UTASIMAMA PEKE YAKO SIKU ILE.

UTASIMAMA PEKE YAKO SIKU ILE.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe..karibu tujifunze mambo ya msingi katika safari ya haya maisha ya hapa duniani..biblia inasema dunia inapita, pamoja na tamaa zake zote, (1Yohana 2:17). Na siku ya hukumu siku moja itafika na kila mmoja atatoa habari zake mwenyewe…(Warumi 14:12).

Wengi hawajui kuwa siku ya hukumu itakapofika kila mtu atasimama mbele ya kiti cha hukumu akiwa peke yake pasipo mtu mwingine pembeni yake…utakuwa peke yako pasipo mzazi wako pembeni yako, wala dada yako, wala kaka yako, wala ndugu yako yoyote..Wala mzazi wako au ndugu yako hatakuwa na wewe pembeni yake..Kila mmoja atakuwa mwenyewe, na kutoa habari zake mwenyewe.

Kama uliishi maisha yanayostahili hukumu utahukumiwa kivyako, na kuzimu kule ni pa kubwa mno..nafasi ya mtu mmoja hadi nyingine haielezeki…Kuzimu ni kubwa kuliko hii dunia.. sasa hebu tafakari pamoja na idadi yetu yote tuliyopo bado haijajaa hata theluthi ukisafiri tu kilometa kadhaa kutoka hapo ulipo, tayari unakutana na mapori, yasiyo na watu…sasa kuzimu ni kubwa mara nyingi kuliko hii dunia..kiasi kwamba hata idadi yote hiyo inayoingia huko na watakaoingia hata nusu ya robo watakua hawajaijaza…ina nafasi ya kutosha..Biblia imesema kuzimu haishibi wala haitosheki kwa inayoyapokea…

Mithali 30:15 “Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!

16 KUZIMU; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!”

Kumbuka jambo moja unapokuwa katika mkutano wa Neno la Mungu na katika mkutano huo kuna watu elfu..kumbuka neno hili kwamba Mungu hazungumzi pale na nyie watu elfu kwa pamoja bali anazungumza na wewe binafsi. Huwa anapotoa onyo ni kama anaongea na mtu mmoja na si wengi.. Hebu tuzitafakari kidogo zile amri 10, ambazo Mungu alimpa Musa awape wana wa Israeli… Kila amri utaona ni kama Mungu anazungumza na mtu mmoja. Hebu tusome..

Kutoka 20: 2 “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

3 Usiwe na miungu mingine ila mimi”….

Hapo hasemi Mimi niliyewatoa katika nchi ya Misri..bali mimi “niliyekutoa”…maana yake anazungumza na mtu mmoja na si wengi..

Tukiendelea amri ya pili anasema..

“4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia”…

hapo tena ni vile vile hasema “msijifanyie sanamu za kuchonga”..bali anasema “usijifanyie”..kuonyesha kwamba anazungumza na mtu mmoja na si wengi…kwahiyo unapoona wengi wanasujudia sanamu usiwaige na kusema mbona tupo wengi..ina maana Mungu atatuhukumu wote?…Atakuhukumu wewe peke yako, kwasababu katika amri hii anazungumza na wewe na si wao..Siku ya hukumu hao hawatakuwepo na wewe…wewe utasimama peke yako..

Na amri nyingine zote zilizobakia ni hivyo hivyo…zinasema USIZINI, USIIBE, USIUE…na sio msizini, au msiibe, au msiue….Leo hii unapozini, siku ya hukumu hutasimama na yule uliyekuwa unazini naye….wala hutamwona…Utahukumiwa wewe binafsi na kutupwa kwenye lile ziwa la moto na huko pia utakuwa peke yako..yule uliyekuwa unazini naye hutamwona tena hata huko kuzimu hutasikia sauti yake…utakuwa peke yako.

Shetani lengo lake kubwa ni kuwapeleka watu kuzimu…kwa kuwatumainisha katika wingi wa watu…Kwamba kwasababu tupo wengi tunaofanya hivyo basi Mungu hawezi kutuhukumu wote..siku ile kwa pamoja ataturehemu…ndugu usidanganyike…ikumbuke ile gharika ya Nuhu, pengine wapo waliodhani hivyo kwamba Mungu hawezi kuihukumu dunia na kuifadhi familia mmoja tu ya Nuhu…lakini gharika iliposhuka wote walipotea na sasa hivi wapo kuzimu wakisubiria hukumu ya mwisho na kutupwa katika ziwa la moto..biblia inasema hivyo.

Na pia shetani anapenda kuwafariji watu kuwa hata mtu akifa na kwenda kuzimu leo basi kuna uwezekano wa kuombewa na watakatifu huku duniani na Mungu akakutoa kutoka kule kuzimu na kukuingiza paradiso… huo pia ni uongo wa Adui, usidanganyike!..ukifa leo katika dhambi na ukijikuta kuzimu huko hutoki tena, milele na milele utakuwa umepotea. Utauliza ni wapi imeandikwa hiyo?

Ayubu 7: 9 “Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, NI VIVYO HUYO ASHUKAYE KUZIMUNI HATAZUKA TENA KABISA.

10 Hatarudi tena nyumbani kwake, Wala mahali pake hapatamjua tena”.

Binti wa Mungu lisikie hili Neno la Mungu linalokuonya leo..suruali unazovaa, vimini unavyovaa, hereni unazizovaa, ngozi unayojichubua, kwasababu unahisi tu mbona mpo wengi mnaofanya hivyo? Mbona hata mhubiri wako anavaa hivyo?…Sikia leo neno la Mungu…siku ile itakuwa peke yako!! Hatakuwepo mhubiri wako pembeni, wala ndugu yako ambaye alikuwa anavaa kama wewe…wala mimi sitakuwepo!..utakuwa wewe na yeye na kitabu chake cha maneno yake…na kitabu cha maisha yako.

Kijana ambaye unabet, unayeshabikia mipira na kuifanya ndio miungu yako..unapata dakika 90 za kuitazama mpaka inaisha lakini kulitazama neno la Mungu dakika kumi macho yanafumba…Neno linasema “usiwe na miungu mingine ila mimi”..sio msiwe na miungu mingine…Ni wewe ndio unayeambiwa hapo…na pia ni mimi ndiye ninayeambiwa…lakini si wote wawili tunaoambiwa kwa pamoja…

Hivyo tubu leo kama hujatubu…siku ni chache sana zimebaki za kuondoshwa watakatifu wa Mungu ulimwenguni…na saa yoyote ile parapanda ya mwisho italia na watakatifu wataondoshwa kupelekwa mbinguni, kitakachosalia ulimwenguni ni dhiki kuu ya mpinga-kristo na hukumu ya siku ya Bwana inayotisha.

Tubu leo ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi zako na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu.

Kuzimu ipo!!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE WAKRISTO TUNARUHUSIWA KUSHEHEREKEA VALENTINE’S DAY?

USISUBIRI MPAKA MUNGU AKUAMBIE, NDIO UFANYE!

Jehanamu ni nini?

NI NANI ALIYEIDHARAU SIKU YA MAMBO MADOGO?.

KAMA ZILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU NA ZA LUTU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments