KUSHURUTISHWA PIA NI SEHEMU YA HUDUMA YAKO.

KUSHURUTISHWA PIA NI SEHEMU YA HUDUMA YAKO.

Mungu anapotaka kumwinua mtu, si kila wakati atampa machaguzi fulani, au atamwagiza kiupendo, bali wakati mwingine atamshurutisha katika jambo ambalo halitaki kabisa, au hajawahi kulifanya, na hapa ndipo wengi hukimbia,

Simoni mkirene, alikuwa ni mkulima tu, akiendelea katika kazi zake za kilimo, lakini ghafla, alikamatwa na kutikwa msalaba ambao si wake,

Ni wazi kabisa hilo jambo halikumpendeza moyoni, na alionyesha ukinzani, ndio maana biblia inasema wakamshurutisha, lakini baadaye ilimbidi akubali tu, Bila kujua kuwa ndio heshima yake, ukuu wake, baraka zake zilipo.

Marko 15:21 Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.

Shuruti maana yake ni kulazimishwa, kufanya matakwa magumu ya mtu mwingine.

Hakuna mtu anayependa shuruti, kulazimishwa kutenda, mambo ambayo hujajiandaa nayo, huna mapenzi nayo, huna nguvu nayo.  Lakini fahamu kuwa kwa Mungu shuruti ni sehemu ya kukuzwa kwako kiroho,

Wakati mwingine Mungu anapoweka shuruti kwa wazazi wako, viongozi wako, wachungaji wako, Maadamu ni jema, tii tu hata kama hujisikii, ukishurutishwa kufunga na kuomba, usiseme mimi sijisikii wakati huu, fungeni nyie, ukishutishwa kutoa huduma fulani, usiseme mimi sijajiandaa,bado ni mchanga kiroho, ukishutishwa kuhudhuria darasa fulani usiwe na udhuru mwingi, ukasema nina ratiba zangu. Tii tu hata kama utaathirika kwenye mambo mengine, kwasababu Mungu huwatumia wao bila kujua, kukuinua kiroho na kihuduma.

Kama Simoni mkirene angegoma kabisa, leo hii tungemjulia wapi, lakini mpaka sasa vizazi vyote vinamjua na kumwona heri kwa kutenda tu hiyo huduma ambayo haikuwa machaguzi yake.

Watumishi wengi makanisani, wanaokuwa kihuduma ukichunguza kwa ukaribu utaona  ni wale ambao wanapopewa majukumu yaliyo nje ya mipango yao, au zaidi ya uwezo na nafasi zao, huyapokea na kuyasimamia kikamilifu bila udhuru, bila kiburi.

Kubali shuruti za Bwana.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply