JIWEKE TAYARI KUYAFANYA MAPENZI YA MUNGU.

JIWEKE TAYARI KUYAFANYA MAPENZI YA MUNGU.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, ASIJIWEKE TAYARI, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi”.

Hebu tulichambue kidogo neno hili kwa undani, neno baada ya Neno na kuna jambo tutajifunza..

maandiko yanasema “Mtumwa aliyejua mapenzi ya bwana wake”.. Kumbe! Kuna watumwa wanaoyajua mapenzi ya Bwana zao na kuna ambao hawayajui mapenzi ya Bwana zao…

Sasa mapenzi hayo ni yapi?.. Bila shaka si mengine zaidi ya yale tunayoyasoma katika kitabu cha

1Wathesalonike 4:2 “Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.

3 Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, KUTAKASWA KWENU, MWEPUKANE NA UASHERATI;

4 KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE KATIKA UTAKATIFU NA HESHIMA;

5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu”.

Mapenzi ya MUNGU kulingana na maandiko hayo ni TUTAKASWE, Kwa kuepukana na uasherati na tamaa mbaya.

Sasa kama hayo ndio mapenzi ya MUNGU, (yaani UTAKASO)..hebu tuendee na maandiko yale ya Luka 12:47 tuone nini Roho Mtakatifu anataka kutufundisha.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, ASIJIWEKE TAYARI, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana”..

Umeona tena hapa! Kumbe kuyajua mapenzi ya MUNGU na KUTOJIWEKA TAYARI KUYAFANYA ni KOSA KUBWA!

Wengi tunadhani kosa ni “kutoyafanya tu”!…Lakini Biblia inatufundisha kuwa kosa linaanza kwa “kutojiweka tayari”.. Sasa nini maana ya kutojiweka tayari.

Tuanze na “kujiweka tayari” maana yake nini?.. kujiweka tayari ni kitendo cha kuwa tayari kiakili, kifahamu, kimkakati, na kiutendaji…. Mara nyingi “kujiweka tayari” kunatangulia kabla ya kitendo chenyewe, na kinyume chake kutojiweka tayari ni ile hali ya “kukataa, kudharau, kupuuzia, kuchukulia jambo juu juu, kusema huu sio wakati, kwa ufupi kutojishughulisha zaidi na kuyajua mapenzi ya MUNGU”.

Sasa Roho Mtakatifu anajua katika hali za kwanza kabisa za kuokoka si rahisi mwamini, awe mkamilifu katika kuyafanya mapenzi yake, Lakini anachokiangalia na kukithamini sana katika hatua za awali ni angalau mtu “kujiweka tayari”.

Maana yake mtu awe tayari kusikiliza maneno ya MUNGU na kuongozwa na Roho Mtakatifu, ili Roho Mtakatifu achukue nafasi ya kumtengeneza zaidi,  pia awe ajiweke tayari kufanywa mpya na Roho Mtakatifu kwa kuendelea kumtii Roho Mtakatifu.

Lakini jambo la kuhuzunisha utakuta mtu analisikia Neno ambayo moyoni anajua kabisa ni kweli ya MUNGU, lakini hana utayari wowote moyoni wa kulitii… Utakuta mtu ndani Roho Mtakatifu anamfunulia kabisa njia sahihi ya kwenda lakini rohoni hana utii  wala utayari bali anaendelea kufanya mambo yake, jambo lenye madhara makubwa kwani Biblia inasema mtu huyu “atapigwa sana”

Na ni wapi atakapopigwa?.. si pengine zaidi ya kwenye ziwa lile liwakalo moto katika siku ya mwisho..

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye AFANYAYE MAPENZI YA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI”.

Sasa ili tuzidi kuona uzito wa jambo hili, tuendelee mbele kidogo na kitabu kile cha Luka, tuone adhabu ya wale ambao hawajajua mapenzi ya MUNGU, lakini wametenda yastahiliyo mapigo, jinsi watakavyoadhibiwa ili itupe kutafakari kwamba “kama wasiyoyajua watapigwa vipi kwa wale walioyajua mapenzi ya MUNGU na hawajajiweka tayari kuyafanya nini kitawapata”.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, ASIJIWEKE TAYARI, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi”.

Umeisikia injili mara ngapi?.. Umefundishwa mara ngapi njia ya kweli na hautaki hata kujiweka tayari?.. je siku ile utasalimikaje kwa maneno yaliyo dhahiri kama haya?. Je utasema sikusikia?..na ili hali hata kujiweka tayari kusikia hukutaka?.. je kuna kusalimika unadhani?… Jibu lipo wazi kuwa hakuna kusalimika, suluhisho ni moja tu, kuanza kujiweka tayari kuyafanya mapenzi yake kabla ya mwisho kufika.

Na kama bado haujaokoka, umechelewa sana, upo nyuma sana, upo mbali sanaa.. leo fanya geuko la maisha kwa kumwamini mwokozi YESU, na kuzingatia kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha, Kwa msaada zaidi juu ya safari ya wokovu, kwa neema tuliyopewa tutakupa mwongozo wa hatua za kufanya, unachopaswa kufanya ni kuwasiliana nasi kupitia namba tajwa hapo chini.

Bwana YESU akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JE! UPO KATIKA MAJI YA UTULIVU?

KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU. 

CHOCHOTE UMFANYIACHO KRISTO KINA THAMANI.

Maana ya Mithali 29:21 “Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe”

Desturi ya maziko kibiblia ilikuwaje?.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply