by Admin | 31 December 2019 08:46 pm12
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu..
Wafilipi 4:12 “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.
13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.
Huu ni mstari unaohamasisha sana, hususani tunapopitia katika hali Fulani ngumu, pale tunapoona hatuwezi kuvuka au kuendelea mbele katika kitu fulani, pale tunapoona bado hatua moja tu ya sisi kukata tamaa.. Lakini tunapousoma mstari huu unatupa nguvu ya kuendelea mbele.. Na kubakia kusema..
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu..
Lakini kama ukisoma vizuri mistari ya juu yake utaona mtume Paulo anazungumzia mambo aliyoyapitia huko nyuma, kuna wakati alipitia kufanikiwa sana, vilevile kuna wakati alipitia kuishiwa sana, akawa hana hata shilingi mfukoni mwake, au kama anayo basi ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji aliyokuwa nayo.Tunalithibitisha hilo, wakati Fulani Paulo akiwa Rumi alimwagiza Timotheo na kumwambia siku atakapokwenda aende la lile joho lake aliloliacha kwa Karpo kabla ya wakati wa baridi kuanza.
2Timotheo 4:13 “Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi”.
Kulikuwa hakuna sababu ya Paulo kumwambia Timotheo ambebee joho lake asafiri nalo mamia kama sio maelfu kwa maelfu ya kilometa na mzigo wa koti, Mtume Paulo angeweza tu kununua joho(koti) lingine kule kule kama angekuwa na fedha ya kutosha, lakini hiyo yote ni kwasababu wakati wa kupungukiwa ulimpitia, lakini hakuiacha imani na maneno yake yalikuwa ni haya.. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
Paulo anasema tena nimefundishwa kushiba na kuona njaa.. Katika ziara zake za kuhubiri injili alipitia vipindi vigumu sana mahali ambapo hakukuwa na namna yoyote ya kupata chakula, tunaweza kuliona pia hilo wakati ule alipokuwa anasafirishwa pamoja na wafungwa wengine kuelekea Rumi..Wakiwa kule kilindi kwa muda mrefu waliishiwa na chakula, mpaka watu waakanza kuishiwa na nguvu..Lakini Mungu alimuuokoa yeye pamoja na wafungwa wale katika hali ile, wala hakutetereka katika imani yake..
Matendo 27:20 “Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.
21 Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.”
Na ndio maana hata huku mbele anaoujasiri wa kusema..
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu..
Anasema tena, nimefundishwa kuwa na vingi na kupungukiwa. Kuna wakati alifika hakuwa na haja ya kitu chochote, mpaka akawa na kitu cha kuwagawia wengine, lakini pia kuna wakati ulifika wa kupungukiwa lakini katika hayo yote kimiujiza ujiza katika vipindi hivyo vyote, baridi , joto, mvua na mafuriko hakutikisika hata kidogo katika imani yake..Anasema:
2Wakorintho 11:26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.
28 Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.
Unaona, mtu kama huyu pamoja na kupitia taabu zote hizi, na bado hajaiacha imani ataachaje kusema..
“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”?
Lakini nataka nikuambie mpaka mtu apokee uweza huu wa kuweza mambo yote..Si suala la kujiamulia tu mtu mwenyewe kwa bidii zake, au kujitamkia tu kwa kinywa chake..Unaweza ukajitamkia kuanzia januari mpaka Disemba kwamba “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Lakini ikija tufani kidogo tu unaweza kwenda na maji.
Kama wewe sio mkristo, ukweli ni kwamba huyawezi mambo yote..Kama unajiita mkristo halafu hujaokoka, bado huyawezi mambo yote..Wala usijidanganye kusema hivyo,…Hutakaa uweze kushinda majaribu yote ya huu ulimwengu na bado ukadumu kwa Kristo kwa moto ule ule, hutakaa uweze kustahimili taabu zote na bado usifanye dhambi..Kwamwe hutakaa uweze..
Kumbuka mtume Paulo hasemi “Nayaweza mambo yote katika mimi au katika nguvu zangu”.. anasema, Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu..”Yeye anitiaye nguvu”..Hivyo ni lazima huyu akutiaye nguvu awe ndani yako ndio uwezo huo wa kuweza mambo yote ukujie.
Unajiuliza saa nyingine ni kwanini unajaribiwa na vishawishi vya uzinzi, halafu unazidiwa na tamaa unakwenda kufanya uzinzi, ni kwasababu huyo akutiaye nguvu za kuweza kushinda vishawishi hivyo hayupo ndani yako, kama angekuwepo usingekaa utamani kufanya jambo hilo..
Au ulitamani usitazame pornography, au usifanye punyeto lakini ukajitahidi siku mbili,tatu mbele. Mwezi ulipopita ukazidiwa na tamaa ukaenda kurudia yale yale uliyokuwa unayafanya…Ni kwasababu gani? Ni kwasababu Yule ambaye angepaswa kukutia nguvu ya kuweza kushinda majaribu hayo milele hakuwepo ndani yako.
Au ulikuwa unaonyesha dalili ya kumpenda Mungu kweli, lakini ulipokutana na vita kutoka kwa ndugu au wazazi wako, au marafiki wako, wakakuzidi nguvu, ukayarudia yaleyale uliyokuwa unayafanya mwanzoni kwa kuogopa tu utatengwa au utachukiwa..Ni kwasababu gani ulishindwa kustahimili? Ni kwasababu Yule akutiaye nguvu hakuwa ndani yako.
Au ulikuwa ni mkristo mzuri tu, unashuhudia hata wengine habari njema..lakini labda ulipitia hali Fulani ngumu ya kiuchumi, ukayumba kidogo na hiyo ikakufanya uamue kuacha wokovu wako na kwenda kujichanganya na dunia..Ni kwanini ulishindwa kuendelea mbele na imani? ni kwasababu Yule akutiaye nguvu ulishamwacha zamani.
Au sio tu katika shida, bali pia hata katika mafanikio,..Pengine Mungu alipokufanikisha katika kitu Fulani, labda pengine alikupa kazi nzuri yenye mshahara mkubwa, au alikupa nyumba nzuri, au alikupeleka nchi za nje kuishi, au alikuponya ugonjwa wako, na matokeo yake umemsahau Mungu wako umeyarudia yale yale ya zamani..Na leo hii unajiuliza imekuwaje kuwaje nimechukuliwa kirahisi na fahari za ulimwengu huu.. Jibu ni kwamba Yule akutiaye nguvu amekuacha na ndio maana huyawezi mambo yote.. Katika hayo bado huwezi kudumu katika njia wa wokovu..Umepimwa katika mizani nawe umepunguka.
Lakini leo hii ukasema ninataka kuanza upya na Bwana, ninataka atembee na mimi, anipe uwezo wa kuyaweza mambo yote, katika milima awe na mimi kunitia nguvu, katika mabonde awe na mimi kunifariji, katikati ya maadui awe na mimi kama mchungaji wangu, katikati ya vilindi awe nahodha wangu, katikati ya raha awe furaha yangu nisimuache..katikati ya mafanikio awe tajiri wangu, katikati ya afya awe sifa yangu..katika chochote kile kiwe ni chema au kibaya, bado awe ni Bwana na mwokozi wa maisha yangu..
Nami niwe na ujasiri wa kusema.. “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” Shetani haniwezi kwa wimbi lolote atakalolita mbele yangu.. Unahitaji uwezo huo sasa ukujie??
Kumbuka ili uweze kupokea nguvu hizo kutoka kwa Bwana, yeye anachotaka kwako tu ni MOYO wa TOBA unaotamani tu kugeuka na kuacha..Moyo uliomaanisha kweli kweli kuacha hivyo vitu..Watu wengi hawaoni matokeo yoyote au badiliko lolote katika maisha yao kwasababu tu, hawamaanishi kuviacha vitu walivyokuwa wanavifanya nyuma.
Mwingine ni mlevi, anataka Mungu ampe nguvu ya kuacha ulevi, lakini hayupo tayari kuacha ulevi wenyewe, mwingine anakula ugoro, mwingine anavuta sigara, mwingine madawa ya kulevya, mwingine punyeto, mwingine ukahaba, wote hawa wanataka Mungu awepe nguvu ya kuacha lakini wao wenyewe bado wanatamani kuendelea kufanya hivyo vitu..
Ukisema nataka niache, unatakiwa umuonyeshe Mungu unakichukia hicho kitu kweli kweli, na kwamba ndio sababu ya kukupeleka kuzimu..Mungu anataka watu wanaomaanisha na sio watu wanaojaribu..Na Mungu akishaona moyo wako kama huo ambao unaambata na vitendo basi moja kwa moja anakushushia nguvu ya ajabu ambayo hiyo itakufanya wewe uone yale uliyokuwa unayafanya nyuma ni takataka na uozo,..
Sisi tulikuwa ni wazinzi wa kupindukia, tulikuwa ni watazamaji wa pornography, tulikuwa ni walevi, tulikuwa ni watukanaji lakini uwezo huo uliposhushwa juu yetu KIU ya hayo mambo yote yalikatwa ghafla. Na muda wote tulikuwa tunatamani tu kumjua Mungu..Na hadi sasa ni miaka mingi imepita hata chembe ya mambo kama hayo haipo ndani yetu.. haijalishi ni vishawishi vingapi vinakuja mbele yetu ..tunaoujasiri wa kusema..
“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”
Tumejengwa juu mwamba imara usioweza kutikiswa kwa kitu chochote.
Hivyo kama Mungu alikuwa mwaminifu katika Neno lake kutufanyia sisi hivyo..Anao uwezo huo pia wa kukuanyia na wewe leo hii kama utakubali..
Kama upo tayari kufanya hivyo kumpa Bwana Maisha yako…
Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo. Ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako sawasasawa na Matendo 2:38. Kumbuka ubatizo sahihi ni muhimu sana kwa mtu aliyeokoka hivyo usipuuzie agizo hilo la Bwana.
Zingatia hayo na Bwana atakuwa pamoja nawe. Vilevile Usiacha kutembelea Website hii https://wingulamashahidi.org mara kwa mara ili ujifunze maneno ya uzima..
Ubarikiwe sana.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.
ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.
KIFO CHA REINHARD BONKEY KINAACHA UJUMBE GANI KWETU?
NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.
Kwanini Musa alipewa mbao mbili za mawe na sio moja au zaidi
UNYAKUO.
CHUKIZO LA UHARIBIFU
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/31/kwanini-nayaweza-mambo-yote-katika-yeye-anitiaye-nguvu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.