Utauliza je “tumbo” linaweza kuwa “mungu”? jibu ni Ndio, maandiko yanasema hivo..
Wafilipi 3:19 “mwisho wao ni uharibifu, MUNGU WAO NI TUMBO, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani”.
Na kama tumbo ni mungu, basi maana yake anaabudiwa na pia anatumikiwa.
Yafuatayo ni makundi mawili makuu ya watu wanaoabudu tumbo, aidha kwa kujua au kwa kutokujua.
1. Manabii wa Uongo.
Hili ndilo kundi la kwanza linaloabudu “tumbo” (kwa kujua kabisa).. Hawa wapo tayari kupotosha maandiko ili tu wapate kushibisha matumbo yao, wapo tayari kuzunguka kote kote kuwalaghai watu kiroho ili wapate fedha kutoka kwao.
Hawa biblia imewataja kwamba hawamtumikii Bwana YESU bali matumbo yao wenyewe..
Warumi 16:18 “Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, BALI MATUMBO YAO WENYEWE; NA KWA MANENO LAINI NA YA KUJIPENDEKEZA WAIDANGANYA MIOYO YA WATU WANYOFU”.
Kundi hili la watu, chochote kile kilichoandikwa kwenye biblia kwao ni fursa ya kupata pesa..wapo tayari kutumia chochote kile na kukupatanisha na biblia lengo si kujenga roho za watu bali kutoa pesa kutoka kwa watu, wanaweza kutumia picha, nguo, maji, mafuta na viungo vingine vyote ili mradi tu kuvuna mali kutoka kwa watu, ili washibishe matumbo yao.
Hawa madhabahu zao ni matumbo yao, shetani ameketi katika matumbo yao..na hawawezi kuishi bila kuyatumikia matumbo. Hawa biblia imetuonya tujihadhari nao, kwani kukuua kiroho wenyewe hawaoni shida.
2. Wakristo vuguvugu.
Hili ni kundi la pili la waabudu matumbo.. Hawa ni wale ambao hawawezi kuitawala miili yao katika eneo la kula, ni wale watu ambao maisha yao hawajawahi kufunga, au kama walifunga basi hawakumbuki ni lini kwasababu ni zamani sana walifanya hivo.
Ni wakristo wa kupenda kuombewa tu, hawawezi wenyewe kutenga muda kufunga na kuomba.. kwani wakijaribu kufanya hivyo wanaona kama wanakufa “roho inawatoka”.. Wanalisha matumbo yao mara tatu kwa siku, mwaka mzima, na wakikosa chakula kidogo tu ni watu wa kunung’unika, kulalamika na kuhisi kama wameonewa sana.
Hawa ni watu wanaoabudu tumbo pasipo kujua. Wakidhani kwamba kwasababu tumeruhusiwa kula, basi kila wakati ni lazima kula, pasipo kufahamu kwamba Bwana YESU alisema mambo mengine hayatoki (yani hayawezekani) pasipo kufunga na kusali.
Mathayo 17:21 “[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]”
Hili ni kundi la watu linalopenda karamu za ulafu za kula kula…kukitokea hafla fulani, au pati, au sherehe au harusi huwa halikosi!.. linaweza kuchangia kila aina ya gharama ilimradi tu lisipitwe na shughuli, lengo kubwa ni chakula.
Mpendwa kama huwezi kulitawala tumbo, fahamu kuwa tumbo lako ni mungu wako hata kama hukiri hivyo!
Roho Mtakatifu aliwahi kunifundisha jambo kuhusu tumbo…
“Wakati fulani nilikuwa katika mfungo, na siku niliyopanga kumaliza, Roho mtakatifu aliniambia niongeze siku nyingine moja mbele, wakati nawaza hilo kama vile najiuliza uliza, kutokana na uchovu wa mwili, akaniambia toka nje tembea na nitapata nguvu, nikatii na kutoka nje na kutembea na nilipokuwa natembea mwili ulianza kupata nguvu, na nikasikia tafakari nyingi za kimaandiko zikipita ndani yangu, wakati naendelea na matembezi nilifika mtaa mwingine ambapo kuna nyumba kubwa sana ya kifahari na nje ya nyumba hiyo hapo getini, kuna kibao kidogo kimeandikwa maneno haya “bwana tumbo estate, niliposoma kibao hiko ambacho labda kilikuwa kinamtambulisha mmiliki wa nyumba hiyo, nilielewa pale pale ni nini Roho Mtakatifu alichokuwa ananiambia, kwamba “tumbo” la mtu ni bwana, kwa kifupi ni mungu” na kila anayelitumikia litampoteza kabisa, na kumfanya akose uzima wa milele”.
Na ndio maana siku za mwisho tumbo litatoweshwa..
1Wakoritho 16:13 “Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili”.
Kama mkristo uliyeokoka hakuna sifa yoyote unayopata kwa kula sana, wala chakula hakikusogezi karibu na MUNGU..
1Wakorintho 8:8 “Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu”.
Kama mkristo ni lazima ujifunze kulitawala tumbo, na si tumbo likuendeshe wewe, ni aibu kwa mkristo kumaliza mwezi haujafunga..hata hivyo kila wiki ni lazima uwe na angalau siku moja ya kufunga, tabia ya mkristo kusema kufunga ni mpaka uongozwe hatuipati katika maandiko, kama vile tunavyoikosa kanuni ya kula mara tatu kwa siku.
Ni kweli ni halali kula, hata mara tano kwa siku lakini si tabia inayofaa..
1Wakorintho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote. 13 Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili”.
1Wakorintho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.
13 Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili”.
Je umeokoka?.. Una uhakika Bwana YESU akirudi leo utakwenda naye?.. Kama bado haujaokoka fahamu kuwa muda umeenda kuliko unavyodhani muda wowote parapanda ya mwisho inalia, na wote walio nje ya Kristo watahukumiwa.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
UVUKISHE MIPAKA UPENDO WAKO.
JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?
Kwa namna gani mauti ya wacha Mungu ina thamani machoni pake? (Zaburi 116:15).
JE! UMEFIKIA VIGEZO VYA KUWA BABA ROHONI?
Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?
Save my name, email, and website in this browser for the next time I comment.
Δ