NIFANYALO WEWE HUJUI SASA; LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE.

by Admin | 25 March 2021 08:46 pm03

Wakati ule ambao Bwana Yesu anawatawadha wanafunzi wake miguu, Petro alimuuliza Bwana swali la mshangao sana, lililoashiria kugoma kutawadhwa miguu na Bwana, kwasababu alitazamia kuwa wao ndio wangepaswa wamtawaze yeye miguu, na sio yeye awatawadhe wao, Lakini Bwana alimwambia maneno haya;

Yohana 13:7 “Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye”.

Nachotaka uone hapo  kuhusu  Bwana Yesu ni kuwa, si kila jambo analolifanya katika maisha yako sasa, au unaloliona akilitenda nje kwa wengine, ambalo hulielewi utalipatia majibu yake leo leo. Mengine amekusudia uyafahamu baadaye.

Yapo maisha Mungu anaweza kukupitisha wewe kama mkristo uliyeokoka  yakawa ni nje kabisa na matarajio yako, na ukijiangalia, huna kasoro yoyote na Mungu, lakini bado unajiuliza, kwanini mimi, mbona wenye dhambi hayawakuti kama yaliyonikutuma mimi..Kwanini matatizo haya yamenipata wakati huu, kwanini ugonjwa huu umenikuta mimi kama mtumishi wa Bwana, kwanini Mungu anaruhusu nichukiwe na ndugu zangu kwasababu ya ukristo wangu, kwanini Mungu mpaka sasa hanipi kazi, japokuwa nimekuwa nikimtumikia muda wote huu..

Maswali kama hayo alijiuliza Ayubu wakati ule alipokumbana na matatizo yasiyoeleweka chanzo chake ni nini.

Nataka nikuambie ukishajiona upo katika mazingira kama hayo, na ndani yako unashuhudiwa kabisa wewe ni mtoto wa Mungu, ni heri tu utulie, kwasababu si kila jambo utapata majibu yake leo leo, pengine ni ushuhuda Mungu anautengeneza ndani yako, ili uje kuwa msaada mkubwa sana kwa watu wengine baadaye, watakaopitia hali kama za kwako ili waimarike.

Au hata kama ikiwa ni kwa ajili yako, basi ujue lipo jambo bora Zaidi litakuja mbele yako, Hivyo usikata tamaa ya kuendelea kumtumikia  Mungu,. Yeye mwenyewe alisema..

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.

Unaona kumbe lipo tumaini kwenye siku za mwisho, siku ambazo huwezi tena kufanya mabadiliko yoyote, siku ambazo huwezi tena kurekebisha chochote hapo ndipo tumaini linatokea.. Siku hizo zikifika utasema, ni heri wakati ule Mungu hakunipa kile, au ni heri wakati ule Mungu alinipitisha pale nione, au ni heri wakati ule Mungu hakunijibu maombi yale, leo hii ningeshakuwa nimepotea, au nimekufa, au nimepoteza kila kitu, au ningefanana na wale waliopata hasara ya nafsi zao.

Tunapaswa tusiwe watu wa kutafuta tafuta sababu za kila ugumu unaokuja mbele yetu mwisho wa siku tutakuwa ni watu wa kulaumu laumu, au kunung’unika nung’unika, si kila jambo utalipatia jawabu lake papo kwa papo, hivyo wewe ishi maisha yanayompendeza Mungu sikuzote, haijalishi mambo yatakuonyookea, au hayatakunyookea sasa.. Songa mbele na Bwana, kwasababu anajua mawazo anayokuwazia, kamwe hawezi kukuacha, utafahamu sababu za yeye kufanya hivyo mbeleni, lakini sasa mtazame Kristo.

Siku hizo ndio zile utasema ni heri nilichagua kumtafuta Mungu, faida yake leo hii nimeiona.

Vivyo hivyo yapo mambo mengi sana kama kanisa la Kristo, Bwana ametuficha leo, kuna maswali ambayo kwa namna ya kawaida hatuwezi kuwa na majibu yake sasa, lakini tutakuja kufahamu baadaye, aidha tukiwa hapa hapa duniani au tukishavuka ng’ambo.

1Wakorintho 13:12 “Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana”.

Kwahiyo, tuzidi kumtazama Bwana Yesu, tumpende, na tumwamini, kamwe hawezi kutuacha. Sifa, heshima na utufuku vina yeye milele na milele.

Amen.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ILI NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE.

Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/25/nifanyalo-wewe-hujui-sasa-lakini-utalifahamu-baadaye/