Title November 2018

MNGOJEE BWANA

KUNGOJA maana yake ni kukaa katika hali ile ile huku ukisubiria kitu ulichokuwa unakitarajia kifike mara, na tunajua kwa namna ya kibinadamu, kungojea kitu Fulani kwa muda mrefu huwa kunachosha, kwamfano leo mtu akitumia saa moja kwenye kufanya shughuli fulani labda tuseme kupika au kufua, na akitumia saa hilo hilo moja katika kumngojea rafiki yake kituoni kwa namna ya kawaida yule mtu ataona ule muda aliotumia kumgojea rafiki yake kituoni umekuwa mrefu zaidi kuliko ule muda ambao alikuwa anapika. Ni kwasababu gani? Ni kwasababu alipokuwa kituoni, hakuwa anajishughulisha na jambo lingine lolote isipokuwa kumtarajia rafiki yake tu. Muda wake mwingi haukupotea katika migawanyo ya shughuli nyingi bali katika jambo moja tu, hivyo muda ukaonekana kuwa mrefu zaidi.


Kadhalika sisi tunapokuwa watoto wa Mungu kwa kuzaliwa mara ya pili [yaani kwa kubatizwa kwa maji na kwa Roho] Mungu analigeuza tumaini letu na tegemeo letu lote kuanzia huo wakati na kuendelea tunakuwa tunamtazamia yeye.

Biblia inasema Luka 12.36 ”nanyi IWENI KAMA WATU WANAOMNGOJEA BWANA WAO, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara”.

Hivyo kukaa huku katika hali ya kungojea kutaingia ndani ya kila mkristo halisi aliyezaliwa mara ya pili, tumaini lake likiwa ni kukamilishwa kwanza hapa duniani, pili akamilishwe katika siku ya UNYAKUO. Hivyo hatuna budi kungojea kwa saburi nyingi na kujizuia na mambo mengi. Lakini biblia inasema katika.

Isaya 40: 29 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;

31 BALI WAO WAMNGOJEAO BWANA WATAPATA NGUVU MPYA; WATAPANDA JUU KWA MBAWA KAMA TAI; WATAPIGA MBIO, WALA HAWATACHOKA; WATAKWENDA KWA MIGUU, WALA HAWATAZIMIA”.

Unaona hapo, wote watumainio nguvu zao ziwasaidie katika maisha yao, watumainiao mambo yao wenyewe yawafikishe katika malengo yao, wote wanaodharau rehema za Bwana,na wokovu wake, wanaosema tangu umekuwa mkristo umepata faida gani, wote wanaosema huyo YESU mnayemngojea yupo wapi? Angalia sisi tumeshapiga hatua kubwa tuna hiki na kile, tuna maendeleo na mafanikio lakini ninyi mnaomtaja YESU mbona haji huo wokovu mnaousubiria miaka 2000 upo wapi? Huo utawala wa YESU mnaousubiria upo wapi? Huyo Yesu ameshakufa, na miaka hiyo yote hajawafaidia kitu.

Unaona hao wote wanaosema hivyo biblia inasema wao watachoka, watazimia na kuanguka, japo watajifariji kwa nguvu zao za sasa lakini ni kwa kitambo tu ipo siku watachoka tu, siku moja wataona na wengine walishaona tayari kwamba vitu wanavyovitumaini siku zote haviwapi uzima wa milele, wanaanza kuona mbona hivi vitu tulivyoviwekea matumaini na kuvitaabikia na kuvingojea havitupi furaha ya kudumu?, Biblia inasema watazimia wote bali wale WAMNGOJEAO BWANA WATAPATA NGUVU MPYA, watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia. Haleluya.

Hatushangai kuona Ulimwengu ulishangaa kipindi cha mitume na bado utaendelea kushangaa wakati wa sasa ni kwanini hawa watu hawakati tamaa kwa hicho wanachokingojea?. Hawajui Ni kwasababu sio kwa uweza wao wapo vile, bali ni kwasababu ya NGUVU wanazozipata kutoka kwa yeye WANAYEMNGOJEA.

Lakini mtu anayemngojea Bwana ni mtu wa namna gani? Ni mtu yule aliyeweka tumaini lake lote kwa Mungu, na kama vile tunavyosema kungojea ni kusubiria kwa uvumilivu na kusubiria huko kunakugharimu kuacha kufanya shughuli nyingine na  kukitazama hicho kitu, vivyo hivyo na mtu yule anayesema anamngojea Mungu ni yule aliyejitenga na ulimwengu, aliyeamua kutokumchanganya Mungu na dunia, aliyesema tangu sasa, ulevi basi, zinaa basi, fashion basi, uchawi basi, wizi basi, usengenyaji basi, pornography basi, kampani mbovu basi, aliyesema tangu sasa namwishia Mungu katika mwenendo wangu wote, tangu sasa nautafuta utakatifu na weupe wa moyo, tangu sasa naanza mwanzo mpya na Bwana..Sasa watu kama hawa biblia inasema japo dunia itaona kama hiyo njia ya kujizuia na mambo yao ni ngumu, lakini Mungu yeye mwenyewe ndiye atakaye wapa NGUVU mpya ya kupaa juu, Mungu atawapa nguvu ya kuendelea kuishi maisha ya kujitakasa kila siku. Utakatifu kwao hautakuwa mgumu kuutimiza japo watu wa nje wataona inawezekanaje kanaje kwao wao kuishi vile?.

Na itaendelea vivyo hivyo mpaka siku ile ya kuipokea ahadi yake hapa duniani na katika siku ile ya UNYAKUO.

Pale Mungu atakapomnyeshea mvua zote mbili, yaani mvua ya masika na mvua ya vuli

Ni kwa nini Bwana anataka sisi tumngojee? Je! ni kwa lengo la kututesa?. Jibu ni hapana. Bali ameruhusu tukipitie hicho kipindi ili kututengeneza sisi, tuweze kuzimudu wingi wa hizo Baraka na hizo AHADI alizoziweka mbele yetu.

Zaburi 37: 9 Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.

Bwana alipowatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri, hakuwafikisha moja kwa moja katika nchi ya AHADI, badala yake aliwapitisha kwanza nyikani katika kipindi cha kumngojea yeye kwa muda wa miaka 40, kuwapa sheria itakayowasaidia kuitawala ile nchi ili iwazalie wenyewe. Jaribu kufikiri kama moja kwa moja baada ya kutoka Misri wangeingia kaanani ni kitu gani kingetokea?. Ni wazi kuwa wangeingia na miungu waliyotoka nayo Misri katika nchi takatifu, wangekuwa na tabia zao za uuaji, uchawi, visasi nk.. katika nchi ambayo Mungu ameibariki wao wangeifanya kuwa laana. Lakini iliwapasa wapitie kipindi Fulani cha kumngojea Mungu ili siku watakapofika waingie na kanuni za kuwasaidia kuishi mule.

Lakini tunasoma wengi wao hawakuwa wavumilivu kumngojea Mungu, wakaanza kurudia mambo ya Misri ambayo walishayaacha zamani, wakaona mbona nchi yenyewe ipo karibu lakini miaka hii yote hatuifikii, hivyo wakakata tamaa na kuasi kama tunavyosoma. katika

Zaburi 10: 7 Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu.

8 Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu.

9 Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda.

10 Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao.

11 Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao.

12 Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.

13 Wakayasahau matendo yake kwa haraka, HAWAKULINGOJEA SHAURI LAKE.

14 Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani.
15 Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao.

16 Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa Bwana.

17 Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu.

18 Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya.

19 Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

20 Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.

21 Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri.

22 Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.

23 Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.

24 Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake.

25 Bali wakanung’unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya Bwana.

26 Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani,

27 Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali.

28 Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu.

29 Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia.

30 Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa.

31 Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.

32 Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao,

33 Kwa sababu waliiasi roho yake,…..”

Hivyo kaka/dada, ikiwa wewe umeshakuwa mkristo, usichoke kumtazama Bwana, usichoke kumngojea Bwana ukayatamani mambo uliyoyaacha nyuma, mngojee Bwana baki katika hali hiyo hiyo ya utakatifu mpaka Bwana ajapo, faida zake utaziona utakapoingia katika nchi yako ya Ahadi pale Bwana atakapokuangazia rehema zake ukiwa hapa duniani kwanza, na kisha baadaye kule mbinguni utakapong’aa kama JUA.

Biblia inasema;

Maombolezo 3: 25 ”Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.

26 Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu”.

Usibabaishwe na chochote, usiyumbishwe na ulimwengu huu wala mambo ya ulimwengu huu kwasababu yanapita.Lakini wote wamngojeao Bwana watadumu milele.

Zaburi 27: 14 Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share ” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.

WALIOITWA NI WENGI, ILA WATEULE NI WACHACHE.

TUKAZE MWENDO ILI TUUFIKILIE UTIMILIFU.

NI KWA NINI TUNASEMA TUNAMWABUDU MUNGU ALIYE HAI ,JE! WALE WANAOMWABUDU SHETANI SIO MUNGU WAO ALIYE HAI?

KWANINI MUNGU ANAMPA NABII HOSEA MAAGIZO YA KUMUOA MWANAMKE KAHABA? (HOSEA 3)


Rudi Nyumbani

Print this post

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

Moja ya dhambi zinazowaangusha wengi ni “kutokusamehe”. Na hii inatokana mara nyingi na kutokuelewa nini maana ya msamaha. Ni rahisi kujilazimisha kusamehe lakini kama msamaha haujatoka ndani basi huo sio msamaha.

Ili kuelewa vizuri, tuchukue mfano una mtoto mdogo labda wa umri wa miaka 6 hivi, ukamkuta siku moja kachukua takataka kaweka ndani ya Friji, kwa namna ya kawaida ni lazima utakasirika na kuamua kumuadhibu ili kwamba siku nyingine asirudie…lakini je! Baada ya kumwadhibu utamwekea kinyongo?..Ni wazi kuwa hutamwekea kwasababu unajua ni mtoto tu! Laiti angefikia umri Fulani wa kujielewa asingefanya hivyo. Kwahiyo unamsamehe tu! Kwasababu unaelewa ni utoto tu ndio ulio ndani yake! Ndio unaomsumbua. Huwezi kwenda huku na kule na kwenda kutangaza kila mahali kwamba mwanao ni mbaya na kuanza kumchukia na kumwekea uadui.

Sasa usingeweza kuamua kumsamehe kabisa kutoka ndani ya moyo wako kama usingeelewa sababu ya kina ya yeye kufanya vile. Na ulipogundua kwamba sababu ni UTOTO ndipo ulipoamua kumsamehe kabisa kabisa.

Kadhalika tunapokuwa wakristo hatuwezi kusamehe watu wanaotuudhi au wanaotufanyia ubaya kutoka ndani ya mioyo yetu,kama hatutaelewa sababu ya wao kutufanyia huo ubaya ni ipi.

Leo tutajifunza sababu kubwa ya watu kutufanyia ubaya, au kutuudhi, au kutuumiza, au kutupangia mabaya, au kutuonea au kutufanyia chochote kile ambacho hakistahili kufanyiwa. Ambayo ukiielewa hiyo itakufanya uweze kumsamehe mtu kutoka ndani ya moyo wako kabisa.

Na sababu hiyo si nyingine zaidi ya DHAMBI ndani ya Mtu.

Mtu yoyote ambaye hajampa Bwana Yesu maisha yake, anakuwa ni milki ya shetani asilimia 100, Na kama anakuwa ni milki ya shetani, tunajua matunda ya shetani ndani ya mtu, ni yapi, Mwovu akiwa ndani ya mtu, Yule mtu lazima atakuwa ni mtu wa chuki, ni lazima atakuwa ni mtu wa kiburi, ni lazima atakuwa ni mtu wa hasira, ni lazima atakuwa ni mtu wa matusi, ni lazima atakuwa mtu wa kujipenda mwenyewe na kujijali nafsi yake, na kujiona yeye ni bora kuliko mwingine,ni lazima atakuwa ni mtu wa mashindano, ni lazima atakuwa mtu wa shari siku zote, mtu wa majivuno na wa dharau, na wakati mwingine atakuwa hata muuaji, n.k Kwa ufupi tabia zote mbaya ambazo zinajulikana zitakuwemo ndani ya huyo mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake.

Sasa kama vile mtoto anapokosa, moja kwa moja unaelewa kabisa tatizo la Yule mtoto ni UTOTO uliopo ndani yake na laiti kama angekuwa mtu mzima asingefanya vile, Vivyo hivyo mtu yoyote ambaye hajampa Yesu Kristo maisha yake anapokutendea ubaya, anapokuonea wivu, anapokutukana pasipo sababu, anapokudharau, anapotafuta kukuangusha, anapokutegea mitego ya kila aina ili uanguke, anapokuchukia bure, anapokusengenya huku na huku, anapokuonea hasira, anapokuumiza kwa njia yoyote ile n.k Unapaswa uelewa kwamba tatizo sio yeye bali ni DHAMBI iliyo ndani yake, unapaswa uelewe laiti angekuwa Mkristo kweli kweli kama wewe asingefanya vile, laiti angekuwa amempa Bwana maisha yake asingekuwa na chuki,asingekulaani,asingekutukana, asingekuonea wivu n.k…

hivyo sio yeye bali ni ile dhambi iliyo ndani yake, Kama vile unavyoielewa hali ya mtoto mdogo anapofanya kosa vivyo hivyo unapaswa uielewa hali ya Mtu asiye ndani ya Kristo anapokukosea.

Ndio maana pale Kalvari Bwana Yesu hakutusamehe sisi kwasababu tu aliamua kutusamehe, au alituvumilia,hapana! bali alitusamehe kwasababu alijua hatujui tutendalo, Alijua laiti tungemjua yeye ni nani kwa wakati ule Tusengelimsulibisha pale msalabani. Alijua laiti tungefunguliwa macho yetu tusingefanya yale mambo…Hivyo alitusamehe katoka ndani ya moyo wake kabisa.

Sasa ukishindwa kuelewa haya, utajikuta kila mtu anakuwa adui yako, utashinda kuelewa tofauti ya mtu aliye ndani ya Kristo na mtu asiye ndani ya Kristo, utajikuta unakesha katika maombi ya kuangamiza maadui zako, utajikuta na wewe unaanza kulipiza mabaya badala ya mema. Utajikuta na wewe shetani amekuingia unaanza kuwa na chuki, unaanza kuwa msengenyaji, unaanza kulipiza visasi n.k

Hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako, anapokutukana, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokusengenya, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokuchukia, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokusaliti, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokutendea ubaya wowote ule, kwasababu unaelewa kabisa kwamba tatizo sio Yule mtu, TATIZO NI DHAMBI ILIYOPO NDANI YAKE, laiti angekuwa mkristo kweli kweli asingefanya vile, hivyo unachopaswa kufanya ni kuchukua hatua ya wewe kumwombea Bwana ampe wokovu ili Dhambi hizo ziondoke ndani yake, lakini sio kushindana naye…Kwasababu ukishindana naye huwezi kumbadilisha kuwa kama wewe, wala hawezi kuvutiwa na kile kilichoko ndani yako. Suluhisho pekee ni kumwombea Rehema na Neema mbele za Mungu.

Ndugu jifunze kusamehe kutoka ndani ya moyo, kwa kuelewa hali ya mtu aliyopo. Kama kuwa na maadui hakuna mtu aliyekuwa na maadui kama Bwana wetu Yesu Kristo, na maadui zake namba moja tulikuwa ni mimi na wewe. Tulimtemea mate…je! wewe katika maisha yako ulishawahi kutemewa mate kama yeye?.. tulimtukana na kumdhihaki, na zaidi ya yote tukampeleka msalabani na kumwaibisha..je! wewe katika maisha yako ulishawahi kuaibishwa hivyo? Lakini yeye hakuwahi kutuita sisi maadui zake.. zaidi sana alisema “Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo” na zaidi ya yote akatuita sisi tuliokuja kumwamini baadaye rafiki zake.

Kama Bwana Yesu alitusamehe madeni makubwa kama hayo, unadhani sisi tunapaswa tuwafanyieje wanaotukosea?..tunapaswa tufanye zaidi ya hapo. Bwana alisema mwenyewe kwamba sisi tusipowasamehe waliotukosea hata Baba yetu wa mbinguni hatatusamehe makosa yetu. Ikiwa na maana kuwa kama kuna mtu yoyote ambaye hatujamsamehe kwa dhati kabisa kutoka ndani ya mioyo yetu, na sisi hatutasamehewa dhambi zetu, hivyo ni ziwa la moto litakuwa linatungoja, na Kristo hawezi kuzungumza uongo.

Ndugu yangu, epuka maombi yakupiga maadui zako, epuka kupeleka mashtaka mabaya mbele za Mungu juu ya watu wanaokuudhi, au kukuumiza, usimtaje ndugu yako kwa ubaya mbele za Mungu, wala usimtakie shari, bali mwombee rehema..ili atubu awe mkamilifu, Biblia inasema katika

Mithali 24: 17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo; Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”

Unaona? Hapo Bwana hafurahii, kuanguka kwake mtu mwovu, wala hafurahii mashataka mabaya tunayompelekea dhidi ya watu wengine, maombi tunayopaswa kuomba mbele zake ni Bwana atuepushe na madhara yao lakini sio awapige, au awaue, au awalaani. Adui yetu mkubwa ni shetani na sio watu.

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa Moyo wa Rehema na Toba dhidi ya ndugu wanaotukosea.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KISASI NI JUU YA BWANA

VITA DHIDI YA MAADUI

OKOA BADALA YA KUANGAMIZA!


Rudi Nyumbani

Print this post