by Admin | 6 September 2021 08:46 pm09
Jina kuu la Bwana na Mwokozi wetu na wa ulimwengu, Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia yetu. (Zab 119:105).
Je unafanya kazi yoyote ya mikono?, ya kujiajiri au kuajiriwa?.. labda una shamba, au mifugo, au biashara, ambayo katika hiyo unategemea kukuingizia kipato?…
Je unayo shughuli ambayo ghafla umeshangaa mambo yameharibika!, yameenda kombo!..wakati mwingine unaweza kujiuliza ni nini chanzo, na ukashinda kujua..Leo nataka uone sababu ya mambo hayo kupitia maandiko?
Kama upo ndani ya Kristo, umesimama vizuri na ni mwaminifu kwa Bwana na mambo yamekuharibikia ghafla!, tambua kuwa chanzo ni kama kile kile cha Ayubu na wala si kingine..
Kwamba Shetani amekwenda kukushitaki mbele za Bwana, kwasababu ya haki yako, na hivyo Bwana akamruhusu aiharibu kazi yako,.. Na majaribu hayo mwisho wake ni mzuri, kwasababu ukiisha kuyashinda basi Bwana atakunyanyua mara dufu.. Ni majaribu ya kuwavusha watu wa Mungu kutoka hatua moja hadi nyingine.
Lakini kama upo nje ya Kristo (Yaani hujampokea Yesu na kumwamini, na kubatizwa, na kuishi maisha ya utakatifu yanayompendeza yeye), na ghafla umeona mambo yako yameharibika, kwa uharibifu usio wa kawaida..nataka nikuambie kuwa jambo ni lile lile lililomtokea Ayubu limekutokea na wewe, isipokuwa katika pande tofauti.
Ni kwamba shetani, au mapepo yake yamekwenda mbele za Mungu na kukushitaki na hivyo kupewa ruhusa ya kuja kuharibu kazi yako, au biashara yako au mifugo yako..na mwisho wa uharibifu huo ni mbaya kwasababu hauna tumaini la kuvipata tena vile ulivyopoteza.
Sasa hebu tusome habari moja katika biblia ambayo hiyo itatusaidia kuelewa vizuri.. tumsome mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa na biashara yake kubwa ya mifugo lakini iliharibika ghafla na wala hakupata kurejeshewa..
Marko 5:6 “Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;
7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.
8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.
10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11 NA HAPO MILIMANI PALIKUWA NA KUNDI KUBWA LA NGURUWE, WAKILISHA.
12 PEPO WOTE WAKAMSIHI, WAKISEMA, TUPELEKE KATIKA NGURUWE, TUPATE KUWAINGIA WAO.
13 AKAWAPA RUHUSA. WALE PEPO WACHAFU WAKATOKA, WAKAINGIA KATIKA WALE NGURUWE; NALO KUNDI LOTE LIKATELEMKA KWA KASI GENGENI, WAKAINGIA BAHARINI, WAPATA ELFU MBILI; WAKAFA BAHARINI.
14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea”.
Umeona hapo?.. huyu mtu pengine alikuwa tajiri sana mwenye nguruwe wengi (biblia inasema walikuwa nguruwe elfu 2), na akaajiri wachungaji wakawachunge kondoo wale milimani.. Na siku hiyo ghafla anakuja kuletewa taarifa kuwa nguruwe wake wote elfu mbili wamekimbilia baharini na wamekufa huko.
Bila shaka kwa haraka haraka angeweza kusema ni uchawi, au ana gundu!.. Lakini kumbe kuna jambo lililokuwa linaendelea katika roho juu yake na mali zake bila yeye kujua. Kwamba mapepo yalikwenda kwanza mbele za Bwana Yesu kuomba ruhusa yaingie kwenye kitega uchumi chake, ili yaiharibu kazi yake! Na Bwana Yesu akayapa ruhusa na wala hakuyakataza..
Kama vile tu!, shetani alivyokwenda mbele za Bwana kuomba ruhusa aharibu mifugo ya Ayubu, na Mungu akampa ruhusa wala hakumkataza.(Ayubu 1:9-12). Ndicho kilichomtokea huyu mtu mwenye nguruwe Elfu 2.
Lakini cha ajabu ni kwamba hatusomi tena habari za huyo tajiri aliyepoteza nguruwe wake, (hao elfu mbili kwa siku moja) kwamba alikuja kuwapata tena.. maana yake ni kwamba hakuja kuwapata tena.. kama ilivyokuwa kwa Ayubu.. Ayubu yeye alipopoteza mifugo yake maandiko yanasema alikuja kupata mara dufu.. Lakini huyu tajiri wa nguruwe hakuna chochote alichoambulia..zaidi ya kupata hasara tu!
Na kinachoshangaza zaidi ni kwamba hata Bwana hakumhurumia wala hakusikitika, yeye kupoteza nguruwe wote wali, Zaidi ya yote aliruhusu mapepo yaingie nguruwe wake.
Sasa ni kwasababu gani hatusomi ushuhuda wowote wa huyu tajiri kuja kupata tena alichokipoteza kama Ayubu?.. Jibu ni rahisi, ni kwasababu hakuwa ndani ya wokovu kama aliokuwa nao Ayubu.. hakutubu!, wala hakumwamini Yesu kabla wala baada ya hapo.. Zaidi ya yote maandiko yanasema wakuu wa miji pengine na yeye akiwemo miongoni mwao, walimfukuza Bwana Yesu atoke katika mipaka yao.
Ndugu unayesoma ujumbe huu, jitafakari je!, hiyo kazi unayoifanya ina usalama kiasi gani?..je upo ndani ya Kristo au nje!.. Unaweza kufikiri mali zako zitakusaidia, au mifugo yako..lakini nataka nikuambie mapepo kila siku yanazitaja hizo mali zako mbele za Mungu.. Na cha kuogopesha ni kwamba Mungu anaweza kuyaruhusu yazichukue au waziue ndani ya siku moja..
Kwasababu kama aliruhusu kwa mtumishi wake Ayubu, ambaye alikuwa mkamilifu mbele zake, wewe na mimi ambaye pengine si wakamilifu mbele zake ni wakina nani, Mungu asiruhusu mabaya hayo?
Jiulize je!, siku ya uharibifu itakapokuja ghafla kama ilivyokuja kwa huyu Tajiri wa nguruwe na Ayubu, utakuwa wapi?.. utakuwa na tumaini kama Ayubu au utapotea moja kwa moja kama huyu Tajiri.
Kama bado hujampokea Yesu, ni vyema ukampokea sasahivi, kwa usalama wa Roho yako na watoto wako, na mali zako na mifugo yako. Kwani usipofanya hivyo kuna hatari ya kukosa tumaini katika siku za kujaribiwa.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kwanini Bwana aliwalenga mbwa na nguruwe tu katika Mathayo 7:6?
Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/09/06/je-una-matumaini-ya-kupata-tena-kile-ulichopoteza/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.