NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

by Admin | 9 January 2020 08:46 am01

Neno la Mungu au kwa jina lingine linaitwa Gombo, ni dawa inayoponya maisha ya mtu kwa ujumla.Tofauti na Dawa nyingine, ambazo zinaweza kuishia kuponya mwili tu, na baada ya hapo hakuna kitu kingine zinaweza kufanya, na licha tu ya kutibu kifo bali hata nafsi iliyopondeka hakuna dawa yoyote inayoweza kuiponya isipokuwa Neno la Mungu peke yake, (Mithali 4:20-22), Na hiyo ndio inayolifanya Neno la Mungu liwe ni dawa bora kuliko dawa yoyote ambayo ilishawahi kuwepo duniani.

Lakini pia kabla ya kuzifurahia dawa tunapaswa tujifunze asili ya dawa jinsi zilivyo, kama mtu hajui dawa huwa zinaasili gani basi ni rahisi kukata tamaa na asikae arudie tena kuzijaribu ..Kwasababu sikuzote dawa huwa hazina ladha nzuri mdomoni, dawa nyingi ni chungu, tena chungu kweli kweli kiasi kwamba zinakufanya uzimeze nzima nzima, vinginevyo unaweza kutapika endapo ukizitafuna..Lakini tunajua pamoja na uchungu wake wote huo zikishafikia tumboni basi uchungu wote unakuwa umeisha hatuusikii tena, baada ya hapo tunasubiria tu matokeo mazuri ya kuponywa miili yetu, na mwisho wa siku tunazifurahi zile dawa, tunazisifia japokuwa hapo mwanzoni tulikuwa tunakunja nyuso zetu kama vile tunamezeshwa sumu.

VIvyo hivyo tunapaswa pia tujue asili ya dawa KUU (Neno la Mungu) pale tunapokusudia kulila, kwa lengo la kupata uzima, linatabia gani rohoni mwetu..Tofauti na dawa za asili kwamba tunapozila zinakuwa chungu mdomoni mwetu lakini zikifika tumboni zinakuwa ni raha..Neno la Mungu (Gombo) ni kinyume chake.. biblia inasema Mdomo ni tamu kama asali lakini likifika tumboni libadilika na kuwa chungu sana…

Yohana alipopewa kitabu kile (yaani Ufunuo ule) aule alipewa angalizo hilo mapema kabisa..tusome.

Ufunuo 10:8 “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.

9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi”.

Ezekieli naye aliambiwa hivyo hivyo…

Ezekieli 2:9 ‘Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.

10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!

3:1 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.

3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali”.

Unaona asili ya dawa KUU (Neno la Mungu), ni tamu kama asali, wengi tunaposikia habari za kwenda mbinguni kwa kumwamini tu YESU tunafurahia, tunaposikia Yesu anakupenda mwenye dhambi tunafurahia, tunaposikia mafunuo mapya kila siku Kristo anayotufundisha kila kona juu ya habari za ufalme wa mbinguni tunafurahia sana, ni asali nzuri, tunaposikiwa tunahesabiwa haki kwa neema, tunafurahia Zaidi, tunaposikia alifanyika maskini ili sisi tuwe matajari ni maneno mazuri yenye faraja..Hiyo inatufanya wengi tuvutiwe na wokovu, si ndio?..Lakini ili Neno la Mungu lifanye kazi yote ya kumwokoa mtu ni lazima lishuke tumboni limengenywe Uponyaji wa Roho yake uanze kufanya kazi na ndio hapo uchungu unapoanzia..

Wengi wanaishia kulitapika na kurudi nyuma, wanafananishwa na zile mbegu zilizoangukia kwenye miamba, ambao ni watu waliopitia dhiki kidogo tu kwa ajili ya lile Neno wakajikwaa wakarudi nyuma.., Pale Bwana Yesu anaposema jitwike msalaba wako unifuate, wengi hawataki kusikia hivyo, wanataka waendelee kukaa katika dhambi zao na huku wanasema wameokoka, wanataka waendelee kwenda disko na huku wanasema tumeokoka na tumebatizwa, wanataka waendelee kuvaa vimini na suruali na kuweka make-up na huku waseme tumeokoka tunampenda Yesu.

Wakidhani kuwa wameokolewa kweli,?.. Sio tu kufurahia unahubiriwa kila siku Neno la Mungu unasema sasa ninajua mafunuo mengi, ukadhani ndio tayari Umekamilishwa Maisha yako, Hapo ndugu bado hujaanza ikiwa hutataka kuyatiii maneno Bwana Yesu aliyoyasema, basi ujue kuwa wokovu wako ni batili.

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

Injili imekuvuta kwa maneno mazuri na ya faraja kwa muda mrefu, umeshauona uzuri uliopo ndani ya Kristo kwa muda mrefu, umeshajua faida zote mtu anazozipata akimfuata Kristo, unaendelea kulifurahia tu Neno la Mungu mdomoni mwako lakini hutaki kulimeza, kisa tu unaogopa Baba atanitenga, mama atanichukia, marafiki watanionaje..kazini watanifikiriaje, wakisikia mimi nimeokoka,..Ndugu kama unapenda Kristo ayaokoe Maisha yako kikweli kweli unapaswa ufanye maamuzi hayo pia..

Mathayo 10:34 “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;

36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.

Huu ni wakati wa kuyapokea maneno ya Mungu kwa moyo wote na kuyafanyia kazi, hizi ni siku za mwisho za kanisa la watu walio vuguvugu lijulikanalo kama Laodikia (Ufunuo 3:14)ambao watu wake ni watu walio vuguvugu wa hali ya juu sana..Na hao Kristo amesema atawatapika. Je na wewe unasubiri utapikwe baada ya kukaa katika uvuguvugu huo kwa muda mrefu?. Fanya uamuzi wa kulimeza Neno lote zima zima bila kujali ni nini kitakutokea mbele kwasababu kwa kufanya hivyo ndivyo utakavyoinusuru roho yako katika nyakati hizi za uvuguvugu ambao kila mtu hata mlevi, mzinzi, fisadi, hata msanii wa nyimbo za kidunia anasema ameokoka..

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

WAZAZI WA YOHANA NA YAKOBO.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

KUOTA UNAKULA CHAKULA.

URIMU NA THUMIMU NI NINI KATIKA BIBLIA?

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/09/neno-la-mungu-ni-dawa-iliyo-tofauti-na-dawa-nyingine/