PONGEZI NA MAONYO YA BWANA KWA WATAKATIFU.

by Admin | 24 July 2021 08:46 pm07

Kama wewe ni mtoto wa Mungu kweli kweli na sio mwana-haramu, ni vema ukafahamu tabia za Mungu kwako zinavyokuwa hususani katika eneo la pongezi na maonyo, ili usije ukaishi maisha ya wasiwasi au maisha ya kujivuna sana.

Unapaswa ufahamu kuwa Mungu akikuonya haimaanishi kuwa wakati wote unamchukiza, na vilevile Mungu akikusifia haimaanishi kuwa wakati wote unampendeza.

Kwamfano embu tafakari ile habari tunayoisoma katika Mathayo 16 ambayo Bwana Yesu aliwauliza mitume wake, kwa habari yake, kuwa wao wanasema yeye ni nani? Utaona Petro alipotoa jibu fasaha wakati ule ule Bwana alimsifia kweli kweli, kwa jinsi alivyoupokea ufunuo mkubwa namna ile,mpaka akaambiwa kuwa juu ya ufunuo ule Kristo atalijenga kanisa lake na milango ya kuzimu haitalishinda,.Na pia atampa funguo za ufalme wa mbinguni..na lo lote atakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote atakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni..(Mathayo 16:13-20)

Ukiambiwa maneno kama haya, unaweza kujiona wewe ni spesheli sana, hakuna mtume mwingine zaidi yako wewe, wewe ni bora, wewe ni mwamba, Mungu amependezwa na wewe kuliko wengine wote, na ndio maana amekufunulia maono makubwa kama hiyo. Si ni kweli?

Lakini wakati Petro anafikiria vile, dakika chache mbeleni, wakati Bwana Yesu anawaeleza juu ya kifo chake, jinsi kitakavyokuwa, Petro huyo huyo akajitokeza tena na kuanza kumkemea Bwana na kumwambia kuwa hayatampata mabaya hayo mabaya yote. Akidhania kuwa na ufunuo wa namna hiyo amefunuliwa tena na Mungu mbinguni. Lakini majibu ya Bwana Yesu, yalikuwa ni ya tofauti kabisa, tusome..

Mathayo 16:21 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.

22 Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23 Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Tafakari, muda mfupi nyuma ameambiwa ufunuo ule wa kumjua Yesu ni nani alipewa na Mungu mwenyewe..Na muda huu tena Yesu haumwona kama ni Petro anayezungumza, ni heri ingekuwa hivyo, lakini anamwona Shetani kabisa, akizungumza kwenye kinywa cha Petro akinena.

Unaweza kujiuliza, Je!, Bwana hakuona, ni kitu gani Petro atakisema  mbele kidogo? Alijua vizuri lakini hilo halibatilishi kusifiwa kwa lile zuri alilolifikiri.

Ikiwa leo hii Mungu atakuambia habari zako njema, akakusifia, au akakupongeza, au akakuthaminisha, usidhani kuwa kwa kila kitu unachokifanya kwake ni sawa,..hapana usijipumbaze kwa namna hiyo bali zaidi jitahidi kumpendeza na kusimama katika njia zake..Vilevile Mungu akikuonya leo, kwa njia zako, haimaanishi kuwa anachukizwa na wewe kwa kila kitu unachokifanya, hapana, usifikirie hivyo utavunjika moyo hata kwa vile vizuri unavyovifanya, bali rekebisha hapo unapoonyewa, kwasababu, ndicho kikwazo anachokiona ndani yako kwa muda huo. Kwasababu vipo pia vizuri unavyomfanyia na anapendezwa na wewe.

Na wakati mwingine vyote viwili vinaweza kwenda sambamba, maonyo na pongezi.  Hivyo bado usichanganyikiwe, na kudhani kuwa moja ni la Mungu na lingine ni la shetani, hapana, bali vyote vinaweza vikawa ni vya Mungu. Vichukue vitendee kazi, kwasababu anayo mawazo mazuri na wewe.Ndicho alichokuwa anakifanya hata kwa yale makanisa 7 tunayoyasoma katika Ufunuo sura ya 2 & 3

Nikutakie maisha ya heri na ya Baraka tele katika safari yako ya kuelekea mbinguni.

SHALOM.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

MILANGO YA KUZIMU.

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/24/pongezi-na-maonyo-ya-bwana-kwa-watakatifu/