TUJIFUNZE UNYENYEKEVU WA YOSHUA.

TUJIFUNZE UNYENYEKEVU WA YOSHUA.

Jina la BWANA YESU libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la MUNGU wetu, lililo taa na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Katika Biblia tunasoma jinsi MUNGU alivyomtukuza Mtumishi wake Musa, na hata kufikia wakati kusema akiwapo nabii mwingine yoyote atasema naye kwa ndoto na maono lakini Musa atasema naye mdomo kwa mdomo.

Hesabu 12:6 “Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, NITASEMA NAYE KATIKA NDOTO.

7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;

8 KWAKE NITANENA MDOMO KWA MDOMO, MAANA, WAZIWAZI WALA SI KWA MAFUMBO; NA UMBO LA BWANA YEYE ATALIONA. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”

Sasa kitendo hiko cha Mungu kumtukuza Musa kuliko watumishi wake wengine, iliwafanya wana wa Israeli waamini kuwa hakutatokea tena mtumishi mwingine au nabii mwingine atakayekubalika na MUNGU kwa kiwango cha MUSA.

Na hata Musa alipokufa, na kijiti cha kuwaongoza wana wa Israeli kukabidhiwa mtumishi wa MUNGU Yoshua hakuna aliyemwamini wala kumheshimu Yoshua kwa kiwango ambacho Musa alichokuwa anaaminiwa na kuheshimiwa.

Na hilo MUNGU aliliona na kumwambia Yoshua maneno yafuatayo..

Yoshua 3:7 “BWANA AKAMWAMBIA YOSHUA, HIVI LEO NITAANZA KUKUTUKUZA MBELE YA ISRAELI WOTE, WAPATE KUJUA YA KUWA MIMI NITAKUWA PAMOJA NA WEWE, KAMA NILIVYOKUWA PAMOJA NA MUSA.

8 Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani”

Sasa mbeleni tunaona ni nini kilitokea baada ya MUNGU kumwambia Yoshua maneno hayo, ni kwamba Maji ya mto Yordani yalitimamishwa yasitiririke kwa muda ili kuruhusu majeshi ya Israeli kuvuka, mfano ule ule tu wa jinsi Musa alivyopasua bahari ya Shamu kwa uweza wa MUNGU kuruhusu majeshi ya Israeli kuvuka.

Hesabu 3:14 “Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la agano wakatangulia mbele ya watu,

15 basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno),

16 ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko”.

Sasa ninachotaka tujifunze si jinsi MUNGU alivyokausha Yordani kwa mkono wa YOSHUA, bali ninachotaka tukione na kujifunza ni unyenyekevu wa Yoshua baada ya MUNGU kumwambia kuwa “anaenda kumtukuza katika Israeli, na kuwafanya watu wote wajue kuwa yupo na yeye kama alivyokuwa na Musa”.

Hebu turejee tena tuweze kutembea vizuri

Yoshua 3:7 “BWANA AKAMWAMBIA YOSHUA, HIVI LEO NITAANZA KUKUTUKUZA MBELE YA ISRAELI WOTE, WAPATE KUJUA YA KUWA MIMI NITAKUWA PAMOJA NA WEWE, KAMA NILIVYOKUWA PAMOJA NA MUSA”.

Sasa tungetemea kwamba kuanzia huo wakati Yoshua awaambie wana wa Israeli wote kuwa …“ yeye ndie kiongozi aliyechaguliwa na MUNGU hivyo wamsikilize na kumtii”.. lakini Yoshua hakufanya hivyo, kinyume chake tunaona alienda kuwaambia kuwa “MUNGU yupo na wao wote, na si yeye peke yake”..

Yoshua 3:9 “BASI YOSHUA AKAWAAMBIA WANA WA ISRAELI, NJONI HUKU, MKAYASIKIE MANENO YA BWANA, MUNGU WENU.

10 YOSHUA AKASEMA, KWA JAMBO HILI MTAJUA YA KUWA MUNGU ALIYE HAI YU KATI YENU, NA YA KUWA HATAKOSA KUWATOA MBELE YENU MKANAANI, NA MHITI, NA MHIVI, NA MPERIZI, NA MGIRGASHI, NA MWAMORI, NA MYEBUSI”.

Huu ni unyenyekevu mkubwa sana, ambao tunapaswa kuuiga, na hii ndio sababu ya MUNGU kumtumia Yoshua kwa uhodari mkuu hata kufanya ishara kubwa ambazo Musa hakuzifanya kama “kusimamisha jua”..kwasababu ni mtu aliye mnyenyekevu na mwenye kumrudishia MUNGU utukufu siku zote, si mtu wa majivuno au kujitukuza.

Nasi hatuna budi kujifunza unyenyekevu wa Yoshua, kwani maandiko yanasema kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi lakini huwapa wanyenyekevu neema (1Petro 5:5).

Huenda kuna hatua Mungu kakuvusha, huna sababu ya kujivunia mbele za watu, badala yake mtukuze MUNGU na usubiri Mungu audhihirishe utukufu wake kwako, au labda kuna Baraka Mungu kakuahidia isiwe sababu ya wewe kujitukuza mbele ya watu, au kujionesha kuwa weweni bora kuliko wengine, bali siku zote jifunze unyenyekevu.

Bwana atusaidie, tuwe mfano wa mtumishi wake Yoshua.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

JAWA NA UPENDO UNAOTAFUTA.

MISTARI YA KUOMBEA AMANI YA FAMILIA.

Unyenyekevu ni nini?

KIJAKAZI ALIYEJUA UPONYAJI ULIPO.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply