Kwanini Bwana alirejea Tiro na Sidoni kwa mfano wa Sodoma?

by Admin | 25 May 2020 08:46 am05

SWALI: Kwanini Bwana Yesu aliitaja Tiro na Sidoni, kwamba kama ingeliona miujiza ile aliyoifanya kule Bethsaida ingalitubu kwa kuvaa magunia na majivu. Kwani miji hii ilikuwa ni ya namna gani, na ilifanya kosa gani?


JIBU: Tusome..

Mathayo 11:21 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo”.

Ukitazama kwa karibu utaona Bwana Yesu aliiona miji hiyo miwili (yaani Tiro na Sidoni), ilifanana na Sodoma na Gomora kwa tabia zake.

Kumbuka Sodoma na Gomora iliangamizwa kwa maovu yaliyopindukia, Vivyo hivyo Tiro na Sidoni ziliangamizwa, lakini wengi wetu hatufahamu iliangamizwaje? Na Kwa kosa gani..Na hiyo ni kutokana na kwamba habari zao hazipo wazi sana katika biblia kama vile zilivyokuwa za Sodoma na Gomora.

Jaribu kufikiria mpaka biblia inamfananisha mfalme wa Tiro na Shetani mwenyewe..Ujue kuwa ilikuwa inamwangaza shetani mwenyewe duniani kwa tabia zake..Tutakuja kuona huko mbele..

Sasa ukisoma agano la kale, utagundua kuwa mji huu ulikuwa ni mkubwa sana kibiashara hususani ule wa TIRO, Ujenzi wa Hekalu la Mfalme Sulemani kwa sehemu kubwa ulitegemea njenzo na vifaa kutoka katika nchi hizi mbili (Soma 1Nyakati 22:4)..

Hivyo enzi zile za wafalme, mataifa haya mawili yalitajirika kwa haraka sana, japokuwa mataifa kama Babeli na Ashuru yalikuwa bado yapo juu yao, lakini mataifa haya mawili yalikuwa na nguvu kubwa sana kiuchumi, ni sawa leo tuyaite CHINA, huku Babeli na Ashuru yabakie kuwa , Marekani na Urusi. Jinsi leo hii China ilivyochangamka kibiashara ndivyo ilivyokuwa miji hiyo miwili.

Sasa ukipata muda unaweza kusoma kitabu cha Ezekieli kuanzia sura ya 26 mpaka ya 28, Ujione jinsi mataifa haya yalivyosifiwa na Mungu kuwa imara kibiashara na kiuchumi, Na jinsi Mungu alivyoyatamkia maangamizo yao, siku moja, ambayo yatatelekezwa na mfalme wa Babeli Nebukadreza..

Ukisoma pale utaona inasema..

nchi hiyo kwa jinsi ilivyokuwa nzuri mpaka ikajiita “Ukamilifu wa Uzuri” hakuna wa kufananishwa nayo. Jinsi Ilivyokuwa kiini cha biashara cha mataifa yote, mpaka Nchi ya Tarshishi ile Yona aliyoikimbilia, ilitegemea kufanya biashara na Tiro, watu wasomi na wenye akili walikuwa wanaishi humo (TIRO).. kila aina ya biashara ya madini na mawe, biashara ya wanyama, na vifaa vya kivita zilifanyika humo. Biashara za nguo na urembo wa kila namna, biashara ya vyakula na matunda. walikuwa na jeshi kubwa la kutosha, mpaka wakawa wanawauzia silaha mataifa mengine.

Hiyo ndio ikampa kiburi mkuu wao mpaka afikie hatua ya kujilinganisha na Mungu, kutokana na Hekima na utajiri aliokuwa nao na fedha nyingi..Na Yezebeli Yule tunayemsoma kwenye biblia alitokea huko(Ndiye aliyemwingiza mungu baali Israeli)..Hivyo Mungu akapanga siku ya maangamizo yao..(Ezekieli 28:1-10)

Biblia inasema Wafalme wa kila mahali watatetemeza kwa jinsi anguko lake litakavyokuwa(Tiro), wakisema wewe uliyekuwa mwenye nguvu imekuaje umeanguka ghafla hivi, kirahisi,

Ezekieli 27:32 “Na katika kulia kwao watakufanyia maombolezo, na kukuombolezea, wakisema, Ni nani aliye kama Tiro, kama yeye aliyenyamazishwa kati ya bahari?

33 Bidhaa zako zilipotoka katika bahari, uliwajaza watu wa kabila nyingi; uliwatajirisha wafalme wa dunia, kwa wingi wa mali zako, na kwa utajiri wako”.

Ezekieli 26: 1 “Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika;

3 basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake.

4 Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu”.

Ukiendelea sasa kusema Ezekieli 28:11-19 utaona Mungu akitoa unabii wa shetani, na jinsi anguko lake lilivyokuwa kule mbinguni kwa kivuli hichi hichi cha mfalme wa Tiro.

Vivyo hivyo na Sidoni naye alikuwa pacha wake, soma habari iliyosalia utaona hilo. Kama vile tu Gomora alivyokuwa pacha wa Sodoma.

Sasa watu wa miji hiyo walitiwa kiburi kwa mali na fedha, wakamsahau Mungu muumba wa mbingu na nchi, wakawa wanaishi maisha ya dhambi, wanawaza tu mambo ya kidunia hadi siku moja Mungu alipoleta uharibifu wao kwa mkono wa Nebukadneza.

Lakini tunaona pale Bwana Yesu anasema.. Laiti ingeliona miujiza iliyokuwa inafanywa na yeye, basi miji hiyo miwili ambayo imefananishwa na utawala wa shetani kwa kujiinua..Watu hao wangalitubu tena kwa kuvaa nguo za magunia na majivu. Mpaka na mfalme wao angetubu.

Tengeneza picha, ni sawa na leo hii, kila mahali tunasikia shuhuda nyingi, tunaona miujiza mingi Kristo akiifanya, mpaka wafu wanafufuliwa mbele ya macho yetu lakini bado tunaupuuzia wokovu, tunaona kama ni habari za kale.

Tujiulize Je siku ile tutastahimili vipi adhabu ya hukumu?.

Ni wazi kuwa kama ziwa la moto litakuwa kali sana, basi kwa vizazi vyetu litakuwa limechochewa mara 7 zaidi,.Bwana atusaidie tusiupuuzie wokovu, Kristo alilipa gharama kubwa sana kwa ajili yetu..kwahiyo tusiudharau wokovu hata kidogo.

Bwana akubariki.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

MAHALI UNAPOPASWA USIMVUMILIE SHETANI HATA KIDOGO.

MTANGO WA YONA.

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/25/kwanini-bwana-alirejea-tiro-na-sidoni-kwa-mfano-wa-sodoma/