UPANDE WA UKUAJI WA KIROHO, ULIOSAHAULIKA

UPANDE WA UKUAJI WA KIROHO, ULIOSAHAULIKA

Ni maswali mengi yanaulizwa na watakatifu,  mbona ninajuhudi sana,  ninahudhuria vipindi vingi vya mafundisho,  mifungo na maombi, semina na mikutano, na makambi makubwa ya ujazo wa Roho Mtakatifu,  ninapokea nguvu, Mungu anatenda makubwa, lakini najiona moyoni bado  sina ukuaji mzuri wa kiroho?

Kwanini, sababu ni nini?

Tukisoma maandiko tunaona kuna upande ambao, tunausahau kuutilia msisitizo katika kumjua Kristo, na pengine hauhubiriwi sana madhabahuni, lakini ni muhim

Upande huo mtume Paulo aliusema katika kitabu cha Wafilipi,

Wafilipi 3:10 ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na USHIRIKA WA MATESO YAKE, nikifananishwa na kufa kwake;

Zingatia hapo, anataja mambo mawili anasema, ili nimjue yeye na uweza wa kufufuka kwake,

Lakini pia..

Na ushirika wa mateso yake.

Watu wanatazama sana, eneo la kwanza, ambalo ni uweza wa kufufuka kwake, yaani wanatafuta nguvu za Mungu kwa juhudu kubwa, miujiza, uponyaji,baraka, unabii, ujazo wa Roho Mtakatifu, jambo ambalo ni zuri sana, na linapaswa litafutwe, lakini, bado mtu huyu kwa bahati mbaya anaweza asikamilike kama hatataka na sehemu ya pili pia ya kumjua Kristo, ambayo ni ‘ushirika wa mateso yake’.

Paulo alifanya miujiza lakini alifungwa pia kwa ajili ya hiyo, aliponya watu lakini alipigwa mawe, alifanya makubwa lakini bado alitukanwa, na kufanyiwa visa.

Ukuaji mzuri wa kiroho, hautazamii tu, kupokea nguvu za Mungu, unatazama pia Ushirika wa mateso yake.

Tunataka tumjue Kristo, lakini hatutaki kuudhiwa kwa gharama tuliziongia kwa ajili yake, Yesu alisema tutapata mara mia kweli, lakini pia tutapata na udhia (Marko 10:30).

Ndege hawezi kuruka kwa bawa moja, ni lazima yote mawili yafanye kazi, Tukimtaka Mungu kwa nguvu zake, tu lakini hatumtaki na mateso yake, bado maendeleo hayatakuwa makubwa. Haijalishwi tutajazwa Roho kiasi gani.

Ushirika wa mateso ni pamoja na kukubali kuchukiwa kwa ajili ya jina lake, kutengwa kwasababu ya misimamo yako ya kiroho, kumbuka gharama ya Danieli kupendwa ni pamoja na kukubali kutupwa kwenye tundu la simba, Yusufu kuwa mkuu ni pamoja na kuuzwa na ndugu zake kwasababu ya misimamo yake, Ayubu kuitwa mcha Mungu ni pamoja na majaribu aliyoyastahimili. Huo ndio ushirika wa mateso yake.

Usifurahie tu, kuona nguvu za Mungu, jiulize binafsi ni wapi nimeshiriki mateso ya Kristo, kwa kuzikubali gharama?  Palipo na gharama na umakini wa kiroho, ushirika wa mateso ni lazima utaambatana nawe.

Tukue kiroho.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply