Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu?

by Admin | 6 January 2020 08:46 pm01

SWALI: Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu, au nikitaka kusoma Neno ninapatwa na usingizi je! hizi ni nguvu za giza zinazisonga au ni nini?.

JIBU: Mtu yeyote aliyeokoka mbele yake, wapo maadui wawili wakubwa, adui wa kwanza ni shetani, na adui wa pili ni Mwili.

Shetani anachofanya ni kuhakikisha kuwa unakaa mbali na Mungu..Atafanya hivyo kwa kuhakikisha analeta kila namna ya presha za nje ili tu kukufanya uchukie maombi au ukose muda wa kusoma Neno la Mungu kwa ujumla..Anaweza kutumia ndugu, au mke au mume, kukukataza kusali, anaweza kunyanyua mazingira Fulani ili kukufanya ukose muda kwenda maombi, au kusikiliza maneno ya Mungu.

Kwamfano muda ambao ungepaswa uwe unasali, shetani anakuletea vipindi vya tamthilia kwenye televisheni, anakuletea magroup ya kuchati, anakuletea party za kuhudhuria, kazi Fulani ya kufanya n.k. Na kama mtu usipokuwa na msimamo katika imani yako , kuhakikisha kuwa Mungu anapewa nafasi ya kwanza, basi utachukuliwa na ulimwengu na kujikuta umesharudi nyuma,.baadaye ndio unakuja kushtuka ukiangalia mara ya mwisho kuomba ilikuwa ni miezi miwili iliyopita, mara ya mwisho kusoma biblia ni miezi mitatu iliyopita…Na ukijaribu kufanya tena hivyo huwezi…Hali kama hiyo ikishakukuta basi ujue shetani amekuweza.

Lakini Adui wa pili ambaye ni mwili: Tofauti na watu wengi wanavyofikiri, kwamba Ukiwa ibadani halafu ukasinzia basi huyo ni shetani aliyekufanya usinzie, au ukiwa anasoma Neno nyumbani ukasinzia basi huyo ni shetani aliyekufanya ulale,..Nataka nikuambie huyo sio shetani bali ni mwili wako mwenyewe. Ukishaokoka shetani hana mamlaka na mwili wako.

Wale ambayo hawajaokoka labda shetani ndio anaweza kuwaletea nguvu nyingine za mapepo kwenye miili yao ili wasimkaribie Mungu, lakini kwa mtu aliyeokoka, shetani hawezi kufanya hivyo.

Yesu alipowachukua wanafunzi wake watatu na kwenda kusali nao saa chache kabla ya kwenda kuteswa, alirudi na kuwakuta wamelala..akawaamsha wasali, akaenda kusali akarudi tena akakuta wamelala ,..Lakini Bwana Yesu hakukimbilia kuwaambia mna mapepo ndani yenu kemeeni hizo roho, hapana alijua tatizo ni nini ndipo akawaambia maneno haya:

Marko 14:37 “Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?

38 Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.

39 Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo”.

Unaona? Aliwaambia Roho I radhi, lakini mwili ni dhaifu..Mwili sikuzote unashindana na roho, haupendi mambo ya rohoni, wakati unasema nataka kusali, mwili unasema lala, wakati unasema nataka nisome Neno la Mungu, mwili unakuambia umechoka sana pumzika, kesho utafanya hivyo.

Hivyo njia pekee ya kuushinda mwili wako ni kuulazimisha uitii Nia ya Kristo. Usiubembeleze, hakikisha ukitaka kusali unakaa mahali ambapo hapana vichocheo vya usingizi, hudhuria ibada za maombi, jumuika na watakatifu wengine katika kusali, hiyo inasaidia sana, biblia inasema kamba ya nyuzi tatu haikatiki haraka..Ukisali na mwenzako utapata motisha na nguvu ya kuzidi kusali kuliko unavyoweza kusali mwenyewe. Ukitaka kila siku kwenda mwenyewe mwenyewe kuna mahali utakwama tu.

Vilevile hakikisha unajijengea utaratibu wa kuongeza kiwango chako cha kusali kila siku..Kama uwezo wako ulikuwa ni dakika 15 kesho ongeza nyingine 5, kesho kutwa 5, hivyo hivyo hadi mwezi unapoisha unakuta uwezo wako wa kwenda masafa marefu umeongezeka, unaenda hata masaa kadhaa katika maombi bila kusimama.. Na ukawa bado hujachoka, siku umesali nusu saa unajiona hujasali kitu.

Vile vile ongeza bidii binafsi katika kujifunza Biblia kila siku, hakikisha siku haipiti bila kusoma NENO,.. sio kusoma mstari Fulani na kwenda kulala, hapana, bali kusoma na kulitafakari Neno, na kujifunza, kwa muda mrefu kwa jinsi uwezavyo..kila jambo linahitaji bidii..

2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Ukizingatia hayo, hutaona ugumu wowote katika kutimiza nguzo zote za Imani.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

Je Mahari ina ulazima wowote?

JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?

JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

NENO LA MUNGU NI TAA

KUOTA UNAENDESHA GARI.

Je! Ni dhambi kwa kijana aliyeokoka kuvaa suruali za kubana (model), kunyoa mitindo (mfano kiduku), ?

KIFO CHA REINHARD BONKEY KINAACHA UJUMBE GANI KWETU?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/06/kwanini-kila-nikitaka-kusali-naingiwa-na-uvivu/