Waefeso 6:16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu
Waefeso sura ya 6, inaeleza mapambano ambayo yapo rohoni kati ya sisi na ufalme wa giza, na namna ambavyo tunapaswa tusimame kushinda vita hivyo, kwa kuvaa zile silaha zote za haki zinazotajwa pale. Kama vile chapeo ya wokovu, dirii ya haki, kweli kiunoni, upanga wa Roho, na ngao ya Imani,.
Lakini pia katika vifungu hivyo tunaelezwa mojawapo ya silaha ya adui, nayo ni “mishale ya moto”. Swali Je hii mishale ya moto ni ipi?
Mishale ni silaha zilizotumika zamani, za kumshambulia adui kwa mbali, na hivyo ili kuziboresha waliweka moto kwa mbele ili zitakapomfikia adui basi zilete madhara zaidi ya yale tu ya kutoboa, bali kuunguza kama sio kumuharibu kabisa adui.
Tofauti na silaha kama rungu, au upanga ambavyo vinahitaji uso kwa uso kutumika. Kwa mbali havina matokeo.
Tukirudi katika ulimwengu wa sasa michale ya vita ni makombora, Kwanini hapo shetani anaonekana akirusha mishale kutokea mbali? Ni kwasababu kwa karibu hamwezi mwamini, kwani nguvu zilizo ndani yake ni nyingi kuliko alizonazo.
Shetani hutumia sana ulimi kuleta, aidha udanganyifu, mafarakao, vita n.k. Ndio maana maandiko yanasema;
Yakobo 3:5 Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.
6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.
7 Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.
8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.
10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.
Hawa alidanganywa na Nyoka kwa ulimi, Mafundisho ya uongo, huanzia katika maneno. Hivyo sisi kama watoto wa Mungu ni lazima tuijue silaha hii na kuidhibiti kwanza sisi wenyewe ndani yetu, kuhakikisha hatutumika kama warusha mishale, kwa kusema yasiyopasa, lakini pia kusimama kwa imani kuhakikisha, tunakuwa thabiti kiimani, kwa kupuuzia, au kutokuweka moyoni kila Neno linalosemwa kinyume chetu, sambamba na kuwa makini kwa kupima kila neno tunaloambiwa kama kweli ni la Mungu au la!.
Mkristo usipojua silaha hii ya adui, utajikuta kila kukicha unaishi kwa machungu ya maneno ya watu, huna raha, una mashindano, au utajikuta unaanguka katika mikono ya manabii wa uongo, na hatimaye shetani anakuwa amekupata.
1Petro 4:12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia
Majaribu yote hutoka kwa Yule mwovu, lengo lake ni kumwangusha mwamini ili amwasi Mungu, hata wakati ule Bwana Yesu anakaribia kusulubiwa, alimwombea Petro ili imani yake isitindike, kwasababu alijua wataingia kwenye majaribu makubwa, kwa upungufu wa maombi yao. Vivyo na sisi yatupaswa tuwe waombaji ili tuizime mishale ya majaribu mbalimbali ya adui tusiyojua pembe ipi yanatokea. Na pia tunapojikuta ndani ya hayo majaribu, yatupaswa kuishikilia imani yetu hasaa, kwa kuamini kuwa Bwana yupo pamoja nasi kutengeneza njia ya kutokea.
Shetani akijua kuwa hana nguvu ya kumshinda mwamini moja kwa moja, hivyo hupenda kuinua ujasiri wake kama silaha, na akiwa mbali anajua akirusha mishale yake kisha Yule mtu akiiogopa basi anamwangusha. Ndio hapo huleta vitisho, mfano wa kipindi kile cha wana wa Israeli walipopewa agizo la kwenda kumjengea Mungu nyumba Yerusalemu, tunasoma baada ya kipindi kifupi maadui zao wakainuka, na kuwasemelea kwa mfalme, hatimaye marufuku ikatoka, wasiendeleze ujenzi, hivyo mahali pa Mungu pakabaki gofu tu la msingi kwa muda mrefu, kisa hofu ya utalawa mpya. Lakini baada ya muda mwingi sana, tunaona Mungu akawaamsha mioyo Hagai pamoja na Zekaria, na kuwaambia Israeli kwanini wameacha kuijenga nyumba ya Bwana. (Hagai 1:1-9), walipogundua makosa yao, kwa kuruhusu hofu, Ndipo walipoamka kwa ujasiri tena na kuijenga, Mungu akawafanikisha sana.
Vivyo hivyo na sisi, tumepewa agizo la kuhubiri injili, ikiwa itapingwa, au tutatishiwa kuuawa au kufungwa, ikiwa tutapitishwa kwenye miiba au miamba hatupaswi kuogopa mishale hiyo, bali tusimame kwa imani kama akina Shedraki na Danieli, wakiwa katika matanuru ya moto, na matundu ya simba hawakutetereka. Bali walimtumaini Mungu anayewaokoa, na hatimaye kweli ikawa vile.
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba ipo kweli mishale mingi ya moto, ya adui lakini hiyo mitatu ndio mikuu. Na tukiweza kusimama kwa imani basi shetani pande zote anakuwa ameshindwa kabisa kabisa, (Akiwa karibu na vilevile akiwa mbali) linda kinywa chako /puuzia/ pima maneno unayoyasikia, vilevile kuwa mwombaji ili usiingie majaribuni/ uyashinde majaribu, Lakini zaidi sana kamwe usiogope vitisho vya adui, kwasababu hawezi kufanya lolote kwa ihari yake mwenyewe.
Mungu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Silaha za Mkono wa kuume na za mkono wa kushoto ni zipi
Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?
About the author