JINI MAHABA NI NINI?

by Admin | 9 March 2020 08:46 pm03

Jini Mahaba yupo kibiblia?, Mtu mwenye jini mahaba anakuwaje?

Moja ya elimu inayowachanganya wengi na inayopotoshwa ni Elimu juu ya mapepo..

Mapepo kwa lugha nyingine wanaiwa majini…Ni kitu kimoja kinachojulikana kwa majina mawili tofauti, ni kama MWANADAMU na MTU. Hayo ni majina mawili tofauti lakini yanaelezea kitu kimoja.

Sasa mapepo ni roho za malaika walioasi mbinguni, ambao walitupwa chini pamoja na kiongozi wao mkuu shetani. Baada ya kutupwa chini ndio yakaitwa mapepo.

Mapepo hayo yanaweza kumwingia mtu na kumfanya awe na tabia yoyote ile wanayotaka wao. Mapepo haya yanaweza kumwingia mtu na kumfanya awe mwizi, mengine yanaweza kumfanya mtu awe mlevi, mengine yanaweza kumfanya mtu awe mzinifu au mwenye tabia ya zinaa.

Sasa mapepo ambayo yanawafanya watu wabadilike tabia na kuwa wazinifu au kuhisi wanafanya mapenzi na watu wakati wa kulala ndio hayo WATU wanayoyaita MAJINI MAHABA. Lakini kiuhalisia mapepo hayo hayana jinsia yoyote kwasababu ni roho. Na haya yanapomwingia mtu yoyote ambaye hajaokoka.(yaani ambaye hajampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake) yanamfanya anakuwa mtumwa wa dhambi hiyo ya zinaa katika ndoto au katika maisha yake ya kawaida..Kwa mtu wa kawaida huwa hayamtokei kwa wazi lakini kwa wale ambao wamekufa kabisa kiroho na wamejiuza kwa shetani huwa yanaweza kujidhihirisha kwa macho kabisa..

Lakini kumbuka shetani siku zote ni mwongo pamoja na mapepo yake yote, biblia inasema shetani  anao uwezo wa kujigeuza na kuwa hata malaika wa Nuru (Kasome 2Wakoritho 11:14), hivyo sio ajabu kuweza kujigeuza na kuwa hata mwanamke mzuri au mwanamume mzuri wa kuvutia, lakini ndani yake ni pepo mbaya na mchafu. Watu wengi wanadanganyia na kufikiri kuna mapepo ya kike..Ndugu usidanganyike hakuna kitu kama hicho…hayo ni maroho tu hayana jinsi, shetani ni baba wa uongo siku zote.

Kwa asili roho hizi za mapepo huwa hazimtokei mtu kwa wazi kama tulivyotangulia kujifunza hapo juu, isipokuwa kwa mtu ambaye tayari amejiuza kwa shetani moja kwa moja, hususani kama mtu ni mshirikina, au mganga au mchawi kabisa, huyu anaweza kuziona kwa macho..Lakini kwa wengine ambao wapo nusunusu, vuguvugu..roho hizi zinawaendesha katika ndoto tu na katika tabia zao. Katika ndoto wanakuwa wanaota wanafanya zinaa na katika tabia wanakuwa wanatabia zilizokithiri za uasherati mpaka wengine kuwafanya kuwa mashoga au wasagaji, au walawiti au wafiraji.

Na zifuatazo ni njia mapepo haya yanayozitumia kuingia ndani ya watu.

  1. Kufanya zinaa nje ya ndoa
  2. Kutazama picha/video za ngono/Pornograph
  3. Mazungumzo machafu yahusuyo zinaa na uasherati
  4. Kuvaa mavazi ya kikahaba, kama kuvaa suruali kwa wanawake, na vitop pamoja na vimini
  5. Matumizi ya vipodozi na urembo..ikiwemo kujichubua, kuchonga nyusi, kusuka mitindo mitindo na kujipulizia marashi kupindukia.
  6. Kusoma hadithi na Majarida ya mambo yanayozungumzia zinaa, pamoja na kutazama filamu na movie za maudhui hayo.

Kujitazama kwenye kioo hakuna uhusiano wowote na kuingiwa na roho hizo..Isipokuwa mtu mwenye tabia ya kujipamba, na kujichubua, kusuka suka, kuchonga nyusi anakuwa na tabia ya kujiangalia kwenye kioo mara kwa mara..hivyo hiyo tabia ya kujipamba na kuchonga nyusi ndio mlango wa mapepo hayo kuingia lakini sio kujitazama kwenye kioo.

Biblia inasema katika..

Ufunuo 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo”.

Kilicho kinyonge kinachozungumziwa hapo ndio hicho chenye roho ya mapepo ndani yake..Kwasababu mtu mwenye roho ya mapepo atakuwa na tabia tu fulani chafu ambazo watu wenye tabia hizo biblia inasema hawataurithi uzima wa milele. Mtu mwenye pepo la zinaa/jini mahaba ni lazima atakuwa mzinifu na mbinguni hawataingia wazinifu..Mtu mwenye pepo la ulevi ni lazima atakuwa tu mlevi na mbinguni hawataingia walevi.

Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili..”

Mbinguni wataingia tu watu wenye Roho Mtakatifu..ambao ni watakatifu.

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; “

Kwanza ni kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako, unatubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi na kisha unajiepusha na milango kujitenga na milango hiyo sita hapo juu tuliyoiona ambayo ndio mlango ya kuingiwa na roho hizo chafu. Na roho hizo zitakuacha kabisa na utakuwa huru.

Bwana akubariki

Group la whatsapp Kwa mgawanyo bora wa masomo download App hapa>> App wingu la mashahidi

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/09/jini-mahaba-ni-nini/