Yohana 2:13 ‘’Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.
14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.
15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;
16 akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.
17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila.
18 Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? 19 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.
20 Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?
21 Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.
22 Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.’’
Tukisoma
kisa hichi ni rahisi kuwahukumu Makuhani na Mafarisayo na Wayahudi kuwa
walikuwa watu wasiofikiri…watu wanaoona miujiza lakini hawaamini…ni
kweli kuna mambo ya kulaumiwa lakini si yote…. hebu leo kwa sehemu
tuchunguze kama ni kweli walikuwa hawafikiri wakati wote..
Jaribu
kuchukua mfano wewe ni mtumishi wa Serikali, labda unatumika kwenye
shirika fulani la Umma..halafu siku moja anatokea mtu usiyemjua anaingia
mahali mnapofanyia kazi na kuanza kuvuruga vuruga nyaraka na hati
muhimu..huku anawapazia sauti na kuwaambia…msigeuze serikali ya Raisi
wangu kuwa pango la mafisadi….na mnapojaribu kumzuia na kumwuliza yeye
ni nani na nani kamtuma kufanya vile, anawajibu…jiuzuluni wote na
mwachie ngazi leo na baada ya siku tatu nitalinyanyua hili shirika upya.
Unafikiri
ni kitu gani..kitagonga kwenye akili…Moja kwa moja aidha utajua huyo
mtu karukwa na akili..Na pili jambo litakalofuata ni kutafuta njia ya
kwenda kumshitaki haraka…Kwasababu anakuja kuharibu kazi na kuzungumza
vitu visivyoeleweka…eti atalinyanyua shirika ndani ya siku
tatu!!…Shirika hili mpaka kulifikisha hapa tumetumia miaka Zaidi ya 20
wewe unataka kulinyanyua ndani ya siku tatu!..
Hebu
fikiria huyo mtu hata akienda mahakamani atashindaje kesi?..kwasababu
amesikiwa na watu wote kwa kinywa chake akisema atalinyanyua shirika kwa
siku tatu.
Na
ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu mahali Fulani, alipowakuta wayahudi
wanafanya biashara kule Hekaluni,aliwaambia wasigeuze nyumba ya Baba
yake kuwa pango la wanyang’anyi lakini walipomuhoji kwa ishara gani
unafanya haya? Akawaambia libomoeni hekalu hili na ndani ya siku tatu
nitalisimamisha.
Sasa
wayahudi walidhani wamemsikia vizuri na kumwelewa…kumbe hawajamwelewa
ingawa wamemsikia,..ndio maana Neno linasema ‘kusikia mtasikia lakini
hamtaelewa..Kutazama mtatazama lakini hamtaona (Mathayo 13:14)’…Walidhani
hekalu litakalobomolewa na kusimamishwa ndani ya siku tatu ni hilo la
mawe wanaloliona mbele yao..kumbe kulikuwa na hekalu lingine ambalo
lilikuwa ni mwili wa Bwana Yesu.
Na waliendelea na huo upofu mpaka siku ya mwisho, pale walipomsulibisha
Walisema maneno haya:
Mathayo
27:40 ‘’Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe
nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani’’.
Lakini
tunaona waliokuja kumwelewa ni wanafanzi wake tu! Tena dakika za
mwisho, Wale waliokuwa wanatembea naye kila siku. Ndio waliopewa neema
ya kumwelewa Bwana Yesu alikuwa anamaanisha nini katika maneno yake. Sio
kila mtu tu alikuwa anamwelewa Bwana Yesu.
Ndugu
huo upofu mpaka leo upo! Unaendelea kwa watu wengi wasio wanafunzi wa
Yesu Kristo..Bwana hana wanafunzi 12..alianza na wanafunzi 12, lakini
sasa anao wanafunzi wengi…Na hao ndio anaowafunua macho ya kuyaelewa
maneno yake…wengine walio nje maneno ya Yesu yatakuwa ni mafumbo
kwao…wataona wanamwelewa sana Bwana Yesu lakini kumbe hawamwelewi..
Watadhani
kwasababu Bwana aliyageuza maji kuwa divai basi alihalalisha unywaji wa
pombe, lakini hawaelewi kuwa Pia kitendo cha Bwana kula na makahaba na
wenye dhambi lengo lake halikuwa kuhalalalisha ukahaba wao wala dhambi
zao…Alifanya vile ili kutafuta njia ya kuwavuta watubu kwa upendo
wake….Na watu walipomwita kuwa mlevi haikumaanisha kuwa yeye kweli ni
mlevi..wewe unaweza kuitwa mlevi na maadui zako lakini isiwe ni mlevi
kweli…kadhalika walipomwita yeye ni mlafi haikumaanisha Bwana Yesu
alikuwa ni mlafi kweli…
Alipomwita
Herode Mbweha!..hakumaanisha kumtukana!!…ingekuwa ndio hivyo, basi yeye
mwenyewe amejitukana sana…alipokuwa anajiita mwanakondoo?..au
anapowafananisha watu wake na kondoo..kwa wale wafugaji wanaelewa ni
afadhali mtu akuite mbwa kuliko kondoo.
Kadhalika
aliposema mkawabatize watu wote kwa jina la Baba, na Mwana na Roho
Mtakatifu hakumaanisha hivyo vyeo bali alimaanisha ni jina moja ambalo
ndio la Baba, na ndio hilo hilo la Mwana na ndio hilo hilo la Roho
Mtakatifu na hilo sio lingine Zaidi ya Jina la YESU (Matendo 2:38).
Na
aliposema…’’aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa
milele’’..hakumaanisha tukamkamate na kumchinjwa na kunywa damu yake
kama simba…bali alimaanisha kuula katika roho na kuinywa damu yake
katika roho..Na chakula cha Roho zetu ni Maneno tunayosikia…Yakiwa ni
Maneno ya Mungu, basi ni chakula bora cha uzima wa milele, na yakiwa
maneno ya yule mwovu basi ni chakula kisichofaa cha mauti.
Kwahiyo
Biblia inatufundisha tuwe na masikio yanayosikia, na macho
yanayoona..ili kwamba tunaposoma Biblia tuielewe…Na hayo tutayapata kwa
kuwa wanafunzi wa Yesu tu!..kwasababu hao ndio Bwana alikuwa anawapa
kuelewa maneno yake…
Na vigezo vya kuwa mwanafunzi ni hivi..
Luka 14:25 ‘’Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
27 MTU YE YOTE ASIYEUCHUKUA MSALABA WAKE NA KUJA NYUMA YANGU, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.
31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?
32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.
33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu’’.
Je!
Umeuchukua msalaba wako?..je! umewachukia ndugu zako, baba yako na mama
yako?…kuchukia kunakozungumziwa hapo sio kuchukia mtu kwa hasira au
chuki ya moyo…hapana! Bali ni kitendo cha kuyakataa na kuyachukia
maamuzi ya wazazi wako au ndugu zako yanayopingana na mapenzi ya Mungu
kwako, na kuamua kuyafuata yale mapenzi ya Mungu tu!..Huko ndio
kuwachukia kunakozungumziwa hapo juu!!…kama baba yako ni mlevi na
anakutaka na wewe uwe kama yeye…hapo unayachukia hayo maamuzi na kusema
hapana!..kama ni msengenyaji hivyo hivyo..kama ni mlarushwa na wewe
anataka uwe kama yeye unasema No! kama ni mchawi au Mwenda kwa
waganga..na anataka kukufundisha na wewe uwe kama yeye..hapo unasema
hapana! N.k.
Na
pia ili uwe mwanafunzi biblia inasema unapiga gharama!! Ukristo sio
jambo la kujaribu na kutoka! Biblia inasema utachekwa….Ukiamua kumfuata
Bwana Yesu, hesabu kuwa kuna kuonekana mpumbavu, kuonekana
mshamba…wakati mwingine kuonekana umerukwa na akili…Na pia ukristo sio
mteremko muda wote…piga hesabu kuwa kuna wakati Bwana anaweza kukuacha
kwa kipindi Fulani kirefu pasipo kuzungumza na wewe kwa njia unayotaka!
Je! Utaendelea kuwa naye!…utakapopitia shida, dhiki na wakati mwingine
misiba utamwacha?
Pia piga gharama! Je asipokupa vile vitu unavyohitaji! Utaendelea kuwa naye?.
Na
mwisho anasema ‘mtu yeyote asiyeacha vyote alivyo navyo hawezi kuwa
mwanafunzi wangu’..Kuacha vyote ulivyonavyo ni mfano wa wakina
Petro…waliacha vyote walivyo navyo na kumfuata Bwana…Kuacha vyote ulivyo
navyo sio lazima kwenda kuuza mali zako au hazina yako…bali ni kuishi
kana kwamba hivyo vitu sio vya kwako…kiasi kwamba hata ikitokea
kimepotea hakipo kwenye akili yako…umeshakiacha siku nyingi…akili yako
imetawaliwa na kutenda mapenzi ya Mungu na kuyaishi…hakina chochote
katika moyo wako…kiwepo au kisiwepo vyote kwako ni sawa sawa tu.
Ukishapiga
hizo gharama, na kujitwika msalaba wako, biblia inasema umekuwa
mwanafunzi wake…ambao wamepewa Neema ya kuzijua siri za ufalme wa
mbinguni…
Hivyo
kama hujampa Kristo Yesu Maisha yako, ni vizuri ukafanya hivyo leo… Na
ili uwe mwanafunzi wake piga gharama za kumfuata…na Bwana akusaidie
katika hilo.
Mungu akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Print this post