JIFUNZE KUTENGA UKUAJI WA KIROHO NA KARAMA YAKO.

JIFUNZE KUTENGA UKUAJI WA KIROHO NA KARAMA YAKO.

Mtu anapookoka, vitu viwili huwa vinaanza kukua ndani yake kwa pamoja cha kwanza ni Karama, na cha pili Roho.

Lakini la kutilia maanani, ni asili ya ukuaji wao, kwasababu karama huwa inatabia ya kukua kwa haraka sana kuliko roho ya mtu.

Karama inaweza ikakua ndani ya mda mfupi sana, baada ya kuokoka, na isiwe na maandalizi mengi, Kwamfano mtu anaweza akawa amepewa karama ya unabii, karama ya uponyaji, karama ya lugha na fasiri za lugha, karama ya miujiza na vikaanza kufanya kazi kwa nguvu sana,. Sasa mahali pa kuwa makini sana ni hapo, kwasababu pale inapoonekana karama wengi hudhani ndio ishara ya ukuaji wa kiroho.

Na pengine huyu mtu anaweza kujiona amepiga hatua kubwa sana, kumbe sio. Ukuaji wa kiroho ni hatua ya taratibu sana, inayochukua safari ya muda mrefu hata miaka. Na ndivyo ambavyo Mungu amekusudia.

Haijalishi utawahi kuelewa maandiko, karama yako itatenda kazi kwa ukubwa kiasi gani, bado Mungu humtengeneza mtu taratibu, kama tu vile mwili wake unavyokuwa taratibu. Ilimchukua Musa miaka  arobaini (40), kuwa mchungaji wa Israeli aliyeaminiwa na Mungu, ilimchukua Paulo miaka kumi na nne (14) mpaka awe mtume wa kiMataifa, ilimchukua Bwana Yesu miaka thelathini (30), mpaka awe mwokozi.

Sio kwamba muda wa hapo katikati walikuwa ni wazembe sana, hawamchi Mungu, ndio maana muda ukapita mrefu hakionekani chochote kilichofanyika hapana, bali matengenezo ya mwanadamu yafanywayo na Mungu huwa yanaenda kwa hatua nyingi ambazo humchukua muda, ijapokuwa sisi tutayataka yawe kufumba na kufumbua, lakini kwa Mungu sivyo.

Je! Ni madarasa yapi ambayo mtu anapitia hapo katikati?

Nyakati za ukimya wa Mungu: Hapa Mungu anamwandaa mtu katika ukimya wake, si rahisi kusikia chochote, kuona chochote, kama ilivyokuwa mwanzo, lakini haimaanishi kuwa Mungu hayupo na mtu huyo, bali anajengewa ndani yake saburi na Imani. Usiishi tena kwa hisia au misisimko bali kwa Imani katika ahadi za Mungu. Jambo hili linaweza kumchukua mamiezi hata miaka.

Nyakati za mafunzo: Hapa Mungu anamweka chini ya waalimu, kumfundisha, ni wakati wa kulishwa Neno, na kupokea maarifa mengi, na uzoefu wa kiroho, kwa waliomtangulia. Kama Kristo alivyokaa chini ya waalimu akiwasilikiliza, akiwatazama, na kuwauliza maswali (Luka 2:46). Vivyo hivyo huyu naye ni lazima tu atapitishwa chini ya watu kumfundisha, na akikwepa darasa hili, hatoona maendeleo yoyote ndani yake.

Nyakati hizi, huambatana na kusikiliza mahubiri, kusoma vitabu, kuwauliza maswali, kuhudhuria semina na vipindi vingi vya mafundisho.

Nyakati za utulivu na kutengwa: Hizi ni nyakati ambazo Mungu atakutenga mbali na ulimwengu, au kukupunguzia mahangaiko, ili upate muda mwingi wa kuomba na kufunga na kujisomea Neno peke yako. Nyakati hizi wengine hata watafute kazi vipi hawapati, ukiona hivyo tumia muda huo kumkaribia Bwana, kwasababu Mungu anakufundisha kujenga mahusiano yako binafsi na yeye. Ili uielewe sauti ya Mungu.

Nyakati za Kunyenyekezwa: Hapa Mungu atakuacha uwe kwenye uhitaji/ utegemezi fulani, atamwagiza kunguru (ndege mchafu), akuhudumie kama ilivyokuwa kwa Eliya, sio kwamba ameshindwa kukuletea mtu mwema, au kukupa tu yeye mwenyewe, hapana, anaweza mtumia yule usiyempenda, usiyemtarajia kukuhudumia eneo fulani, lengo akufundishe unyenyekevu wake, na upendo usio na sharti. Ikiwa mtu atakwepa darasa hili, anaukwepa unyenyekevu wa Mungu.

Nyakati za Majaribio: Ibrahimu alipitishwa kwenye majaribio, lengo sio kuangamizwa, bali kuhakikiwa imani yake, , ijapokuwa Ibrahimu alishinda katika mengi ikiwemo kumtoa mwanawe sadaka, lakini alishindwa kwa kusikiliza sauti ya mkewe Sara akazaa na kijakazi wake. Ni kuonyesha kuwa lile utakaloshindwa lisiwe sababu ya wewe kudhani kuwa Mungu amekutupa, lengo, jirekebishe, jifunze kutokana na makosa, ili uwe mkamilifu. Ibrahimu aliposhindwa kwa Sara Mungu alimwambia uwe mkamilifu mbele zangu (Mwanzo 17:1). Kipindi hichi ni kufanywa mkamilifu.

Nyakati za huduma: Hapa Bwana atakujaribu kwa lililo dogo, atakuweka katika utumishi wake, uwahudumie wengine, hapa anapima uaminifu wako. Je! Utatenda kwa uaminifu? Ndicho alichokifanya kwa mitume wake (Mathayo 10), alipowatuma wawili wawili, kabla ya huduma kamili kuja juu yao siku ya pentekoste.

Wito kamili: Hapa Mungu amekuhakiki na kukuthibitisha, kuwa chombo chake kiteule. Ndipo anapokutumia jinsi apendavyo, yawe kwa makubwa au madogo, Hapa ni rahisi kuona mema mengi sana ya Mungu, katika maeneo mbalimbali ya rohoni.

La kufahamu tu, hatua hizi zinaweza kuingiliana, yaani ukapitishwa tatu, au nne, kwa wakati mmoja, na huweza jirudia rudia, mzunguko ukawa huo huo kwa kipindi kirefu.

Lakini mwisho wa mnyororo huo , utaona mwisho wa madarasa hayo Umefundishwa;

Saburi, Imani, maarifa, Kiasi Uaminifu, ukamilifu (utauwa), upendo

Ambavyo vinaenda sambamba kabisa na lile Mtume Petro aliloliandika kwa uweza wa Roho katika..

( 2Petro 1:5-11)

5 Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,
6 na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,
7 na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.
8 Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.
11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Hivyo ikiwa umemwamini kweli Kristo, na kumfuata, basi fahamu kuwa lengo kubwa na Mungu ni wewe  ufikie ukuaji bora wa kiroho, jitahidi kutembea kikamilifu kwenye madarasa yake ambayo huchukua muda,  lakini mwisho wake ni TAJI LA UZIMA lisilonyauka, kwa kufuzu madarasa ya Mungu.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply