Swali: Je ni kwamba Mungu anafurahia Mauti ya watu wake mpaka aseme hivyo?
Jibu: Turejee mstari huo…
Zaburi 116:15 “Ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake”
Sasa ili tupate vizuri maana ya huu mstari hebu tuweke msingi kwa kusoma tena mstari ufuatao…
Ezekieli 33:11 “Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, SIKUFURAHII KUFA KWAKE MTU MWOVU; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?”
Kama Bwana hakufurahii kufa kwake MTU MWOVU, basi kinyume chake ni kweli!! kuwa “KUFA KWAKE MTU MWENYE HAKI ikiwa amemaliza kusudi lake duniani NI JAMBO LINALOMPENDEZA MUNGU”… Na Ndio hapo kwenye Zaburi 116:15 anasema “Ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake”.
Sasa kwanini MAUTI YA WENYE HAKI NI YA THAMANI MACHONI PA MUNGU?
1. DUNIANI NI MAHALI PA DHIKI.
Hii ndio sababu KUU..Duniani si mahali pa raha kwa “Wanaomcha Mungu”.. Kwa wengine wasiomcha Mungu panaweza kuwa mahali pao kwa raha ya kitambo..lakini kwa wacha Mungu si sehemu ya faraja hata kidogo..
Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. ULIMWENGUNI MNAYO DHIKI; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.
Kutokana na kwamba ulimwenguni ni mahali pa dhiki, na tena pa mapito, ni mahali pa kutaabika kupambana na dhambi na kutaabika kuhubiri injili.. hivyo MAUTI ni sehemu ya mapumziko kwa wanaomcha Mungu kutokana na taabu hizo za ulimwengu…ndivyo maandiko yanavyosema..
Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, HERI WAFU WAFAO KATIKA BWANA TANGU SASA. NAAM, ASEMA ROHO, WAPATE KUPUMZIKA BAADA YA TAABU ZAO; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao”.
Hiyo ndiyo sababu kwanini KIFO ni sehemu bora kwa WANAOMCHA MUNGU KULIKO KUENDELEA KUSHI DUNIANI. Na Mkristo yeyote yule wa kweli, ni lazima atamani kuondoka katika haya maisha kuliko kuendelea kubaki hapa!!, ni lazima atamani kila siku ile siku ya unyakuo ifike, au siku ya kulala kwake (kufa) ifike akamwone Bwana.
Kitu pekee ambacho kinapaswa kutufanya tuendelee kutaka kubaki duniani ni “kuimaliza kazi yake”, (maana yake tusiondoke kabla ya kuimaliza kazi yake aliyotuitia, kwani kuna hatari ya kufa bila kuifanya kazi yake au kuimaliza).. na hakuna sababu nyingine tofauti na hiyo…
Ukiona unatamani uendelee kubaki duniani, ili uwe milionea, au ili uendeshe na kumiliki magari, au utengeneze majumba kwa fahari yako, kuna shida katika Imani yako!..(Ni muhimu kujipambanua upya).. wewe utakuwa wenyeji wako ni hapa duniani, sio mbinguni.
Walio wa mbinguni wanatamani ya mbinguni, na walio waduniani wanatamani, na kuwekeza, na kusifia vya duniani…
Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo”
Soma pia 1 Petro 2:11 utaona jambo hilo, hivyo jihakiki ni nini kinakupa sababu ya wewe kuendelea kubaki hapa duniani?..ni vitu vya dunia hii au vile vijavyo?.
Mtume Paulo kwa ufunuo wa Roho aliandikia kuwa “kuishi kwake ni Kristo na kufa ni faida”,..Maana yake kusudi lake kuu la kuendelea kubaki duniani ni Kristo (yaani kufanya kazi Kristo aliyomuitia na kuimaliza)..Nje na hapo kufa ni FAIDA KUU!
Wafilipi 1:21 “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni KRISTO, NA KUFA NI FAIDA.
22 Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui.
23 Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana;
24 bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu”.
Hapo anasema kudumu katika mwili (yaani kuendelea kuishi) kwahitajika kwaajili yao, na si kwaajili yake (maana yake kwaajili ya kuwahubiria wao injili).
Je mimi na wewe kubaki kwetu katika mwili kwahitajika kwaajili ya nini??…je ni kwaajili ya matumbo yetu, na tamaa, na anasa au kwaajili ya Bwana?..
Kumbuka pia, ni hasara kubwa sana kufa katika dhambi!.. na hakuna maombi yoyote ya kumtoa mtu aliyekufa kutoka katika mateso ya moto wa jehanamu na kumingiza paradiso. (Hayo maombi hayapo usidanganyike).
Hakuna maombi yoyote ya Mchungaji, au Askofu, au Nabii, au Mtume, au Papa, au Padre, au Kadinali, au Mwalimu, au Rabi, au Mwinjilisti, au Kuhani au Malaika wa mbinguni…. yatakayomtoa mtu kwenye mateso ya moto wa jehanamu na kumwamisha kumwingiza peponi, Mtu akifa katika dhambi!, habari yake ndio imeishia hapo..
Bwana YESU Kwa kinywa chake mwenyewe ametupa tahadhari hiyo katika kitabu cha Yohana..
Yohana 8:24 “Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU”.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!
UMEFUNGWA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI?
WAANDAA MEZA MBELE YANGU, MACHONI PA WATESI WANGU
About the author