MUNGU AKAAYE KATIKA GIZA KUU.

MUNGU AKAAYE KATIKA GIZA KUU.

Shalom nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 

Ukichunguza utagundua kuna mahali ambapo watumishi wa Mungu, kwa namna fulani wanakwazika, hadi wengine wanaanzisha mashambulizi ya wazi kabisa pale wanapoona baadhi ya vitu ambavyo si vya kiungu vinasimama kwenye eneo la Injili au kazi ya Mungu.

Tengeneza picha wacha Mungu wa kweli wakati ule  wanawaona mamajusi (wasoma nyota), wanawaetea habari za kuzaliwa kwa Yesu duniani, unadhani lilikuwa na ladha nzuri kwao?  mchawi wa Endori analeta taarifa za Samweli, Koreshi mfalme wa kipagani Mungu anamwita mchungaji wake? Ni kama mambo yanachanganyikana hivi.

Wakati mwingine unaweza kusema mbona Mungu anajipinga mwenyewe?

Tunasoma katika maandiko..

Wakati fulani Mungu alimtokea Musa katika giza nene sana, na sisi tunajua Mungu ni nuru hakai gizani, ni wazi kuwa wote wanaotokewa na Mungu ni lazima nuru iwaangazie kama kiwakilishi chake mfano Paulo alivyotokewa na Yesu kule Dameski, lakini tunaona hapa Mungu anamwita Musa katika giza nene.

Kutoka 20:21

[21]Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia LILE GIZA KUU MUNGU ALIPIKUWAPO.

[22]BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni. 

[23]Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. 

Hili ni jambo gumu ambalo huwenda liliwashangaza sana wayahudi, je Musa anaitwa na Mungu gizani? Mbona Mungu anajitokeza mahali pa ajabu hivi, gizani?

Kwanini asingemwita ndani ya mawingu meupe?  Kwenye mwali wa moto kama afanyavyo? Ni kwanini Mungu afanye vile?

Ni kwasababu anataka tufahamu kuwa njia zake hazichunguziki. Yeye hakaririki. 

Warumi 11:33

[33]Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! 

Tukijua kuwa Mungu ni zaidi ya upeo wetu, basi tusimfunge Mungu katika namna fulani moja, kwamba ili Mungu kumbariki fulani ni lazima awe mtoaji mkubwa sana, ili Mungu ampe yule miujiza mikubwa ni lazima awe mwombaji na mfungaji.

Ili yule awe mtumishi wa kweli wa Mungu ni lazima apite chini ya walezi wa kiroho, kama hana huyo basi hawezi tumiwa na Mungu.

 Ni kweli kwa sehemu kubwa ya wito wa  ki-Mungu hufuata mikondo hiyo, lakini alikuwepo yule mtu anayefanya miujiza kwa jina la Yesu lakini hafuatani na Yesu kabisa wala mitume wake, mpaka mitume wakaanza kumpiga vita..baadaye wakaja kujua kuwa walikuwa wanashindana na kusudi la Mungu.(Marko 9:38-39)

Tafsiri yake ni nini?

Kuna mahali sisi kama watoto wa Mungu tunalazimika kuikubali mipaka na kukiri kuwa si kila njia ya Mungu tutaielezea ipasavyo, kwasababu anaweza kujitokeza pia katika giza  nene, Hivyo tukijua hilo hatupaswi kupoteza muda wetu mwingi kupambana na watu, bali tutumie nguvu zetu nyingi kusimama na kweli, mengine yabaki kwa Mungu tukijua kuwa Iwe kwa hila au kwa nia njema, injili itahubiriwa tu, sisi tutasimama katika njia yetu aliyotuonyesha Bwana.

 Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply