au Binti wa ki-Kristo, kataa hiyo roho kuanzia leo. Kataa hizo hila za shetani juu yako, jishushe kwa wenzako, na mwenzako naye ajishushe kwako, shirikianane, ili mpate kupokea thawabu timilifu. Bidii yako ina thamani machoni pa Mungu, lakini umepungukiwa ushirikiano na wenzako,
Embu angalia wale wanawake walioizunguka huduma ya Yesu walivyokuwa. Walikuwepo waliokuwa ni matajiri sana, wenye vyeo vikubwa katika jamii kwamfano Yoana, mke wa Kuza, wakili wa Herode, lakini alikuwa tayari kushirikiana na Mariamu Magdalene aliyetolewa pepo saba. Angalia tena Mariamu ambaye alimzaa Yesu, hakujiona yeye ni zaidi ya wengine kisa kapewa neema ya kumzaa mwokozi wa ulimwengu, lakini alishirikiana na wenzake kwa nia moja. Na sio hao tu, biblia inasema na WENGINE WENGI, walikuwa ni nguzo muhimu sana kwenye huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, 2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, 3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na WENGINE WENGI, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao”.
Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye,
2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,
3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na WENGINE WENGI, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao”.
Hata sasa wanawake wanaoshirikiana, wenye nia moja, watabakia kuwa muhimili mkubwa sana katika kanisa. Lakini shetani atalipiga vita, Hivyo ikiwa wewe ni Euodia, leo hii badilika, ikiwa wewe ni Sintike vilevile badilika, zitambue hila za shetani, kwa kuanza unyenyekevu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MWANAMKE ULIYEKOMAA KI-UMRI, ITAMBUE HUDUMA YAKO.
TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.
JE NI KWELI BWANA YESU SIKU YA KURUDI ATAFIKIA ISRAEL
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA
Rudi nyumbani
Print this post