NIFANYE NINI PALE NINAPOSAHAU NDOTO NILIZOOTA?

NIFANYE NINI PALE NINAPOSAHAU NDOTO NILIZOOTA?

Moja la lango ambalo Mungu hulitumia sana, kutufikishia  sisi taarifa zake, ni ndoto. Na kama ni lango la Mungu basi ni vema tufahamu kuwa ibilisi hatalipenda. Hivyo atahakikisha taarifa hizo anazivuruga au hazitufikii vema, kama tu vile anavyohakikisha watu hawaliewi Neno, au mahubiri, Ndivyo anavyofanya na kwenye ndoto pia.

Taarifa zitokazo kwa Mungu zinaangukia katika makundi matatu;

  1. Tahadhari
  2. Unabii
  3. Baraka

1) Tahadhari

Hizi ni taarifa za maonyo, au hatari zinazokuja mbeleni. Mfano wa taarifa hizi ni kama zile zilizomfikia Yusufu, alipokuwa Israeli, akaambiwa akimbilie Misri, kwasababu Herode anataka kumuua mtoto, na aliporudi baadaye, akaonywa tena asikae Yerusalemu, bali aende Nazareti.

Mathayo 2:19-22

19 Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20 akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.
21 Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.
22 Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya,

Lengo la taarifa hizi ni mtu kuchukua hatua, aidha ya kivitendo au ya kimaombi.

Kwamfano Mungu anaweza kukuonyesha ajali, au msiba fulani. Hapo ujue hasaa unahitajika kuchukua hatua kimaombi kuharibu hizo roho za mauti, kwa kinywa chako.

 

Hizi ni taarifa za mambo yajayo, Yale yatakayotokea baadaye, kwenye maisha yako, huduma, familia, nchi, au taifa. Mfano wa ndoto hizi, ni kama ile ya Farao juu ya miaka saba ya shibe na njaa, (Mwanzo 41) na Nebukadreza, juu ya ile sanamu kubwa, iliyowakilisha falme nne, zitakazokuja kusimama ulimwenguni (Danieli 2).

Halikadhalika Mungu anaweza kukuonyesha, maisha yako baadaye yatakuwaje, huduma yako baadaye, itasimamaje, maono yako baadaye yatafikia wapi, anaweza kukuonyesha mambo ya siku za mwisho, matukio yajayo, kuhusu nchi, watu, familia. Hatua unayopasa kuichukua ni kuomba, na kuandaa mazingira sasa. Mfano Farao aliposaidiwa tafsiri ya ndoto yake na Yusufu, alichukua hatua ya kuweka hazina ya vyakula kwasababu njaa ilikuwa inakuja mbele. Mungu akikuonyesha huduma yako itakuwa kubwa, anza leo kujiwekea hazina ya maarifa ya Neno la Mungu, anza kutendea kazi wito wako,. Akikuonyesha unawaombea watu wengi wanapona, anza leo kuwaombea watu hata kama hawaponi, omba hivyo hivyo kila siku, usikae tu ukasubiri ije kutimia huonyeshi jitahada yoyote, akikuonyesha biashara yako imekuwa, ongeza juhudi kufanya kazi.

3) Baraka

Mungu anaweza kuachia Neno la Baraka kwako, kwamfano ukaota, ndoto njema, labda unatiwa mafuta na Kristo, au unaambiwa maneno ya mafanikio kama vile  Sulemani alipotokewa na Mungu na kuelezwa atapokea Hekima, na kuwa na mali nyingi. Uotapo ndoto ambazo ni za mafanikio kwako, uamkapo, hakikisha unazinenea kwa Imani. Unasema

“Na iwe kwangu kwa jina la Yesu Kristo”. Kama tu vile unavyobatilisha ndoto za maovu, labda mauti, vivyo hivyo hizi unazipokea kwa kinywa chako. Ni muhimu sana.

Ibrahimu aliota ndoto

Mwanzo 51:1-6

Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.
2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?
3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.
4 Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.
5 Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.
6 Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.

Sasa kinachotokea ni kwamba ndoto nyingi sana, za taarifa mbalimbali  kutoka kwa Mungu zinapotea akilini mwetu, na tunaona kawaida,

Ndoto hupotea kwa aidha namna mbili;

  • Tunakumbuka kwamba tuliota ndoto, lakini hatujui ni ndoto gani
  • Hatukumbuki kabisa kama tuliota ndoto yoyote. Lakini ipo ndoto tuliyoota

Namna mojawapo inaweza kutokea kwa mtu. Usikae ukafikiria kisa hukumbuki chochote, ukadhani hukuota ndoto yoyote. Zipo ndoto ulizoota. Hivyo ni vema ukajifunza namna ya kukabiliana na lango lako la ndoto. Ndio maana utaona wengine tukio likishatokea ndio anakumbuka kuwa alishawahi onyeshwa tukio hilo. Hiyo haitakiwi.

Nifanye nini ili nikumbuke ndoto zangu?

Njia tatu zinazoweza kumfanya mtu akumbuke ndoto.

i) Kuomba:

Kila asubuhi uamkapo, katika maombi yako, hakikisha unashika Kichwa chako, kisha unasema maneno haya

‘Baba, nafungua lango la ndoto zangu, yote uliyosema nami usiku nilipolala, ninayoyakumbuka na nisiyoyakumbuka yakawe bayana sasa kwa  kwa jina la Yesu, ndoto zilizoibiwa na ibilisi, kumbukumbu zangu, na fikra zangu zilizofutika, navirejesha vyote ndani ya ufahamu wangu sasa kwa jina la Yesu Kristo’.

Ukijifunza kuomba namna hiyo, tayari umekaribisha msaada wa Mungu, mahususi katika eneo lako la ndoto na hivyo urahisi wa kukumbuka unakuja.

ii) Utulivu (Kutafakari)

Ukishaomba, pendelea kupata utulivu, kisha tafakari kwanza Neno la Mungu. Kila asubuhi hakikisha unapata kwanza mkate wa uzima ambao ni Neno, tafakari Neno kwa muda kidogo, jiulize vifungu hivi vinamaana gani, je! Siku ya leo nitaviwekaje katika maisha yangu? Fanya tu hivyo tembea maeneo mbalimbali ya kwenye biblia, kisha tafakari tena juu ya maisha yako ya rohoni, juu ya maono yako, juu ya familia yako utajiboreshaje, baadaye juu ya ratiba zako za siku..

Katika wingi wa kutafakari, mara nyingi Mungu hurejesha ndoto zilizosahaulika, utashangaa katika tafakari Fulani hapo hapo unakumbuka kuna jambo uliota, linaloendana na tukio hilo. Ujue huo ni ujumbe wa Mungu.

Ukikosa muda wa kutosha asubuhi, Fanya hivyo muda wa usiku kabla ya kulala, Pata utulivu mwingi peke yako, Utakumbushwa ndoto nyingi.

iii) Mazungumzo

Njia nyingine ambayo humfanya Mungu arejeshe ndoto zetu kirahisi, ni katika mazungumzo, kumbuka kila eneo la maisha yako au wengine, yamkini Bwana alishawahi kusema na wewe, kwa njia ya ndoto, lakini hujui.

Kwamfano ukiwa na mwenzako, au wenzako, mnazungumza sana, Habari njema za kanisa, katika mazungumzo ya muda mrefu ikiwa lipo ambalo Bwana alikuonyesha, utaona kumbukumbu hiyo inakujia, au labda mnazungumza kwa kina Habari ya siku za mwisho, Kumbukumbu ya ndoto kama hiyo itakujia, au malengo ya maono yako.

Hivyo mazungumzo mazuri na yenye maana hurejesha fikra zilizopotea. Kwahiyo, jijengee desturi ya kuwa na mazungumzo mema.

Zingatia pia si kila ndoto hutoka kwa Mungu, ili kuweza kutofautisha ndoto za Mungu na za shetani, fungua link hii, uweze kupitia..>>>> https://wingulamashahidi.org/2019/09/03/nitajuaje-kama-ndoto-ni-ya-mungu-au-ya-shetani/

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply