UPONYAJI WA ASILI

by Admin | 7 August 2020 08:46 pm08

Jina la Bwana libarikiwe.

Kuna kitu kimoja cha kipekee ambacho Mungu katuumbia sisi wanadamu “nacho ni uponyaji wa asili”

Huu uponyaji wa asili upo katika miili yetu na vile vile upo katika roho zetu. Na huo Uponyaji tumepewa bure wanadamu wote kama zawadi na Mungu wetu, na huo hauhitaji uwe mkristo au utumie jina la Yesu kuupata. Upo tu Mungu kauweka ndani ya kila mtu.

Kwamfano unapojikata na kisu mkononi kwa bahati mbaya, inaweza kukuchukua wiki kadhaa tu kupona na nyama yako ikarudi  vile vile, au unapoanguka na kuchubuka sehemu ya mwili wako, baada ya wiki kadhaa au mwezi Ngozi yako itakuwa imesharudia katika hali yake kama ilivyokuwa mwanzo, litabaki kovu tu lakini si jeraha!..

Kwahiyo ni kitendo cha muda tu..lakini mwisho wa siku utapona majeraha yako yote. Vinginevyo Mungu wetu asingeuweka huo uponyaji wa asili basi dunia ingekuwa ni jehanamu..pangekuwa si mahali pa kuishi.

Na katika roho ni hivyo hivyo, yapo majeraha ya rohoni ambayo mtu unaweza kuumizwa au kujiumiza mwenyewe. Majeraha hayo yanaweza kutokana na mambo Fulani Fulani ya kimaisha, na hayo pia Mungu kayawekea uponyaji wake wa asili…

Ndio maana unaweza ukakasirika sana sasahivi, ukapita muda kadhaa ile hasira inaanza kutulia na mwishowe inaisha kabisa… hapo ni uponyaji unafanya kazi yake.

Hivyo kama vile tunavyotumia njia za kuponya majeraha ya nje tutumie njia hiyo hiyo kuyatibu yale ya ndani.

Tukiumia kwa majeraha ya nje kama vidonda, huwa tunavisafisha vizuri, tunavipaka dawa na kisha tunavifunga..na kikubwa Zaidi tunahakikisha hatuvitoneshi, baada ya siku moja au mbili tunarudia tena hilo zoezi, mpaka mwishoni tunapona kabisa. Sasa zoezi hilo la kukisafisha na kukifunga na kuzuia kukitonesha ndilo litasaidia kidonda kile kipone haraka, lakini kisipofanyiwa matunzo hayo..basi hakitapona haraka, na matokeo yake kinaweza kuzidi kuwa kikubwa Zaidi na kutengeneza tatizo lingine likubwa zaidi.

Na majeraha ya ndani tunayaponya kwa njia hiyo hiyo. Pale tunapoumizwa na watu au mazingira Fulani kama wakristo, njia ni hiyo hiyo;

  1. Kwanza unaliosha jeraha lako: Maana yake unaondoa vitu vyote vya kando kando ambavyo vinaweza kukusababishia jeraha kuwa kubwa Zaidi. Hiyo ikiwapo kulikumbuka kumbuka lile tukio. Katika hatua hii bado maumivu utakuwa unayasikia.

  2. Unapaka dawa: Dawa ni Neno la Mungu; Hichi ni kipengele cha muhimu sana..Yapo maandiko mengi katika biblia yanayohusiana na hali unayopitia…Kama umeumizwa kwa kuaibishwa kwa kuzungumziwa maneno mabaya, vipo visa kama vyako katika biblia, kavisome hivyo ndio dawa ya majeraha unayopitia, kama umerushwa vipo visa vya waliorushwa katika biblia na Mungu akawaponya katika shida zao, kama ni tatizo kwa mume wako/mke wako, vipo visa vingi kama vyako katika biblia ambavyo Mungu aliwaponya watu n.k. Hiyo ndio dawa, n.k. Biblia inafariji, biblia inajengwa, biblia ina amanisha.

Yohana 8:32 “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”.

  1. Funga jeraha lako: Baada ya kupaka dawa (kwa maandiko), unalifunga jeraha lako,..Maana yake unasali (huu ni wakati wa wewe kufunga na kusali)…Neno la Mungu (ambalo ni dawa) linaambata na kufunga na kusali.. Unaposali unamzuia adui shetani, kukuletea majaribu ya kuzidi kuliongeza jeraha lako. Maombi ya kufunga yanaizuia sumu ya adui kuingia katika jeraha unalolipitia.(Mathayo 17:21)

  2. Usijitoneshe: Hii ni hatua ya mwisho..hakikisha hujitoneshi toneshi..hii ni ile hali ya kukumbuka kumbuka lile tukio na kulifikiri fikiri, jitahidi kwa kadri uwezavyo kutoliweka akilini.

Fanya hivyo siku ya kwanza, rudia tena siku zinazofuata, kila siku soma maandiko, funga, omba na usijikumbushe kumbushe…Kwa kufanya hivyo nakuambia ukweli..Haitapita kipindi kirefu utaona mabadiliko makubwa sana. Utapona majeraha yako ya muda mfupi sana. Kwasababu umeiwekea mazingira yanayofaa, ile nguvu ya uponyaji wa asili kufanya kazi ndani yako.

Lakini usipofanya hivyo..Utakuwa na majeraha ambayo hayaponyeki kila kukicha…Utaishi Maisha ya kuumia kila siku, na ya chuki, na ya vinyongo. Kila mtu utamwona ni adui yako, na kila Neno litakuwa linakuumiza. Utakuwa na majeraha ya miaka 20 iliyopita ambayo hayajapona bado! Utakuwa mtu wa kutokusamehe…Nakuambia ukweli sio mpango wa Mungu kuwa na majeraha ya rohoni kwa miaka 10..Ukiona una kinyongo, au bado unaumia kwa jambo lililotokea miaka 10 au 20 iliyopita..jaribu kutafuta suluhisho mapema..kwasababu kuna uwezekano nguvu ya msamaha haipo ndani yako, na jeraha unapozidi kuliacha huwa ndio linazidi kuwa kubwa kila siku na kuweza kuzaa tatizo kubwa Zaidi ya hilo.

Zaburi 38:5 “Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu”

Na sababu ya kutopona majeraha ndio hizo hapo juu kutofunga jeraha na kutoweka dawa!.. Unaweza kuwa unatatizo la kutopata mtoto, na ukasikia watu wanakusema vibaya..na hilo likawa ni jeraha kwako!..lakini kama Neno la Mungu halipo ndani yako; kama hujui Habari za akina Sara na wengineo ambao Mungu aliwafungua matumbo katika uzee wao, kama hujui Habari za Hana na Raheli ambao walisemwa kupita maelezo, basi hutaweza kupona haraka jeraha ulilonalo. Kwahiyo Neno la Mungu ndio dawa, inayoharakisha uponyaji wa ki-Mungu.

Zaburi 147:3 “Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao”

Ndicho kinachowakuta watu wasiolijua Neno la Mungu (watu wa kidunia), wanahangaika na majeraha ya muda mrefu yasiyopona kwasababu hawana dawa, wala hawaijui dawa..Hivyo jeraha lolote lililo ndani yako, lisiwe kikwazo cha wewe kuikosa mbingu anza sasa kuusafisha moyo wako.

Bwana akubariki.

Mwisho kama hujaokoka, wakati umeenda sana, wakati wowote Kristo anarudi, biblia inasema..itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima halafu tupate hasara za nafsi zetu?. Mambo ya ulimwengu yanapita lakini Neno la Mungu lipo pale pale. Mgueukie leo Kristo, utubu dhambi zako, uoshwe kwa damu yake, ukabatizwe na kisha upokee Roho Mtakatifu, ambaye atakuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko.

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

ALIJARIBIWA SAWASAWA NA SISI KATIKA MAMBO YOTE.

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

UTASIMAMA PEKE YAKO SIKU ILE.

JIRANI YANGU NI NANI?

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

WAKAKAA KWAKE SIKU ILE. NAYO ILIKUWA YAPATA SAA KUMI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/07/uponyaji-wa-asili/