NI NINI KINAKUPATA UNAPOIPUUZIA INJILI?

by Admin | 1 January 2020 08:46 pm01

unapoipuuzia injili unayohubiriwa mwaka mzima, Ni nini kinakupata?


Siku zote kuna makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni watu ambao wakishaisikia injili kidogo tu, na kuchomwa dhimira zao ndani saa hiyo hiyo wapo tayari kutii na kutubu na kugeuka, mfano wa kundi hili tunalona katika siku ile ya Pentekoste, Mtume Petro alipofungua kinywa chake na kuanza kuwahubiria wale watu waliokuwa wanawashangaa walipokuwa wananena kwa lugha nyingine. Tunaona kwa maneno machache tu ya Petro, wengi wao walikuwa tayari kutubu na kugeuka.

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu’’.

Lakini kundi la pili: Ni lile ambalo hata lihubiriweje injili, hata lioneje miujiza mingi kiasi gani, hata livutwe kwa maneno ya rohoni mazuri namna gani, hata lihubiriwe kuanzia asubuhi hadi jioni, bado litafanya moyo yao kuwa mgumu tu. Mfano wa kundi hili tunaliona kwa mtume Paulo pale alipofika Rumi na kukutana na mkusanyiko mkubwa wa watu ambao walikuwa tayari kumsikia kuanzia asubuhi mpaka jioni tusome.

Matendo 28:23 “Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni.

24 Wengine waliamini yale yaliyonenwa, WENGINE HAWAKUYAAMINI”.

Hata sasa kuna watu wanahubiriwa injili tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka, lakini hawataki kugeuka, japo wanaisikia injili ikihubiriwa mitaani kwao, wanaisikia ikihubiriwa kwenye maredio kila siku, wanasikia injili ikihubiriwa kwenye matelevisheni, lakini bado wanafanya mioyo yao kuwa migumu, wanasikia injili ikihubiriwa mitandaoni kama hivi sasa, kuanzia mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka lakini wanapuuzia tu,wanaona ni kama habari zisizokuwa na manufaa yoyote katika maisha yake….Lakini hawafahamu kuwa maisha yao yapo hatarini sana.

Ndugu Neema ya Kristo si “jua” kwamba itakuwepo wakati wote, Jua likizama leo kuna matumaini kesho yake tena kuchomoza lakini neema ya Kristo ikishakupita ndugu, ndio imekupita hivyo milele, hutasema siku moja nitamgeukia Mungu, kwasababu kumgeukia Mungu ni kitendo kinachochochewa na Roho Mtakatifu mwenyewe, na si kama mtu atakavyo maandiko yapo wazi yanasema hivyo, “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka;(Yohana 6:44)”..Sasa kama Roho wa kukuvuta kwa Mungu hayupo ndani yako, kwamwe hutakaa umfuate Mungu kwa mapenzi yako mwenyewe au kwa jitihada zako..Badala yake kama ulikuwa zamani unasikia kuchomwa unaposikia mahubiri safari hii husikii tena hiyo hali ndani yako..Kama ulikuwa una kiu ya kusikiliza habari za Mungu hiyo kiu inakatika ndani yako…Ukiona hivyo ile nguvu ya kukuvuta kwa Mungu imeshaondolewa kwako.

Na biblia utakiona kama kitabu cha kipuuzi tu kwako, utaishia kukisoa, au kutokiamini kabisa..Hata uhubiriweje injili utasema hawa walokole, wanamsubiria Yesu ambaye harudi wamechanganyikiwa, utasema hakuna unyakuo, utakuwa unajiona unajua kila kitu…Utakuwa huna tofauti na mpagani ambaye hajawahi kumjua Mungu kabisa..

Na kibaya zaidi utakapokuwa unafanya hivyo utakuwa na uhakika wa unachokisema, utajiamini kupita kiasi, wala hutasikia hukumu yoyote ndani yako, kwamba kitu unachokifanya sio sahihi, hilo jambo hutasikia kabisa kwasababu Roho wa Mungu alishaondoka ndani yako siku nyingi..leo hii Unapoona watu wa mataifa wanavyomtukana Mungu usidhani ni wajinga sana, au si watu wa kutafakari sana, si wajinga ni kwasababu Yule Roho wa kuwavuta kwa Mungu hayupo ndani yao, wanatafuta point katika kitu point katika biblia hawaioni, wanatafuta kitu kimoja angalau cha kuwashawishi kuhusu Yesu ili waamini hawakioni…

Na ndio maana wanakufa katika dhambi zao, hata kama umshuhudie vipi habari za kuzimu, Zaidi sana ataishi kukutukana tu. Hafanyi hivyo makusudi, ni kwasababu ni kweli ndani yake hakuna chochote kinachomshawishi au kinachompa kila sababu ya yeye kuamini..

Na ndivyo itakavyokuwa kwa mtu Yule anayeichezea neema anayohubiriwa kila siku.

Biblia inaeleza pia katika agano la kale, kwamba unapofika mwaka wa maachilio, yaani mwaka wa watumwa wote kuwekwa huru..Ni sharti mabwana zao wawaache huru, amruhusu kila mmoja arudi nyumbani kwake kama alichukuliwa kwao, au aende kwake kama alishakuwa na kwake. ..Lakini sasa kama ikitokea mtumwa Yule anaukataa uhuru aliopewa..Yaana kwa mapenzi yake mwenyewe anasema mimi sitaki kuondoka kwa bwana wangu nataka kuendelea kuwa mtumwa wake milele. Soma.(Kumbukumbu 15:17)

Basi Yule Bwana wake anachofanya ni kuchukua uma wa moto, na kumtoboa sikio lake.. Na ile inakuwa kama muhuri kuwa Yule mtumwa sasa atamtumikia Bwana wake milele..Kama vile lile shimo katika sikio linavyokaa milele, ndivyo hivyo na yeye atakavyokaa katika hali hiyo ya utumwa milele.

Na leo hii Mungu anatutangazia mwaka wa maachilio, kwa kupitia damu ya mwanawe mpendwa Yesu Kristo kwamba kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Lakini kama inatokea mwaka huu tuliopewa wa maachilio, tunauchezea, bado mguu mmoja upo nje mwingine ndani, bado tunaendelea kuutamani utumwa wa shetani ambao ametutumikisha kwa muda mrefu, na haujatupa faida yoyote, bado tunataka kuendelea kuishi katika maisha ya kwenda motoni..Basi tujue kuwa tumetaka hivyo kwa hiari yetu wenyewe.

Sasa kitu kinachofanyika hapo katika ulimwengu wa roho, Yule bwana wako, ambaye ni shetani anakuja na uma huo wa moto, na kuupitisha katika sikio lako la rohoni..Na hiyo inakuwa ishara kwamba wewe ni wake milele..Ukishafikia hatua hiyo basi ile neema ya Mungu unakuacha, wala Mungu hashughuliki tena na wewe. Unakuwa mtu wa tofauti na pale ulipokuwa mwanzo, unaishi kuwa mtoto wa shetani ukisubiria kufa uende kuzimu.

Tangu Januari mpaka Disemba hii unasikia injili, Mungu anakupa neema ya kuwa na pumzi ya kuishi, aone kama huu mwaka hautaisha unamgeukia yeye, lakini bado hufanyi hivyo, alikutazama miaka ya nyuma lakini bado ukawa vilevile, na tena unaenda kuingia mwaka mwingine mpya, na bado unataka kuendelea kuwa katika hali hiyo hiyo ya dhambi..Unadhani neema ya Kristo itazidi kukusubiria hivyo milele?..Ule Uma shetani ameshauandaa, anasubiria wakati wake ufike tu..Na moja ya hizi siku usipokuwa tayari kuchagua njia ya kuiendea, ibilisi atakuchagulia njia kwa nguvu.

Ndugu kitu cha kuthamini cha kwanza katika maisha yako ni hii neema, ambayo haipo kwa watu wote. Mpaka sasa Bado unaendelea kunywa pombe, bado unaendelea kuzini, bado unaendelea kwenda disko, bado unatazama pornography, bado unafanya masturbation na hali unajua kabisa ni dhambi.. bado unafanya biashara haramu, bado unakula rushwa, bado ni mchawi na mshirikina wa chinichini, bado unakwenda kwa waganga, bado unaendelea kuishi na huyo mtu ambaye hamjafunga ndoa, ambaye si mke wako wala mume wako..Na kibaya zaidi wakati huo huo bado unaisikia injili ya kristo na kuipuuzia.

Injili ya Kristo sio kiburudisho kama miziki ya dunia hii ambayo unaisikiliza unapotaka kupunguza mawazo..Biblia imesema kuwa “Mungu hadhihakiwi, apandacho mtu ndicho atakachovuna”

Yageuze maisha yako kwa Bwana..Na yeye yupo tayari kukubadilisha kama utataka kumpokea leo hii. Anachotaka kwako ni aumue kwa moyo wako wote kugeuka leo, na sio nusu nusu, kama bado hujafikia kiwango cha maamuzi hayo ni heri uendelee tu..Kwasababu Mungu hatakugeuza na kukufanya kuwa mtu mwingine kama utakuwa bado unayatamani maisha ya dhambi..

Lakini kama unasema leo hii nipo tayari kumgeukia Yesu Kristo na nataka kuanza mwaka wangu mpya nikiwa ndani ya wokovu. Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika hali ya utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI KWA MUDA MREFU, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU KWA KUTOKUITII SAUTI YAKO KWA KIPINDI CHOTE HICHO. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KWA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo. Ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo kuanzia dakika hii, unaanza kwenda disko kuanzia sasa, unaacha pombe, sigara, uasherati, wizi, na unawasamehe wote waliokukosea kutoka moyoni kabisa.

Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile baada ya hapo unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwabudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako(Sawa sawa na Matendo 2:38). Ubatizo ni agizo la msingi kwa mtu Yule aliyeokoka hivyo usilipuuzie, hata kidogo, wala usijikawiishe kupata ubatizo.

Zingatia hayo na Bwana atakuwa pamoja nawe. Vilevile Usiacha kutembelea Website hii https://wingulamashahidi.org mara kwa mara ili ujifunze maneno ya uzima yatakayokusaidia kukua kiroho katika wakati huu wa kumalizia.

Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

ALIJARIBIWA SAWASAWA NA SISI KATIKA MAMBO YOTE.

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

URIMU NA THUMIMU NI NINI KATIKA BIBLIA?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

NUHU WA SASA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/01/ni-nini-kinakupata-unapoipuuzia-injili/