Ufunuo 12 inaelezea vita vya wakati upi?

by Admin | 17 March 2021 08:46 am03

Swali: Yale maelezo ya Ufunuo 12:7-12, yanaeleza vita vya wakati upi?, ile ya kwanza kabisa kabla ya sisi kuumbwa au kuna nyingine iliyotokea tena?


Zipo vita mbili kuu zinazowahusu shetani na Malaika watakatifu.

Vita ya kwanza: Ni ile iliyopiganwa mbinguni, zamani sana kabla ya wanadamu kuumbwa,  pale ambapo ibilisi (yaani shetani), alipoasi kwa kutamani kuwa kama Mungu, na hivyo akashindwa vita ile na kutupwa chini, na baada ya kushindwa vita hiyo akawa hana uwezo tena wala mamlaka ya kurudi katika nafasi yake mbinguni. (akaondolewa mbinguni). Lakini hiyo haikumfanya asifike kwenye enzi ya haki ya Mungu iliyopo mbinguni.

Hata katika maisha ya kawaida, mtu anapoasi katika ngazi Fulani kuu ya serikalini mfano Uwaziri, na hata kufikia kufukuzwa, na kuipoteza ile nafasi, hiyo haimfanyi asiwasilishe mashtaka yake mahakamani. Maana yake kama ana haki zake za msingi, anazozidai kule alipoondolewa, au anajambo la kupashitaki kule alipotoka, mahakama ya haki lazima imsikilize na kumpa haki yake kama anastahili. Kwasababu Mahakama ni moja ya muhimili wa serikali ambayo, haina upandeo fulani wa kuegemea wala kupendelea, ina uwezo hata wa kuishtaki serikali nzima ilimradi tu impatie mtu  mmoja haki yake, na mtu yeyote anauwezo wa kwenda mahamani kushitaki.

Na pia enzi ya Mungu (yaani mbinguni) pamegawanyika katika sehemu kuu mbili, ipo sehemu ambapo Malaika wapo, ambapo ndio kule shetani alipokuwepo kabla ya kuasi, na pia kuna mahali pa kiti cha Hukumu ya Mungu.

Sasa shetani aliondolewa katika nafasi yake huko mahali malaika walipo, huko hawezi kufika tena wala kurudi, lakini mahali pa hukumu ya Mungu, mbinguni bado ana uwezo wa kufika, na kupeleka hoja zake, na mashtaka yake. Na Mungu siku zote ni wa haki, huwa hana upendeleo, anayestahili kumpatia haki yake anampatia na asiyestahili  hampatii.

Sasa  vita ya kwanza ilimwondoa shetani katika nafasi yake ya ukuu kule mbinguni, lakini haikuishia hapo, ipo vita nyingine ya pili ambayo ilianza kuendelea tangu alipoondolewa mbinguni mpaka sasa, na hiyo si nyingine zaidi ya vita katika enzi ya hukumu ya Mungu, huko shetani anafika kila siku, kupeleka hoja zake na mashtaka yake dhidi yetu. Na siku zote inajulikana vita vya mtu aliyeshindwa huwa ni vikali mno na vinaumiza kichwa, kwasababu kila siku utasikia yupo mahakamani kushitaki hiki au kile, mara kakata rufaa n.k. Kwahiyo hata baada ya shetani kushindwa mbinguni, bado anaendeleza vita katika enzi ya hukumu ya Mungu, iliyopo mbinguni.

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kumpokea Yesu, na kuishi maisha ya ukamilifu na uangalifu, kwasababu adui  yetu shetani yupo kila siku kuchukua habari zetu na kuzifikisha mbele za Mungu, na kutushitaki.

Lakini tunapookoka na kuishi maisha ya uangalifu katika hii dunia, shetani anakosa hoja za kupeleka mbele za Mungu, na badala yake, malaika watakatifu wanapeleka mambo mazuri tunayoyafanya mbele za Mungu, ili tupewe thawabu. Kwasababu kama vile wanavyotumwa na Mungu kutulinda, vile vile wanachukua mambo yetu mazuri tunayoyafanya na kuyapeleka mbele za haki ya Mungu..

Mathayo 18: 10  “Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni”.

Na kamwe malaika watakatifu hawapeleki mashitaka yetu mabaya mbele za Mungu wetu..ni shetani peke yake ndio anafanya hivyo…

2Petro 2: 11 “Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana

Kwahiyo kwasasa  kinachoendelea mbinguni, mahali pa haki ya Mungu, wanasimama malaika watakatifu kututetea na wakati huo huo anapita shetani kila mara kutushitaki.. Hiyo ndio vita inayoendelea sasa katika roho, (mapambano kati ya Mikaeli na malaika zake wakishindana na Yule joka na malaika zake), kuhusu mambo yetu sisi tuliomwamini Yesu, Malaika wanatutetea, shetani anatushitaki..(Kwa urefu juu ya hoja hizo fungua hapa >> Huduma ya Malaika watakatifu)

Na vita hivyo  vitahitimishwa na unyakuo,  wakati watakatifu watakapoondolewa duniani, shetani hatakuwa tena na mtu wa kumshitaki, wala hoja ya kwenda kupeleka mbele za Mungu, kuwashitaki wateule, kwasababu watakuwa wameshashinda na wapo mbinguni wakati huo, na hivyo atatolewa moja kwa moja katika hiyo enzi ya haki ya Mungu, na baada ya kuondolewa na kutupwa chini atakasirika kwasababu hatafika tena kumshtaki mtu yeyote wa Mungu, hivyo atashuka kwa hasira na kuanza kufikiri jambo lingine la kufanya..

Na jambo la kwanza litakalomjia ni kutafuta kufanya vita na vita na Taifa la Israeli, pamoja na wale wakristo vuguvugu walioachwa kwenye unyakuo, ambao watakataa kuipokea chapa yake. Hivyo atashuka chini  na kumwingia Yule mwana wa kuasi (Mpinga-Kristo) na kuonyesha rangi zake zote kwa ulimwengu mzima,  atawatesa watu kwa miaka mitatu na nusu (Miezi 42). Huo ndio ule wakati wa dhiki kuu.

kama tunavyosoma katika Ufunuo 12..

Ufunuo 12:7  “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;

8  nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.

9  Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.

10  NIKASIKIA SAUTI KUU MBINGUNI, IKISEMA, SASA KUMEKUWA WOKOVU, NA NGUVU, NA UFALME WA MUNGU WETU, NA MAMLAKA YA KRISTO WAKE; KWA MAANA AMETUPWA CHINI MSHITAKI WA NDUGU ZETU, YEYE AWASHITAKIYE MBELE ZA MUNGU WETU, MCHANA NA USIKU.

11  Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.

12  Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu”

Hapo katika mstari wa 10, utaona Malaika mmoja anatangaza kwamba…“Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku”..Maana yake Yule anayewashitaki watakatifu hawezi tena kupanda kwenda kuwashitaki…kashashindwa, kwasababu wateule wameshamshinda kwa damu ya mwanakondoo, na wameenda kwenye unyakuo mbinguni..huko hawezi kuwashitaki tena awatoe huko..

Lakini “ole wa nchi na bahari”..maana yake ole wa waliobakia ambao hawakwenda mbinguni. Ibilisi anashuka kwao mwenye ghadhabu nyingi, na pia ole kwa Taifa la Israeli, ambalo ndio “Yule mwanamke mwenye mimba (Ufu.12:1)”.

Hivyo hiyo biblia inatutahadharisha, juu ya mambo yanayokuja. Ndugu sasa hivi  unafahamika kama ni mkristo lakini unazini kwa siri, unaiba, unaua, unacheza kamari, unavaa vibaya, unatukana, n.k..kumbuka shetani anayefikisha hayo kila siku mbele za haki ya Mungu, na kukushitaki. Na lengo lake ni ufe katika hizo dhambi ili uwe wake milele, au kama unyakuo utapita leo wewe ubaki, uingie katika dhiki kuu.

Dhiki kuu sio sehemu ya kutamani kuwepo, kama umeshindwa leo  kumkiri Yesu wakati neema ya Mungu bado  ipo, hutaweza siku ile katika dhiki kuu. Kama umeshindwa kuvumilia njaa ya siku moja katika kufunga ili uutafute uso wa Mungu hutaweza kuvumilia njaa ya miaka mitatu na nusu ya dhiki kuu. Kama leo hii kipindi cha amani unashindwa kujikana nafsi na kuchukua msalaba wako umfuate Yesu, kamwe hutaweza kufanya hivyo wakati wa dhiki kuu.

Hapo Yule malaika anasema… “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; AMBAO HAWAKUPENDA MAISHA YAO HATA KUFA”.

Je leo hii unayapenda maisha yako kiasi kwamba, wokovu kwako ni jambo lililopitwa na wakati?, fashion za dunia,umaarufu, kusifiwa, kutukuzwa, kupendwa na kila mtu ndio mambo ya heshima kwako?…Hapo biblia inasema “ambao hawakupenda maisha yao hata kufa!!!”, ndio waliomshinda shetani!!.

Bwana Yesu pia alisema.. Yohana 12:25  “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele”.

Kama bado hujampokea Kristo maishani, ni vizuri ukampokea leo, kwa kumwamini kwamba alikuja duniani akafa kwaajili ya dhambi zako, na akafufuka na kupaa mbinguni, na pia atarudi tena. Na kwa kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kutozifanya tena, Na pia kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38, 8:16), naye atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu, atakayekuongoza na kukutia katika kweli yote ya kuyaelewa maandiko.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

HUDUMU YA MALAIKA WATAKATIFU.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/17/swali-ufunuo-12-inaelezea-vita-vya-wakati-upi/