Ubora wa Kuhubiri au kufundisha haupimwi kwa elimu kubwa ya biblia, au mifano mizuri, au utashi fulani wa kupangilia maneno. Hapana, bali ni uwezo wa kupenya katika mioyo ya watu.
Haimaanishi kuwa na elimu ya biblia haichangii ubora wa fundisho au hubiri..inachangia sana lakini hiyo ni kama gamba la juu sana..ambalo linaweza lisitoe pia matokeo yoyote.
Pale fundisho linapoweza kuingia ndani ya moyo wa mtu, kupambanua, kuchoma, kulainisha, kupindua-pindua, kukarabati, kuponya hadi kumfanya mtu kuwa na mwitikio wa dhahiri wa nje. Hilo ndio linaitwa fundisho au hubiri kibiblia.
Sasa tendo hilo mpaka kufikiwa, si jambo rahisi hata kidogo, hakuna utashi wa kibinadamu unaweza kufanya hivyo.
Kwasababu hakuna anayejua ndani ya mtu mwingine kuna nini?
Lakini lililo gumu zaidi ni kuwa hata yeye mwenyewe hajijui vema, kama anahitaji matengenezo katika eneo fulani la moyo wake. Anaweza akawa ana hofu akadhani huwenda chanzo cha hofu hiyo ni ule ugonjwa uliomshika, kumbe chanzo ni kingine kabisa.
Kwasababu mwanadamu mwenyewe moyo wake ni fumbo kubwa.
Yeremia 17:9
[9]Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
Umeona jinsi ilivyo ngumu sana. Ikiwa yeye mwenyewe hajijui, wewe mtu wa tatu utayajulia wapi yaliyomo moyoni mwake? Lakini Mungu anataka uyahubiri yahusuyo moyo wake.
Usifikiri unapomwona mtu, labda ana huzuni, au furaha au ana tabia za ulevi, wizi, , ukadhani anahitaji fundisho linaloendana na hiyo tabia unayoiona kwa nje.
Unaweza ukakosa shabaha kwa maili nyingi sana, ukifikiri tu hivyo.
Utamwona analia, pengine ni mgonjwa, amefiwa, amepoteza kila kitu kama ilivyokuwa kwa Ayubu na wewe unamfuata na fundisho la faraja, ukadhani kuwa ndio uponyaji wake utakapotokea.
Kumbe Mungu anajua anataka makemeo, na makaripio ili aponywe.
Wakati mwingine utasimama kwenye mkusanyiko wa watu wengi labda mia. Huko huko wapo wanaohitaji faraja, wanaohitaji unabii, wanaohitaji maonyo, wanaohitaji maarifa, wanaohitaji kufunguliwa. Sasa wewe unasimama na fundisho lako lenye mlengo mmoja wa makemeo, unadhani wote watahudumiwa na hilo. Kama ukikosa namna ya ki-ungu, unaweza ukawa unazungumza maneno yako.
Na lengo la Mungu ni watu wote wahudumiwe na Neno.
Hapo ndio linakuja suala la hakuna mbobezi wa fundisho au hubiri. Inahitaji hekima nyingine itokayo juu, ya kuhubiri usichokuwa na ufahamu nacho, au ujuzi nacho.
Siku ile ya Pentekoste, kilichotendeka mpaka ikapelekea watu wale kuchomwa mioyo, na hatimaye kuamini kwa idadi ile kubwa ya watu.
Haikuwa kwasababu walipaza sauti sana, au walihubiri kwa ujasiri sana, au maneno yao yalikuwa na elimu kubwa ya theolojia..
Hapana angalia utaona yalikuwa ni maneno ya kawaida kabisa… lakini yaliyoundwa na Roho Mtakatifu kwa namna ambayo yalipenya katika moyo wa kila mmoja.
Utaona, hatua ya kwanza walinena kwa lugha ambazo hata wao wenyewe hawakuzijua, lugha hizo zilikuwa zinawahubiria wengine.. zinanena mambo yao ya sirini, zinawakemea, zinawafariji, zinawaponya, zinawashuhudia Kristo.
Mpaka baadaye wanamaliza kunena tayari injili imeshahubiriwa wasijue ni kitu gani kimehubiriwa.
Petro aliposimama kumalizia maneno yake, wote wamenywea wanasubiri tu kupewa maelekezo ni nini cha kufanya baada ya pale..
Matendo ya Mitume 2:37
[37]Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
Hao ni watu wasio na elimu yoyote, walikuwapo waandishi, na mafarisayo wenye elimu lakini hakuna matokeo yoyote ya mafundisho yao.
Hata leo hii mimi na wewe.. Tujue kuwa kuhubiri na kufundisha hakutegemei sana ujuzi, au utashi, bali kunategemea zaidi Roho Mtakatifu.
Kwanini Roho Mtakatifu?
Kwasababu yeye ndiye anayeweza kuzama ndani ya mioyo ya watu na kujua shida zao, na kuwaponya.
Ni nini tunapaswa kufanya, ili fundisho likazame moyoni, lisitoke kwa makisio yetu?
Jambo kuu ni Kuwa na maandalizi ya kutosha.
Maandalizi hayo yapo kwa namna mbili.
1) Kumwandalia Roho Mtakatifu njia ya kuanzia..Ndio hapo unahitaji kwanza kusoma na kuandaa somo / fundisho. Kumbuka Ni lazama utenge muda kuandaa fundisho ambalo utalihubiri. Andika, na ujue pa kuanzia, bila kuwa na maandalizi hayo, unasema nitaenda tu kuzungumza. Ujue tayari umeizuia njia ya Roho Mtakatifu kufundisha.
2) Lakini hilo peke yake halitoshi, hatua nyingine ni kuomba maingilio ya Roho Mtakatifu yawe makubwa. Hapo ndipo unatenga muda mrefu wa kuomba, ili Roho Mtakatifu akatembee kwenye vyumba vya ndani kabisa ambavyo wewe hujui, wakati utakaposimama na kufundisha, kushuhudia.
Sasa ukimaliza hapo. Jiandae kwenda kusema ulichokusudia.. kumbuka mhubiri anayetumia dakika kumi kufundisha lakini amekuwa na maandalizi ya masaa matano kwenye kusoma na maombi. Ana nguvu zaidi ya yule atakayefundisha masaa matano, halafu alijiandaa kwa dakika tano.
Mwisho Ukienda kufundisha na kuona mazungumzo yako yanasogea nje ya mada, au taarifa nyingine zinakuja kichwani mwako tofauti na zile ulizoziandika kwenye daftari ujue ni kazi za Roho Mtakatifu usizizuie.
Baadaye utakuja kusikia tu shuhuda, na hata kama hazitasemwa, ujue Neno lako halijakwenda bure.
Tukiwa wahubiri na waalimu wa namna hii. Roho nyingi za watu zitaokolewa.
Kuhubiri ni kusema tusichokijua, cha wengine.
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Save my name, email, and website in this browser for the next time I comment.
Δ