VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 8 (Kitabu cha Ezekieli)

by Admin | 3 August 2020 08:46 pm08

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Biblia. Huu ni mwendelezo wa vitabu vya biblia ambao tumeshatazama vitabu 17 vya mwanzo..Ikiwemo kitabu cha Ezra na Yeremia. Hivyo leo kwa Neema za Bwana tutaendelea na kitabu kimoja mbele ambacho ni kitabu cha Ezekieli. Kama hujapitia vitabu vya nyuma nakushauri ukavipitia kwanza wewe binafsi taratibu na kwa utulivu, ili hapa iwe ni sehemu ya kujiongezea vitu vichache juu ya vile ambavyo unavifahamu.

Kitabu cha Ezekieli ni kitabu cha 26 katika orodha ya vitabu vya Biblia na kina sura 48. Mwandishi wa kitabu hichi ni Ezekieli mwenyewe…na tafsiri ya jina Ezekieli ni “Mungu atatia nguvu”. Kitabu hichi kinakadiriwa kuandikwa kati ya mwaka 593-570 KK. Kiliandikwa kwa miaka isiyopungua 20. Na kilianzwa kuandikwa wakati wa lile kundi la pili la wayahudi kupelekwa Babeli.

Kumbuka hatuna za kupelekwa Babeli kwa wana wa Israeli ziligawanyika katika makundi matatu.

  1. Kundi la kwanza: ndio lile lililokuwa chini ya Mfalme, Yehoyakimu, ambalo Danieli alikuwa miongoni mwao.
  2. Kundi la Pili: lilikuwa chini ya huyu Mfalme Yekonia/Yehoyakini, ambapo Nabii Ezekieli ndio alikuwa ndani ya kundi hili.
  3. Na kundi la tatu Na la mwisho: lilikuwa ni la mfalme Sedekia, ambaye huyu alionyesha kiburi kwa Nebukadneza ikamfanya mpaka atobolewe macho, na kusababibishia kundi kubwa sana la wa-Yuda kuchukuliwa utumwani. Na ndio ikawa mwisho wa Wayahudi kuwepo katika nchi yao ya Ahadi. 

Sasa ukisoma vitabu vya nyuma vya Mambo ya nyakati na Wafalme, na kitabu cha Yeremia utaona ni jinsi gani Nabii Yeremia alivyowalilia wana wa Israeli juu ya kuamishwa kwao, lakini hawakusikia mpaka walipotolewa wote kwenye nchi ya ahadi na kupelekwa Babeli.

Sasa wakina Danieli, Shedraka, Meshaki na Abednego walichukuliwa wakiwa vijana wadogo sana katika kundi la kwanza na kutangulia Babeli..Tutakuja kuona Habari zao vizuri katika mfululizo wetu  baada ya kitabu hichi. Lakini kipindi kifupi tu baada ya wao kufika Babeli likatolewa kundi lingine la pili ambalo ndilo Ezekieli alikuwepo ndani yake. Wakiwa njiani kuelekea Babeli kijana mdogo Ezekieli alianza kuona maono. Hatuwezi kuyaandika haya maono yote aliyoyaona hapa (unaweza kuyasoma binafsi katika kitabu hicho cha Ezekieli 1 na 2).

Lakini kwa ufupi tu ni kwamba aliona Mbingu zimefunguka kama Nabii Isaya na Mtume Yohana walivyoona, na akaona makerubi na kiti cha enzi cha Mungu.

Ezekieli 1:1“Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu”.

Akiwa katika maono hayo Mungu alimpa “gombo” alile (Ezekieli 2:9).. Na gombo lile lilikuwa limeandikwa nje na ndani. Sasa tafsiri ya gombo hapo sio kitu Fulani mfano wa chakula, hapana bali ni aina Fulani ya vitabu vya kale ambavyo vinaandikwa kwa kuviringishwa. Hivyo ni kitabu ndicho alichopewa akile, na sio chakula..Sasa utauliza alikulaje kulaje kitabu?..Hatujui!..kama kiligeuka na kuwa mkate hilo hatujui..lakini mwisho  ni kwamba tunajua alikula kile kitabu alichopewa.

Na kile kitabu kilikuwa kimendikwa maneno nje na ndani.. Na maneno yalioandikwa humo yalikuwa yanahusiana na MAOMBOLEZO, VILIO NA OLE.

Sasa Huduma/ kusudi la Mungu kumwita Ezekieli lilikuwa ni lipi?

Tusome kidogo mistari ifuatayo ndipo tutajua Zaidi..

Ezekieli 3:1 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.

 2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.

 3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. 

4 Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu. 

5 Maana wewe hukutumwa kwa watu wa maneno mageni, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;

  6 si kwa watu wa kabila nyingi wenye maneno mageni, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza”

Umeona hapo? Ezekieli alitumwa  kwa watu wa Israeli…Hususani kwa lile kundi la mwisho..ambalo bado limebaki nyuma, halijafika bado Babeli..Kile kitabu alicholishwa ni lugha ya rohoni inayofunua KULISHWA MANENO YA MUNGU,  Na maneno hayo ni  Kuwaonya (yaani OLE), kuwaombolezea kwa yatakayowapata wasipotubu, na kuwatabiria vilio vitakavyowakuta kipindi kifupi kama hawatatubu.

Baada tu ya kula hicho kitabu katika maono…Roho ya Mungu ilimshukia kwa nguvu na kuanza kuwatabiria wana wa Israeli yatakayowakuta. Wakati huo Sedekia akiwa mfalme wa waisraeli, alikuwa ni mbishi na mwenye kiburi, hakutaka kuamini kwamba atachukuliwa utumwani kwenda Babeli, Nabii Yeremia alikuwa bado yupo hai kipindi hicho na alikuwa anamwonya aache njia zake mbaya na ajinyenyekeze, lakini hakusikia…Ikiwa bado imesalia miaka michache Mji wote uchomwe moto Ezekieli naye huko anaona maono na maneno kama yale yale ya Yeremia ya kuwaonya juu ya hukumu ile ile. Kwa hiyo huko Israeli yupo Yeremia na huku njiani kuelekea Babeli yupo Ezekieli..Wote wanazungumza kitu kimoja!.

Hivyo kuanzia Sura ya 1 hadi ya 24 ya kitabu cha Ezekieli.. Inaelezea Unabii juu ya kuangamizwa kwa Yerusalemu, kwa lile kundi lililobakia. Na maono hayo yalikuja kutimia vile vile kama alivyosema.

Baada ya Yerusalemu kuteketezwa na hilo kundi la tatu kufikishwa utumwani, Bwana alianza kumpa Ezekieli maono mengine..juu ya mataifa mengine yaliyobaki kama Misri na mengine yaliyo kando kando, kwamba nayo pia yatachukuliwa utumwani kwenda Babeli. Jambo ambalo Nabii Yeremia pia alilitabiri.

Hivyo kuanzia Sura ya 25-32. Bwana anampa Ezekieli maono juu ya kuangamizwa kwa mataifa mengine yaliyosalia, kwani nayo pia yalikuwa yamemwasi Mungu.

Na baada ya mataifa hayo yote kupitia kile yalichokipitia Israeli (yaani yote kuangamizwa na watu wao kupelekwa utumwani Babeli). Bwana akaanza kumpa Ezekieli tena maono mengine ya kuwaonya Wana wa Israeli watubu sana.. kwasababu anawazia kuwafanyia mema mwishoni. Katika Sura ya 33 utaona wito huo Mungu anaowaita wana wa Israeli.

Na mwisho kabisa baada ya wito huo kuanzia Sura ya 34-48. Bwana anampa Ezekieli maono mengine ya mwisho kabisa…Maono ni juu ya  kujengwa upya Yerusalemu katika siku za mwisho..Na baadhi ya maono hayo bado hayajatimia mpaka sasa…kwani kuna Hekalu la Tatu la mwisho ambalo limezungumziwa humo kwamba litatengenezwa siku za mwisho bado halijatimia…Ingawa mpaka sasa vifaa vyote vya ujenzi vipo tayari, vinasubiriwa nyakati na majira tu yaliyoamriwa na mbingu…ambapo siku moja isiyokuwa na jina Hekalu litaanza kujengwa kwa haraka sana na kwa kipindi kifupi kutimiza huo unabii wa Ezekieli.

Hivyo huo ndio ufupisho wa kitabu cha Ezekieli ..(katika Sura hizo zote zimejaa, maonyo mengi sana, na tabiri nyingi sana zihusuzo siku za mwisho, na ole nyingi na maombolezo),  na ole nyingine zinatuhusu hata sisi!..Ndani yake Bwana aliwaonya manabii wote wa Uongo vikali, na kuwalaani….kwamfano hebu soma ole hii..

Ezekieli 13:1 “Kisha neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana; 

3 Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!”

Unaona, yapo mafunzo mengi na maonyo, ambayo Roho Mtakatifu anatamani kumfunulia kila mtu atakayekisoma kitabu hiki. (Ndani ya kitabu cha Ezekieli utajifunza ni jinsi gani Mungu hapendi ibada za sanamu, utajifunza ni jinsi gani Mungu hapendezwi na maovu, na kusema kila nafsi itendayo dhambi itakufa! Kasome Eze.18:4,18:20). Pia ndani ya kitabu hichi utajifunza madhara ya kutokuifanya kazi ya Mungu, maana yake ni kwamba Mungu anapokuambia kitu ili ukawaonye watu na wewe hutaki kwenda kuwaonya basi wakifa katika dhambi zao bila wewe kuwaonya, damu yao itakuwa juu yako.

Ezekieli 33:7 “Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu. 

8 Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. 

9 Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako”.

Hivyo sio kufurahia kusikia tu…bali tunaposikia injili au maonyo ya Mungu yanageuka kuwa deni kwetu kwenda kuwaonya wengine. Ndio maana Ezekieli baada ya kula lile gombo, kinywa aliliona litamu lakini tumboni lichungu..

Ndani ya kitabu hichi, utajifunza juu ya vita kubwa ambayo itakuja kupigwana pale Israeli, ambapo mataifa yanayoizunguka nchi ile yataongozwa na nchi ya magogu (Urusi kwa sasa),ili kupigana nao, Vita hiyo Israeli itashinda, pengine mimi na wewe tunaweza kuishuhudia vita hiyo katika kizazi chetu.

Hivyo tenga muda wa kukisoma chote wewe binafsi, usiridhike na haya yaliyoandikwa  hapa, na kujitumainisha kwamba tayari umeshakielewa! Huu ni muhtasari tu wa kukupa dira!,..kila kitu kipo kule!..

Biblia haijaeleza kifo cha Ezekieli, lakini ni wazi kuwa alifia huko huko Babeli..Na sehemu kubwa ya maono yake inafanana na maono aliyoyaona Mtume Yohana katika kisiwa cha Patmo..tutakapofika kitabu cha Ufunuo wa Yohana, tutaelewa Zaidi.

Mwisho kabisa…Kumbuka hizi ni siku za mwisho!..tunaishi katika kanisa la Mwisho lijulikanalo kama kanisa la Laodikia…Kanisa la Laodikia sio dhehebu linaloitwa Laodikia, au shirika Fulani la dini hapana!…Bali ni hali ya kanisa ya dunia nzima inavyoonekana mbele za Mungu, kwamba inafananishwa na kanisa la saba kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Ufunuo 3:14. Ni kanisa vuguvugu, ambalo Kristo alisema atalitapika. Na hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili. Hivyo Kristo anatuita kwasababu ule mwisho umekaribia, na hataki hata mmoja wetu apotee.

Hivyo kama hujaokoka kikamilifu, kama hujaacha ya ulimwengu..kama ni mwasherati bado, kama ni mzinzi, kama ni mtazamaji wa pornography kama ni mtukanaji, tubu leo..kwasababu wokovu ni bure, na atakusamehe na kukutengeneza upya. Na kusudia kuacha yote mabaya unayoyafanya na Bwana atakupa Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote.

Bwana akubariki.

Kama utahitaji uchambuzi wa vitabu vya nyuma basi utatumia ujumbe inbox. Kitabu kitakachofuata kitakuwa ni kitabu cha Danieli hivyo usikose mwendelezo.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

DANIELI: Mlango wa 1

Je! Ni ipi tarehe sahihi Evil-merodaki alimtoa Yekonia gerezani?

UFUFUO TUNAOUSUBIRIA UTAHITIMISHA YOTE.

 

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Wafilisti ni watu gani.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/03/vitabu-vya-biblia-sehemu-ya-8-kitabu-cha-ezekieli/