Mtu mwenye “kitango” ni mtu wa namna gani kibiblia?

by Admin | 19 December 2020 08:46 pm12

Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi;

Mithali 20:13 “Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

Mithali 20:19 “Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana”.

Mtu mwenye kitango kwa lugha ya sasa ambayo ni rahisi kueleweka na watu wengi ni mtu  “MMBEA”. Yaani mtu ambaye hawezi kusitiri jambo, yupo tayari kukizungumza kila kitu anachokisikia au kukiona kwa watu wengine.

Kwamfano utakuta mtu labda kakaribishwa nyumbani kwa jirani yake au ndugu yake wa mbali, ili akae au aishi tu pale kwa muda, sasa katika kuishi kwake akaona mapungufu fulani fulani ndani ya nyumba ile, ambayo hata wenye nyumba wenyewe hawakuona vema, kuyatangaza, lakini utakuta  yeye anatoka pale na kuanza kufichua siri za nyumba hiyo kwa watu wengine, bila hata kujali utu, wale wapo hivi, wapo vile, yule mwanaume kumbe yupo hivi au vile n.k… Sasa mtu kama huyo ni mtu mwenye kitango ambaye biblia imetuonya, tusishirikane naye.

Mwingine ataelezwa jambo la siri na rafiki yake pengine labda ugonjwa fulani usiotibika, na akaombwa sana asimwambie mtu yeyote iwe siri yake, lakini yeye anatoka pale, anaanza kutangaza mtaa mzima yule fulani ana hiki au kile, mpaka habari inamrudia yule mwenyewe muhusika. Sasa watu wa namna hiyo ni hatari sana, hatupaswi kushirikiana nao, kwasababu hata kwa namna ya kawaida ikiwa anaweza kufichua siri za watu wengine kwako, ni wazi  kuwa hata za kwako ameshawahi kuzifichua kwa watu wengine. Hivyo ukishakutana na watu kama hawa usijaribu kuwaeleza mambo yako ya siri, wala usikubali kusikiliza wanachokuambia.

Mara nyingi tunaziharibu siku zetu mapema kabisa kunapopambazuka, kwa midomo yetu wenyewe, biblia inasema;

1Petro 3:10 “Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, NA KUONA SIKU NJEMA, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila”.

Ukitaka ufurahie maisha, jifunze,kuudhibiti ulimi wako, ukitaka siku yako ibarikiwe tangu asubuhi mpaka jioni, jifunze kuutawala mdomo wako, sio kila jambo unaloliona au unalolisikia ni la kutangaza kwa watu , jifunze kutunza siri za watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo sio tu siku yako itakuwa ni nzuri, lakini pia utakuwa unampendeza Mungu, Kwasababu Mungu naye hachukui mambo yetu ya siri na kwenda kuyatangaza kwa watu ovyo ovyo, japokuwa anajua mambo yetu wote ya siri tunayoyafanya.

Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

JIHADHARI NA DHAMBI YA WIVU/HUSUDA.

Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Tofauti kati ya lijamu na hatamu ni ipi kibiblia?

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/19/mtu-mwenye-kitango-ni-mtu-wa-namna-gani-kibiblia/