LAMEKI NA MARA SABINI NA SABA.

LAMEKI NA MARA SABINI NA SABA.

Mwanzo 4:23 -34

23 Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;
24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.

Baada ya Kaini kumuua ndugu yake Habili, tunaona, Mungu anamlaani,na kumwambia atakuwa mtu asiyekuwa na kikao duniani,  lakini alipoomba adhabu yake ipunguzwe, Mungu akasema atakaye muua kaini atalipizwa kisasi mara saba.

Baadaye tunakuja kuona tabia ya uuaji ikiendelea kwa uzao wake, anatajwa mmoja aliyeitwa Lameki, ambaye kwa kosa dogo alilotendewa na mtu, adhabu yake ilikuwa ni kifo, mpaka anashuhudia yeye mwenyewe, anasema nimemuua mtu kwa jeraha, kwa kunichubua. Hivyo kwake uuaji ulikuwa karibu sana. Alikuwa ni mtu hatari, kwamfano akiumizwa tu kwa jeraha dogo, yeye kisasi chake kilikuwa ni kifo.

Lakini bado akajijengea, falsafa yake, kwa majivuno, akisema, ikiwa mtu atalipizwa kisasi mara saba kwa kumuua Kaini, basi mtu yeyote atakayejaribu kunikaribia mimi, kuniua, atakutana na  kisasi  cha mara sabini na saba.

Jambo ambalo Mungu alifanya kwa neema zake ili tu kumstahi Kaini, yeye anatumia kama fursa, ya kujihalalishia na zaidi kujithibitishia ulinzi wa tabia yake ya uuaji, kwa kuongeza Kauli yake, ya kisasi mara sabini na saba.

Lakini lipo jambo ambalo Kristo, alikuja kusema, kwa Habari ya kisasi,

Mathayo 18:21-22

21 Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?
22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

Lameki anataka kisasi mara sabini na saba, Kristo anasema samehe mara saba sabini.

Ulimwengu unaishi kwa visasi visivyokoma, lakini ufalme wa Mungu unatembea katika msamaha usio na ukomo. Uzao wa Mungu unasemehe, Uzao wa Kaini, unawaza kuharibu, na kuua, kwasababu ndio tabia ya shetani tangu mwanzo.

Moyo wa chuki, visasi, vinyongo, ndio uuaji wenyewe,  ni moyo wa Kaini, ambalo ulianzia kwa ibilisi, Uuaji wa sasa sio Kwenda kumwaga damu, lakini kumchukia ndugu yako ni saw ana muuaji.

Hivyo ni lazima tuhakikishe maisha yetu yanageuzwa, na anayegeuza maisha ni Yesu Kristo peke yake. Swali ni Je! Umemwamini Kristo?

Kama Hapana basi wakati ndio huu, okoka, uupokee wokovu, uzaliwe mara ya pili.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply