WATU WALIOINGIA  KAANANI, LAKINI SI NCHI YA AHADI.

WATU WALIOINGIA  KAANANI, LAKINI SI NCHI YA AHADI.

Nuru ya UpendobibliayetuEdit Profile

Wana wa Israeli walitoka kweli Misri, na Mungu akawaahidia kuwa mbele yao wamewekewa nchi njema ibubujikayo maziwa na asali, nchi yenye raha, na ya kustarehe (Kutoka 3:8). Na kweli wakaifikia hiyo nchi, waliyoahidiwa lakini biblia inasema hawakuipata ile raha aliyoikusudia Mungu.

Waebrania 4:8-10

Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.
Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.
10 Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.

Walidhani, wingi wa utajiri walioukuta, na ardhi yenye rutuba, na chakula kingi walichokutana nacho huko ndiyo raha yenyewe, lakini kumbe sio.  Mungu alikuwa amewawekea Raha yake maalumu, ambayo wao walikuwa hawaithamini.

Raha yenyewe ilikuwa ni YESU KRISTO.

Mathayo 11:28

28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

Mathayo 12:8

Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

Tangu wakiwa jangwani, Yesu alianza kujidhihirisha kwao kwa njia ya maumbo, na ishara,  lakini walimkataa, mfano ule mwamba waliounywea alikuwa ni Kristo (1Kor 10: 4:3), yule nyoka wa shaba  aliyeinuliwa (Yohana 3:14-17) alikuwa ni Kristo, ile Mana alikuwa ni Kristo (Yohana 6:48-58), Jinsi ile hema ya kukutania ilivyokuwa imepangiliwa, makabila yote kuzunguka hema, huchora umbo la msalaba, ilikuwa ni msalaba wa Kristo.

Hivyo Kristo alikuwa tayari ni raha yao, Hivyo hata walipokuwa wanaingia katika nchi ya Ahadi wamengemwona kwa maumbile mengi yaliyo bora kuliko yale, akiwaponya kimiujiza, akiwapa raha nafsini mwao, kwa kuwatiririshia  maji ya uzima mioyoni mwao, maziwa na asali yangeyaona halisi kabisa nafsini mwao, starehe wangeifikia, mpaka atakapotokea mwenyewe halisi katika mwili, ili kuubadilisha mfumo wa ulimwengu mzima kuwa milki ya Mungu.

Lakini baada ya kufika kwenye ile nchi walimpinga, sana, hata alipowatuma manabii wake bado hawakuwasikiliza, hatimaye, wakabakia tu Kaanani lakini sio rahani. Jambo hilo liliendelea kwa maelfu ya miaka, mpaka yeye mwenyewe Kristo alipochukua mwili na kuja katikati yetu,

Na tunaona wote waliompokea, waliingizwa kwenye Raha hii halisi, ambayo kwanza inaanza kwa kuwekwa huru mbali na utumwa wa dhambi, Lakini pia kujazwa Roho Mtakatifu, ndani yake ili kuruhusu badiliko kubwa kutokea ili kumfanya mtu aone kumpata Mungu ni raha zaidi ya fahari na mali zote za dunia.

Raha hii inaendelea ndani ya waamini, mpaka leo, na hadi Atakaporudi mara ya pili kuitimiza kwa ukamilifu wote wa macho kwa kutuingiza kwenye ile Mbingu mpya na nchi mpya, aliyotuandalia.

Hivyo kwasasa  tumekabidhiwa jukumu la kuitunza, kwasababu tusipodumu ndani ya Kristo haijalishi tumeingia Kaanani kwa kubarikiwa mwilini, kiasi gani, pengine kiafya, ki-makazi au vinginevyo, haitufaidii kitu, bado tupo matesoni na utumwani. Ni wajibu wetu kuhakikisha nyakati zote tunadumu ndani ya Kristo, ili tukifikishwe kwenye kilele cha raha hiyo atakaporudi.

Waebrania4:1-11

Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.
Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.
Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu:
Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote;
na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao,
aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.
Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.
Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.
10 Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.
11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.

Hama Kaanani, zama rahani mwa Kristo.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

 

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply