USISUBIRI MPAKA MUNGU AKUAMBIE, NDIO UFANYE!

USISUBIRI MPAKA MUNGU AKUAMBIE, NDIO UFANYE!

Unajua ni kwanini Daudi alipewa jina kuu na kubwa kuliko wafalme wote na watu wote waliomtangulia katika Israeli? Ni kwasababu kuna kipindi aliwaza, Mungu amenipa vyote, amenipa ufalme, amenipa uongozi bora juu ya Israeli yote, amenipa nyumba nzuri ya kukaa, lakini mbona ni mimi tu ananifanyia wema, na mimi simfanyii chochote?. Akatazama huku na kule, akaangalia ni wapi pamepunguka, akagundua kuwa Mungu hana maskani yoyote ya kukaa, akatazama akaona lile sanduku la agano la Mungu linakaa kwenye mapazia, katika giza nene (1Wafalme 8:12) kwenye vihema vilivyochoka na kuchakaa..

Akajiwazia tu moyoni akasema hii haiwezekani, nitamjengea Mungu nyumba ya kukaa..

Lakini biblia inatuambia usiku huo huo Neno la Mungu lilimfikia Nadhani nabii wa Mungu, kwa Daudi kumwambia kwamba Mungu anasema: Je nilishawahi kusema Neno lolote kwa mwamuzi yoyote wa Israeli juu ya kujengewa mimi nyumba? Nilishawahi kumdokeza Yoshua juu ya jambo hilo? Nilishawahi kumdokeza Gideoni kuhusu kunijengea nyumba, Au Samsoni, au Ehudi au Yeftha, au Samweli juu ya jambo hilo?

Kwa namna nyingine Bwana alikuwa anamaanisha kumwambia Daudi hivi..

Sikuwahi kuwauliza chochote, ili nisionekane kama nawalazimisha, bali niliwaacha wao wenyewe waligundue hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyelijali jambo hilo isipokuwa wewe Daudi, Sasa Basi kwa kuwa umefikiria hivyo, kunipa heshima, kunitoa katika giza nene, kwenye vihema vibovu, mimi nami nitakupa jina kuu sana, na sehemu nzuri Zaidi.

2 SAMWELI: MLANGO 7

1 Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,

2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe. 4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,

5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?

6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.

7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?

8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;

9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; NAMI NITAKUFANYIA JINA KUU, KAMA JINA LA WAKUU WALIOKO DUNIANI”.

Na tunaona Daudi alianza maandalizi yote ya ujenzi wa hekalu la Bwana, na mwanawe Sulemani akaja kulimalizia..

Sasa leo hii sisi ndio tunaojua vizuri ni jinsi gani Mungu amempa Daudi jina kuu kuliko wengine wengine wote waliomtangulia.. (hata Bwana wetu Yesu katokea katika huo huo uzao wa Daudi katika mwili) Lakini hiyo yote ni kutokana na kwamba hakusubiri aambiwe ndipo afanye..

Hata leo hii, zipo kazi Mungu nyingi sana zimepwaya, Na Mungu amekaa kimya anaangaalia, wala hasemi chochote, Ni kweli ataendelea kuwa na sisi kama Watoto wake, kama watumishi wake, atatutumia sisi kama manabii wake, mfano wa Samweli, Lakini kama hatutachunguza na kuchukua hatua ni wapi palipopunguka, tusitazamie kamwe kama Mungu siku moja atakuja kutuambia naomba unifanyie hiki au kile.

Vivyo hivyo ikiwa wewe umeokoka, na unajua kabisa ni jukumu lako kumtolea Mungu, kamwe usidhani ipo siku Mungu atakuuliza mbona hujanitolea, au mbona hujanifanyia hichi au kile….hilo jambo hawezi kufanya kabisa, wewe ndio unapaswa ulitambue hilo si yeye.

Unajua kabisa unapaswa ukaisambaze injili kwa wengine kwa karama Mungu aliyoiweka ndani yako, halafu unasubiria siku moja Mungu akutokee akwambie nenda kahubiri, hilo wazo lifute kabisa, ni rahisi kumwambia yule ambaye ndio kwanza anaingia kwenye wokovu lakini wewe ambaye umeshakaa miezi, na miaka,na huna ushuhuda wowote, unasubiri siku moja Mungu akuambie uipeleke Habari njema katika maono, hawezi kufanya, kwasababu anajua kabisa unajua jukumu lako, kwanini tena akuambie, si itakuwa kama anakulazimisha?..

Pale tunapochukua hatua ndipo hapo Mungu anatuongezea na hatua nyingine..(Usisubiri mpaka Mungu akuambie)

Hivyo siku ya leo ya tarehe hii na mwezu huu, biblia inatufundisha kuwa na jicho kama la Daudi, ili na sisi pia Bwana atupe jina lililo huku na kule ng’ambo tutakapofika.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

Kwanini Mungu anasema “Afanyaye malaika zake kuwa pepo”?

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

KUOTA MTU AMEKUFA/NDUGU AMEKUFA.

Ni kura ya aina gani waliipiga wale watu waliosafiri na Yona?

JE MUSA ALIFIA WAPI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas mhula
Lucas mhula
2 years ago

Amina mtumishi wa Mungu nimebarikiwa sana na ujumbe