SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.

SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.

Ukisoma biblia kuna maneno  mtume Paulo aliyasema ambayo kwamfano yangetamkwa leo mbele za watu wengi, kimsingi yangeonekana kama ni kufuru. Jaribu kuwazia heshima Mungu aliwayowapa  mitume wake  12, hata kabla hawajaanza  kutumika  Mungu aliwaandaa kwa muda wa miaka 3,ukizingatia maandalizi yao hayakuwa kama haya ya kwetu, wao walipewa nafasi ya juu sana ya kipekee ya kuishi, kula, kulala na mkuu wa uzima mwenyewe kwa muda wa miaka mitatu na nusu.

Watu ambao Kristo mwenyewe alisema wamesha kuwa safi kwa lile Neno alilokuwa anawafundisha (Yohana 15:3), watu ambao Yesu aliyewatawaza mwenyewe na kuwatia mafuta wawe misingi ya Kanisa lake takatifu lililohai, Watu waliokuwa wamejaa Roho wa Mungu wenye sifa, na vyeo, walioheshimiwa na kuogopwa na kila mtu katika kanisa la Kristo mitume 12 wa Bwana.


Lakini ilifika wakati  siku moja mkristo mmoja aliyechipukia chini asiyejulikana sana ambaye hata hakuwepo siku ya Pentekoste anasimama kwa ujasiri na kuyaeleza makanisa  hakuna kitu cha ziada alichokiona wanacho zaidi yake yeye, licha ya kuwa na sifa nyingi katikati ya watakatifu lakini bado anasema wote wao ni mamoja kwake,. Habari Hiyo Tunaisoma katika..

 Wagalatia 2:6 “Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu; 

7 bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa;

 8 (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); 

9 tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”

Unaweza ukajiuliza  ni kwanini mtume Paulo alisema vile?, unadhani ni kwa kuonyesha kiburi chake kwa kufanikiwa kwake au vinginevyo?, jibu ni hapana lakini aliuzungumza ukweli wote katika Kristo, kwamba Mungu hapokei uso wa mwanadamu yoyote na ndivyo ilivyo. Kama biblia inavyosema katika

Matendo 10:34 “… Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; 

35 bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”

Mtume Paulo alionyesha kuwa sio cheo, wala maono,wala karama wala sifa yoyote ile itokayo kwa Mungu au kwa mwanadamu ndiyo kiashiria cha mtu huyo kuwa analo daraja kubwa mbele za Mungu, na kwamba hakuna yeyote atakayeweza kuwa juu yake kisa tu kaitwa  na Mungu.. Ilifikia wakati Mtume Paulo kwa neema za Mungu alizopewa alijishuhudia katika Roho kuwa kati ya waliomtangulia hakuna aliyetenda kazi zaidi yake yeye. ( 1Wakorintho 15:10), Leo  tunaweza kujifunza machache juu ya matukio ya mitume yaliyorekodiwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume.

MATENDO YA MITUME:

Ndugu kitabu cha Matendo ya mitume, unajua ni kwanini kiliitwa vile?. Kilitwa vile kwasababu Ule ulikuwa ni uwanja wa mapambano katika roho kati ya mitume wa Kristo wote waliokuwepo kwa wakati ule, Kila mmoja akionyesha matendo ya Imani yake katika mashindano yaliyokuwa yamewekwa mbele yake.Lakini kama ukichunguza kwa makini utaona mwanzoni kabisa mwa sura za mwanzo za kitabu kile,

Ulikuwa unaweza kusoma habari za watu wengi na watakatifu wengi, na ushujaa wao wote waliokuwa wanaufanya, pamoja na habari za mitume mbalimbali wa Kristo, utaona kulikuwa na watu 500 waliotokewa na Kristo baada ya kufufuka kwake  kama alivyotokewa mtume Paulo,Ambao Bwana alifanya makusudi kujidhihirisha kwao ili wakawe mashuhuda wa kutangaza habari ya kufufuka kwake, utawaona pia wale watu 120 waliokuwako siku ile ya Pentekoste, utamwona Filipo,akitenda kazi ya Mungu kwa bidii, kadhalika utaona  habari ikirudi tena kwa Yohana, Utamwona Barnaba, utamwona Stephano, utamwona Petro, utawaona wakina Prisila na Akila, utamwona Anania, Apolo, utamwona nabii Agabo, Marko, Sila, luka, na wengineo.

Na kila mmoja ambaye habari zake zilisikika,  Mwandishi aliyevuviwa na Roho aliyekiandika  kitabu kile cha matendo ya mitume aliziweka habari zake, hakukuwa na upendeleo wowote. Na ndio maana ukichunguza mwanzoni walianza wengi kwa moto, habari za kila mmoja zikawa zinagusiwa, mara huyu, mara  Yule, lakini ukizidi kuendelea mbele kuanzia sura ya 13…mpaka ya mwisho kabisa wa sura ya 21 utaona ni Paulo tu peke yake ndiye anayezungumziwa kana kwamba hakukuwa na wengine wanaofanya ziara au wanaotenda kazi ya Mungu.

Sio kana kwamba hawakuwepo, walikuwepo, lakini aliyeonekena anapiga mbio zaidi ndio habari yake iliyopewa uzito mkubwa zaidi kuandikwa. Ni kama leo tu kwamfano  ukiangalia kwenye TV labla wanariadha wanaoshiriki katika michezo ya kukimbia umbali wa km 40, utaona kwa pale mwanzo  kamera haimlengi mtu Fulani mmoja maalumu, bali watu wote, kwasababu bado haijajulikana mshindi atakuwa ni nani, hivyo Yule anayeonekana inaongoza wenzake kamera itamchukua,

Kadhalika akipitwa tu kidogo kamera itahahamia kwa mwingine hivyo hivyo. Lakini ukiangalia wakishafika labda km ya 30 kuelekea 40 hapo wameshaachana nafasi kubwa sana, utaona kamera inamchukua tu Yule wa kwanza peke yake mpaka anapokwenda maliza. Kana kwamba ni yeye tu ndiye anayeshiriki michezoni lakini ukweli ni kwamba huko nyuma kuna umati wa mamia ya watu nao pia wanapiga mbio isipokuwa wameachwa nyuma sana.

Na ndivyo ilivyokuwa katika kitabu cha matendo ya mitume, Walianza wengi, lakini aliyemaliza ni mmoja. Naye si mwingine zaidi ya Mtume Paulo. Sio kana kwamba yeye alikuwa na kitu cha ziada sana zaidi ya wale wengine hapana, walikuwepo watu 500 waliotokewa na YESU kama yeye, na wengi wao walikuwepo siku ya Pentekoste na pengine hata kabla ya hapo, Bwana alitazamia na wao pia wapige mbio lakini kilichomtofautisha Mtume Paulo na wengine ni kwamba yeye alikuwa akimwomba Mungu neema na akionyesha bidii katika Bwana.

Lakini mambo hayo yanatufundisha nini?. Hayo yalitendeka katika kanisa la kwanza, lakini pia  lilikuwepo kanisa la pili na la tatu na la nne mpaka la mwisho la saba ambalo ndilo hili tunaloishi mimi na wewe, na kila kanisa linao mitume wake [watumishi wa Mungu],  nao pia kitabu cha matendo yao kinaandikwa mbinguni wanarekodiwa wanaopiga mbio,

Lakini swali je! Ni nani atakayemaliza na ushindi kwa Laodikia?.. Ni William seyomor, mwanzilishi wa kanisa la Pentekoste, ni Billy Granham? ni Oral Robert, ni WILLIAM BRANHAM mjumbe wa Kanisa la LAODIKIA? Ni TL Osborn Ni Hellen white? Ni Kulola, ni Kakobe, ni mchungaji wako, mwalimu wako wa madarasa ya jumapili? au ni WEWE?..

Hakika unaweza ukawa ni wewe.

Wote wanaodai walitokewa  na YESU na kupewa huduma kubwa wawe ni mamoja kwako, kwasababu wapo sio tu kutokewa , bali pia kuishi naye na kulala naye lakini bado walipitwa katika mbio, wanaodai wameonyeshwa maono makubwa sana watakuwa ni wainjilisti wa kimataifa wawe ni mamoja kwako, walio na sifa kubwa katika taifa na kanisa kuwa ni watumishi wa Mungu wawe ni mamoja kwako, wanaojulikana kuwa ni wajumbe wa makanisa na manabii wa vizazi wawe ni mamoja kwako Mungu hapokei uso wa mwanadamu.

Tujifunze kwa Mtume Paulo mtu ambaye hapo mwanzo aliuharibu uzima wake kuliko watu wote, lakini baada ya kutubu kwake alisimama na kuanza upya na kushinda kuliko wote  waliomtangulia yeye alisema maneno haya:

1Wakorintho 9: 23 “Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine. 

24 Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. 

25 NA KILA ASHINDANAYE KATIKA MICHEZO HUJIZUIA KATIKA YOTE; BASI HAO HUFANYA HIVYO KUSUDI WAPOKEE TAJI IHARIBIKAYO; BALI SISI TUPOKEE TAJI ISIYOHARIBIKA. 

26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; 

27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”.

Alisema pia..

2 Timotheo 2: 4 “Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari. 

5 HATA MTU AKISHINDANA KATIKA MACHEZO HAPEWI TAJI, ASIPOSHINDANA KWA HALALI. 

6 Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda. 

7 Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.”

Je! Mambo ya dunia bado yanakusonga na huku bado unataka ufanikiwe zaidi ya hao mashujaa wa imani Hilo wingu kubwa la mashahidi lililotutangulia lililonenwa katika Waebrania 12 wanapaswa wawe mamoja kwetu?. Weka kando mizigo yote ya dhambi chini, tubu dhambi zako anza kumwangalia Bwana kwasababu ushindi hakika utaupata kama ukishindana kihalali.

Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, 

2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

SIKU ZA MAPATILIZO.

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

ALITOKA HUKO, AKAENDA MAHALI KARIBU NA JANGWA.

MARIAMU

Podo ni nini na umuhimu wake ni upi rohoni?

JE! KUSHIRIKI AU KUJIHUSISHA KWENYE MICHEZO NI DHAMBI?

Tofauti kati ya mbinguni, peponi, Kuzimu, Jehanamu, na Paradiso ni ipi?

JE! NI DHAMBI KWA KIJANA ALIYEOKOKA KUVAA SURUALI ZA KUBANA (MODEL), KUNYOA MITINDO?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joseph Likare
Joseph Likare
3 years ago

Watumishi wa Mungu ninawasalimu katika jina la Yesu Kristo , lakini kitabu cha Matendo kiliandikwa na nani