MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA MATHAYO.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA MATHAYO.

(Hotuba za Yesu)

Kitabu cha Mathayo ni moja ya vitabu vinne (4), vya injili. Yapo mambo mengi ya kujifunza ndani yake, lakini katika makala hii, tutaona mambo muhimu ya kufahamu ambayo yatakusaidia katika usomaji wako.

Tukiachia mbali matukio, na huduma mbalimbali ikiwemo za uponyaji alizozifanya Yesu. Tunafahamu kuwa Bwana “ALIFUNDISHA” pia. Na hapa ndipo kiini cha kujifunza kwetu.

Hivyo katika kufundisha kwake, kuligawanyika mara mbili. Kuna taarifa ambazo alizotoa bila kutolea maelezo mengi, lakini pia kuna taarifa alizitoa kama hotuba.

Sasa tutaangazia hizo HOTUBA, ambazo zimerekodiwa kwenye kitabu hichi.

Zipo tano (5), Nazo ni

  1. Hotuba ya Mlimani. (Mathayo 5-7)
  2. Hotuba ya utume (Mathayo 10)
  3. Hotuba ya ufalme wa mbinguni (Mathayo 13)
  4. Hotuba ya kanisa (Mathayo 18)
  5. Hotuba ya siku za mwisho (Mathayo 24)

Kabla ya kuziangalia kwa upana kidogo. Tufahamu kwanza hapo tusemapo “hotuba” tunamaanisha nini.

Hotuba ni mahubiri/mafundisho aliyoyasema Yesu kwa upana, yaliyolenga mada Fulani maalumu.

Ni mazungumzo marefu ya Bwana Yesu. kukazia jambo lile lile moja. Sasa embu Tuangalie kiini cha kila hotuba.

1) Hotuba ya mlimani. (Mwenendo wa Mkristo)

Hii tunaisoma katika sura ile ya 5,6,7. Ni wakati ambapo Bwana Yesu alipanda mlimani, kisha wanafunzi wake wakamfuata, akaanza kuwafundisha mambo mengi. Sasa kiini cha hotuba hii, kilikuwa ni kuwafundisha mwenendo sahihi wa Mkristo, unaokubaliwa na Mungu.

Anaanza kwa kusema HERI, HERI, HERI, maskini wa roho, wapole, wenye rehema, wapatanishi, wenye moyo safi, wenye kiu na njaa ya haki, n.k. anaendelea jinsi tunapavyopaswa tuwapende maadui, tusamehe, tusilipize kisasi, akafundisha usahihi wa kuomba, kufunga, kutoa sadaka, usafi wa moyo, na upendo, na mambo mengine kadha wa kadha.

Ni maneno ambayo kama wewe ni mwamini basi unapaswa uyasome na kuyatafakari kila inapoitwa leo. Kwasababu Huu ndio uliokuwa mwenendo wa Yesu duniani. Akahesabiwa kumpendeza Mungu kabla hata hajaanza huduma yake ya kuhubiri, kwasababu aliishi aliyokuwa anayasema. Hivyo siri iliyopo hapa ni kwamba alikuwa anasema mwenendo wa maisha yake yalivyokuwa.

Na sisi pia tukitaka tufanane, na Kristo kimwenendo na tabia, basi tuzingatie sana, kuyaaishi haya tunayoyasoma katika sura hizi tatu yaani 5,6,7, Ni muhimu sana, sio kuimba “natamani kufanana na wewe”, lakini hatujui tunafananaje na yeye.

2) Hotuba ya Utume (Mathayo 10)

Katika mahubiri haya, Bwana Yesu aliwaita wanafunzi wake na kuanza, kuwapa maelezo ya namna ya kuhubiri kule atakapowatuma. Akawaeleza kwa upana jinsi mazingira ya kuhubiri yalivyo, kwamba kuna mahali pia hawatakubalika, akawafundisha pia jinsi ya kuhubiri, akawaondoa hofu ya wanadamu, na hofu ya kusumbukia mahitaji kwamba huko huko mbele ya safari Bwana atakuwa nao, akawafundisha pia mahali pa kuanzia kuhubiri, akawafundisha hekima ya kuhubiri, na kuponya watu. Na mambo mengine kadha wa kadha.

Kiasi kwamba, wewe kama mtendakazi katika shamba la Bwana ukisoma habari hizi, zitakusaidia katika ustahimilivu wako shambani mwa Bwana, tukikumbuka kuwa kila mmoja wetu ameitwa na Bwana kwenda kuwafanya wengine kuwa wanafunzi. Hivyo, Usomapo habari hii ya kitume, itakusaidia kunoa vema utumishi wako, katika eneo la upelekaji kazi ya Mungu mbali. Pata nafasi pitia wewe mwenyewe kwa utulivu sura yote ya kumi. Bwana atakupa kuelewa mengi ndani yake. Na hivyo utakuwa mtume, kama mitume wako walivyokuwa.

3) Hotuba ya ufalme wa mbinguni (Mathayo 13)

Hii ni hotuba, iliyohusu siri za ufalme wa Mbingu. Ambapo Bwana Yesu alitumia mifano (mafumbo), kuulezea. Biblia inaposema ufalme wa mbinguni, inamlenga YESU mwenyewe, na kazi yake aliyokuja kuifanya duniani (Luka 4:18-19).

Katika sura hii ya 13, alieleza mifano mikuu saba (7), japokuwa kulikuwa na mengine aliyokuwa iliyohusu ufalme wa mbinguni isipokuwa haijarekodiwa katika kitabu hichi. Mfano wa kwanza ulikuwa ni wa mpanzi, kisha magugu na ngano, kisha chembe ya haradali, kisha chachu katika unga, kisha hazina iliyositirika katika shamba, kisha mfano wa mfanyabiashara na lulu, na juya lililotupwa baharini.

Katika mifano hii yote, maudhui ni kuonyesha ukubwa ulio ndani ya Kristo Yesu, pale mtu anapomwamini na kustahimili kumfuata ukweli ni kwamba ataanza kama chenye ya haradali, lakini ataishia mti mkubwa, ni kama aliyepata hazina na lulu kubwa sana, akaenda kuuza akawa tajiri,.

Hivyo usomapo kwa makini mifano hii, utakuwa na kila sababu ya kuutafuta sana ufalme wa Mungu (yaani Kumuhufadhi Kristo sana moyoni mwako). Kwasababu unajua ulichokitapata ni zaidi ya vitu vyote duniani. Ambavyo utakuja kuvifurahia vema uendapo kule ng’ambo mbinguni.

4) Hotuba ya kanisa (Mathayo 18)

Hotuba hii inalenga, namna ya kuchukuliana sisi kwa sisi (Kanisa), tuliomwamini Yesu katika eneo la kujishusha na kunyenyekeana, kutokwazana, kutokupuuziana, lakini pia kuwa tayari kuwatafuta wale waliopotea na kuwarudisha kundini, ni muhimu sana, akatoa mfano wa mtu aliyeacha kondoo wake tisini na tisa, na kwenda kumtafuta Yule mmoja aliyepotea. Na sisi yatupaswa tuwe na moyo huo wa kichungaji.

Vilevile kusameheana sisi kwa sisi hata saba mara sabini akatoa mfano wa Yule mtu aliyesamehewa talanta elfu kumi, lakini yeye hakuwa tayari kumsamehe aliyemdai dinari mia, pia alifundisha njia nzuri ya kuonyana kingazi kufatana na utaratibu kwa kikanisa.

Hivyo usomapo hotuba hii, utafahamu namna ambavyo Bwana anataka sisi tuishi kama ndugu tuwapo pamoja kama kanisa lake.

5) Hotuba ya siku za mwisho (Mathayo 24)

Hii ni hotuba inayohusu, matukio yote ya siku za mwisho wa dunia, na kurudi kwa Yesu kutakavyokuwa, anaeleza kwa urefu dalili zake, mabadiliko ya kimwenendo ya watu, yatakavyokuwa, majanga ya asili, na vita vitakavyofuata baadaye, anatoa tahadhari ya manabii wa uongo, unyakuo wa kanisa, dhiki kuu na mapigo ya Mungu, Na mwisho anatoa angalizo ni nini tunapaswa tufanye. Kwamba “Tukeshe”, kwasababu hatujui siku wala saa.

Hotuba hii ni vizuri ukaisoma kwa urefu, na kuelewa kwa undani, kwasababu nyakati tulizopo sasa, tupo katika “mwisho wa siku za mwisho.” Dalili nyingi zilizotabiriwa zilishatimia. Jiulize umejiandaaje kwa yaliyo mbele yetu?

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa, ufahamupo Mahubiri hayo (Hotuba), utapata uelewa wa undani kimaudhui ndani ya kitabu cha Mathayo, Jifunze kusoma sana, na kurudia rudia, hotuba hizi, kulikuwa na sababu kwanini Bwana atoe habari zake kwa urefu, kwasababu ndio “Fundisho” la mwamini. Zingatia hayo na Bwana akubariki.

Tutakuwa na uchambuzi wa vitabu vingine..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments